WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Friday, June 10, 2016

TOBA YA KWELI



June 10

Matendo ya Mitume 2:38

Tafakari ya leo inatukumbusha umuhimu wa kufanya Toba ya kweli; Kufanya toba maana yake ni kufanya mageuzi katika akili yako na katika tabia yako. Toba mara nyingi inahusisha mageuzi ya kuacha dhambi na kumrudia Mungu. Hapo tunatakiwa kubadilisha akili zetu jinsi tunavyofikiri na kutenda; kubadili mtazamo wetu na hivyo itatusaidia kubadilisha tabia zetu ambazo kabla ya Toba zilikuwa mbaya. Ni mabadiliko ya jinsi tunavyoishi kutoka katika njia ambayo sio sahihi ambayo inakwenda kinyume na maagizo ya mungu. Kwa maneno rahisi kabisa Toba ni kuyaweka maisha yetu chini ya ulinzi wa Mungu na kutenda na kuishi kadiri ya maelekzo yake na maagizo yake. Matendo ya Mitume 3:19 Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa  tukiangalia mafundisho ya Yohana Mbatizaji tunaona jinsi gani alikuwa anafundisha kuhusu kutubu na kubadilisha tabia zetu za kibinadamu ili ziendane na Tabia za Kimungu. Tukisoma Luka 3: 10-14 Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.  Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu. Tabia za kidunia tunajifikia sana sisi wenyewe na kusahau kabisa kuwafikiria wenzetu; hatuweki masihahi mapana ya jamii yetu tunaangalia zaidi faida gani mimi nitapata sasa.

Tafakari yetu leo inaturudisha katika mstari wa kuishi vyema ili kuweza kuyafurahia maisha yetu sio sasa tu bali na hata baadae. Tumwangalie mfalme Daudi alitenda dhambi kubwa sana lakini alimrudia Mungu akamwomba msamaha kwa makosa yake na kuahidi kubadilisha tabia yake. Kwa Kufanya toba ya kweli Mungu alimsamehe. Ni fundisho kwetu Mungu wetu ni mwepesi sana kusamehe. Unamkumbuka Yule mtu wa mataifa alipokwenda kusali hakuinua hata kichwa chake alikiri dhambi zake na kuomba msamaha. Na Mungu alimsamehe; tunakumbuka kisa cha mwana mpotevu alijua makosa yake alijua kuwa tabia yake ilikuwa mbaya na ilikuwa haipendezi Mungu; akaamua kurudi nyumbani na kuomba msamaha wa kweli mbele ya Mungu na baba yake na akasamehewa;

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa Mungu alimwondoa Adamu kutoka katika bustani ya Eden kwa kufanya dhambi moja; sasa je sisi leo kama hatutafanya toba ya kweli tunafikiri tutaweza kushiriki furaha ya milele kwa dhambi zetu nyingi zinazotuzunguka? Mara nyingi tuna sikia watu wakisema mimi sina dhambi ya kuomba msahaha au kufanya toba; je wewe ambaye unasoma tafakari hii huna kitu ambacho umefanya kinyume na utaratibu wa Mungu ambao unahitaji msamaha? Jitatimini mwenyewe na ujipime kama kweli hutitaji toba ya jambo lolote lile ulilomkosea Mungu; nafikiri kuwa tunatakiwa kuwa watu wa Toba kila wakati;

Tafakari yetu leo bado inatukumbusha kuwa toba inaleta mabadiliko ndani mwetu na hasa katika akili zetu na kukubali kuacha dhambi na kuyaendea maisha ya utakatifu; Toba ya kweli inakwenda sambamba na Imani; Imani ya kweli huzaa toba ya kweli hivyo ni wajibu wetu kuendelea kuimarisha imani yetu na kwa imani tutaweza kuyagundua matendo ambayo yanahitaji Toba ya kweli.

Hii ndio Tafakari yetu ya leo-Amina

Emmanuel Turuka


No comments:

Post a Comment