WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Wednesday, March 29, 2017

TAFAKARI: WOGA KATIKA MATENDO YETU UWE SILAHA YA USHINDI




Tafakari yetu ya juma hili tunaangalia dhana ya woga katika maisha yetu; woga ni kielelezo kuwa kuna kitu kimesimama katika njia mbayo tunastahili kupita; lakini pengine kwa mantiti ya ukweli kabisa hakuna kitu cha namna hii; woga huleta wasiwasi na kutufanya kushindwa kufanikiwa malengo yetu; woga hutupotezea kabisa uwezo wetu wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi wa kufikia malengo ambayo ndio lengo la mafanikio yetu;

Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa vizuizi kama woga visiwe kikwazo katika maisha yetu hasa ya kiroho tunakumbushwa hata tukijikwaa kwenye ukuta  ni lazima tukubali kuwa kujikwaa sio mwisho wa safari. Woga ambao husabibisha akili zetu kudumaa lazima upate ufumbuzi ndani ya akili zetu. Akili zetu lazima zijue kuwa kushindwa kunakutokana na woga hatupaswi kutoa  nafasi kwani bibilia inatukumbusha kuwa neema yake inatosha katika shida zetu. Woga utupe sisi ujasili wa kupata ushindi; kushindwa kunakosababishwa na woga kuwe sehemu ya ushindi; Yesu alipokuwa akitembea juu ya maji wafuasi wake walishituka na kujawa na woga wakifikiri kuwa wameona ni jini; walipomtambua kuwa alilikuwa Yesu Petro akamwambia Yesu bwana nami naomba nitembee juu ya maji Yesu alimwita akamwambia njoo, alianza vizuri lakini kwa vile alileta silaha ya woga akaanza kuzama.

Je woga wetu hutoka wapi? Woga katika maisha yetu huletwa na watu wengine, pengine tunatamani kumpendezesha kila mtu, au kuishi kwa matarajio ya maisha ya watu wengine na kwa macho yao  hivyo kwa kuishi katika maisha ya namna hiyo huweza kutupa sisi wakati mgumu sana; lazima kutakuwa na vizingiti vingi sana lakini bado hatutakiwa kukubali kuwa vikwazo vituzuea katika maisha yetu. Tunatakiwa kuwa tayari kuruka vihunzi, na daima macho yetu yawe yanangalia mpira ili tuweze kushinda na sio kuwa watu ambao tumejaa woga. Tukiwa na mawazo ya kushindwa sio sehemu ya ushindi; kushindwa ambako kunatokana na woga ni ishara ya kutuambia sisi kuwa hatuko sawa;

Najua kabisa hatuwezi kuepuka woga lakini woga usitawale maisha yetu, hata Yesu alitawaliwa na woga alipokuwa katika bustani kabla ya safari ya mateso yake lakini kwa ujasiri mkubwa aliushinda woga na kuweza kubeba kikombe cha mateso kwa ujasiri mkubwa hatimaye kuleta ukombozi kwetu sote kwa damu yake pale msalabani.

Tukiendekeza woga basi tumeshajiwekea sisi wenyewe dalili kubwa ya kushindwa;woga unatakiwa utufundishe sisi na kutuletea mageuzi na kutufanya kuwa watu bora zaidi. Tunaposoma kuhusu maisha ya jehanamu tunajawa na woga; basi Woga huu unatakiwa utusaidie sisi tuyafuate maelekezo ya mungu katika kuishi maisha bora ambayo yanampendeza Mungu wetu. Hivyo woga utujengee sisi ushindi kama Yesu alivyofanya na leo tumekombolewa kupitia damu yake takatifu sisi sana kwa ukombozi huu jukumu letu  ni kufanya matendo mema ambayo yanampendeza Mungu.


 Ni jambo nzuri ambalo sisi binadamu tumewekewa Mwenyezi Mungu alijua uzaifu wetu kuwa kwa kushindwa kwetu ambako kunatokana na woga awetu tumewekewa namna ya kuweza kuomba msamaha. Ndio maana  ya kipindi hiki cha toba, kipindi hiki ni alama tu ambayo tunatakiwa kuishi kwa namna hii katika maisha yetu yote. Natukiweza kuishi katika namna hii tutakuwa tumefanikiwa sana sana. Kristo ametuonyesha mfano kuwa yeye aliweza kusimama kidete katika kutuonyesha mfano maisha yale ambayo Mwenyezi Mungu anataka sisi tuishi; tumepewa nafasi ya pili ya kujirekebisha na kuishi bila kutanguliza woga mbele bali kutanguliza ushujaa wa kumpigania Yesu; tunatakiwa tutambue udhaifu wetu na kupata nguvu za kuukabili udhaifu huo; tubadilishe tabia zetu; 

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa pamoja na kukabiliwa   maisha wakati mwingine yanakuwa magumu sana; kupitia kipindi hiki cha mfungo na kumrudia Mungu tumepata nafasi nyingine nzuri sana na ya ajabu sana; Mungu anaendelea kutujalia sisi siri kubwa ya ushindi wa maisha yetu na mbinu za kumshinda shetani; lazima tukubali kuendelea kujifunza na kuwa tayari kubadilika; maisha ya ushindi ni magumu na kuwa mwoga haitasaidia kushinda vikwazo ambavyo vinachelewesha ukamilifu wa safari yetu hapa duniani bali lazima tusimame imara na kuamini kuwa bila nguvu za kristo ndani yetu sisi wenyewe hatuwezi kuipigana vita hii kwa ushindi mkubwa; woga wetu utaendelea kuwako bali tukimpokea Kristo woga hauna na nafasi hata kidogo. Maisha yatendelea kuwa mazuri kwa wale wanaomwamini kristo na wako tayari kufa pamoja naye. Woga wako ukimtegemea kristo hauna nafasi kabisa na utakuwa huru; tufunge na Kristo na tufe naye msalabani kwa kuishi maisha yale ambayo kristo aliishi na kuwa alama ya ukombozi wetu ;

Huu ndio ujumbe wetu wa wiki hii ya kwaresma.

Amina            Amina            Amina

Emmanuel Turuka
2017



Friday, March 10, 2017

TAFAKARI: TUNAIPOKEAJE ZAWADI KUTOKA KWA MUNGU?


·        KWA MOYO WA SHUKRANI NA UNYENYEKEVU?
·        KWA MOYO WA MALALAMIKO?


Katika kipindi hiki cha Kwaresma tafakari yetu ya wiki hii inatuuliza swali moja je sisi ni watu wa kushukuru au ni watu ambao tumejaa malalamiko tunavyoyakabili maisha yetu ya kila siku?

Tujikumbushe kuwa Mungu wetu ni Mungu aliyejaa huruma na ni Mungu ambaye ni mtoaji; lakini sisi kama wana wake je tunatambua ukuu wa mungu katika maisha yetu? Je zawadi zote ambazo Mwenyezi Mungu anatujalia sisi tunazipokeaje, tunazipokea kwa moyo uliojaa shukrani au tunazipokea kwa kuturidhika na kwa malalamiko? Tatizo letu tunasahau haraka sana zawadi ambazo Mungu anatujalia katika maisha yetu, na daima tunaishia kuwa watu ambao tunakuwa wa kulalamika zaidi na sio kushukuru na kuomba bila kuchoka.

Lakini tunabahati kubwa pamoja na malalmiko yetu Mwenyezi Mungu bado anaendelea kutupenda na kutujalia sisi mahitaji yetu. Tukumbuke jinsi wana wa Israeli walivyokuwa wakilalamika lakini kila siku mpya Mwenyezi Mungu aliendelea kuwalinda na kuwapa mahitaji ambayo walikuwa wakihitaji kwa siku hiyo.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima tuendelee kufunga na kusali tukiomba msamaha kwa kosa hili kubwa la kulalamika hata pale tunapotendewa mema. Tunatakiwa kupokea kila zawadi tunayojaliwa katika mikono ya shukrani. Tukumbuke kuwa mbele ya Mungu malalamishi sio kitu cha kujivunia. Unyenyekevu, moyo wa shukrani ndio vitu vya kujivunia mbele ya wenzetu na Mungu.

Tukumbuke kuwa wakati mwingine Mungu anatupa sisi zawadi ambazo hatustahili kabisa. Je kuna zawadi gani kuwa zaidi ya Kumtoa mwanaye aje ulimwenguni ateseke na kufa kifo cha aibu kwa ajili ya dhambi zetu ili sisi nasi tufurahie utukufu wa Mungu Mbinguni. Kwa kuja kwake sisi tumekombolewa.

Tunavyo kumbuka mateso ya Yesu, tujikumbushe kuwa mateso yake yamekuwa ufunguo ambao umetufungulia sisi uzima wa milele. Yesu ameweza kutusaidia sisi kukata kiu ya kufurahia maisha maisha yetu ya baadae; kwani tukiweza kuishi ndani yake kwa matendo kamwe hatuwezi kuogopa kifo; kwani uchungu na ugumu wa Kifo Yesu ameshauondoa.

Kwaresima hii itukumbusha kuwa Yesu ndio mkate kweli wa uzima ambao unasafisha kabisa njaa, wajibu wetu ni kuendelea kuishi kulingana na mafundisho yake. Na kubwa ambalo tunakumbushwa leo tuache kulalamika bali tupokee zawadi zote tunazopewa kwa upendo na kwa moyo wa shukrani ili neema ya mungu ibaki juu yetu.

Ili kuweza kuijiimarisha katika zawadi hii Yesu anataka sisi leo kuendelea kujifunza umuhimu wa zawadi zote ambazo tunazipata leo kupitia watumishi wake ambao wamepewa uwezo wa uwakilishi wa Kristo katika maisha yetu. Wao ni binadamu kama sisi bali ni chombo kilichobarikiwa katika kutekeleza mafundisho ya kutuelimisha sisi umuhimu wa kupokea zawadi zetu kwa moyo mkunjufu uliojaa upendo na shukrani na sio kujijengea tabia  ya kulalamika  na kuona kuwa Mungu anatuchukia;

Tukiweza kupokea zawadi hii ndipo tunapotambua ukuu wa neema ya mungu juu yetu; Mungu anatujenga sisi katika imani kubwa kama tutaweza kuacha kabisa malalamiko, tutakuwa tumekomaa katika imani. Katika tafakari yetu ya wiki hii tumpe asante mungu kwa upendo wetu kwetu kwa kutujalia sisi ridhiki yetu ya kila siku na tunamshukuru kwa kutujalia sisi pia mkate wa uzima jambo la msingi ambalo ndilo linalotawala tafakari yetu je sisi tunapokeaje hii zawadi kubwa ya ukombozi wa maisha yetu?



Emmanuel Turuka

Wednesday, March 1, 2017

SIKU 40 NI KIPINDI CHA KUTENDA MEMA (KWARESMA/LENT)





Kwaresma ni kipindi ambacho tunakumbuka maisha ya Mwokozi wetu Yesu kristo na kazi yake ya ukombozi wa maisha yetu katika safari ya maisha yetu baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa maneno mengine Kwaresma ni kipindi maalum ambacho wakristo
Wanatakiwa wayaelekeze maisha yao zaidi katika sala, kufunga na kuwasaidia wale ambao wanahitaji masaada. Ni kipindi zaidi cha kutafakari na kufanya toba na kumrudia Mungu.

Kipindi cha Kwaresma  kinajumuisha siku arobaini za toba na shukurani kwa Mungu. Tukisoma katika maandiko matakatifu tunaweza kuona jinsi  watumishi wa Mungu manabii ambao Mungu aliwapa majukumu mazito baada ya kufunga na kusali kwa siku 40; Walitakiwa kutubu kabla ya maombi au ahadi ambazo Mwenyezi Mungu aliwaandaa kuzipokea kwa faida ya watu wao.  Musa alifunga siku 40 kabla ya kupokea amri kumi za Mungu “Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.” (Kutoka 34:28). Nabii Eliya alifunga siku 40 kabla ya kuonana na Mungu kwenye mlima Orebu: “Akainuka, akala akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu mlima wa Mungu.(I Wafalme 19:8)

Kipindi cha kwaresma siku 40 kwa mfuasi mtiifu wa kristo lazima atapambana na mitihani mingi; kwa vile shetani naye anakuwa kazini kupinga mema ambayo unataka kufanya lazima utakutana chaweza taabu, wasiwasi, uzuzu, woga, kukosa msimamo au mwelekeo.

Tukumbuke maisha ya Yesu kabla ajeanza utume wake Katika Agano jipya, Yesu alifunga siku 40 (jangwani) akipambana na majaribu kabla ya kuanza kazi yake. Alijaribiwa na shetani mara tatu; lakini aliyashinda majaribu ya shetani;

Tukumbuke kuwa Kufunga ni jambo linalomsaidia mtu kutafakari kuhusu mambo ya kiroho na kumkumbusha kwamba kuna mambo muhimu maishani kuliko mali na chakula. Funga inatusaidia sana sisi kujenga uhusiano mzuri pamoja na Mungu. Na kubwa zaidi funga inatusaidia sana sisi tuaminio  katika kutimiza ahadi ya kumshukuru Mungu na kuonyesha kwamba mtu amejitoa kwake. Ninafunga kwa sababu ninampenda Mungu.

Yesu alitoa taadhari ambayo sisi tunapotekeleza Kwaresima hii ya mwaka 2017 tujiepushe kujiona kuwa sisi ni bora zaidi; mimi ni mwadilifu zaidi kuliko mwenzangu; Tuondoe dhana ya kuhukumu; hii ni sawa na kujisifia mwenyewe wakati hujui mwenzako pia amefanya nini ambacho kimempendeza Mungu. Tumkumbuke Yule farisayo mwenye kiburi aliyejiona kuwa bora kuliko wengine kwa sababu alifunga kwa ukawaida, unaonyesha wazi kwamba Mungu anakataa mtazamo kama huo. Yesu anatukumbusha kuwa tendo la kufunga ni tendo jema lakini ni tendo linalohusisha nafsi yako na Mungu na hupaswi kuwaambia wengine kwamba umefunga.

Wote wakitambua hali yao ya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu hutumia wakati huo katika kutubu, kuungama na kukiri makosa yao mbele ya Mwenyezi Mungu. Toba hiyo hufanyika kwa njia mbalimbali. Licha ya kufanya hiyo toba, pia wanashauriwa kusali zaidi wakati huo wa toba. Tunavyofahamu sala ni mahusiano ya karibu sana ya binadamu na Muumba wake. Hapo hutoa sala za kushukuru, sala za kuabudu, sala za kumsifu Mwenyezi Mungu, sala za kumtukuza, sala za kuomba msamaha kwa dhambi mbalimbali tulizomkosea Mwenyezi Mungu na pia zile ambazo tumewakosea binadamu wenzetu.

Maisha yetu sisi kama binadamu maisha yetu yamejaa matendo maovu; hivyo kipindi cha kwaresima ni wakati mzuri wa  kujipatanisha na Mungu kwani kwa kutenda dhambi sisi tunajifarakanisha na Muumbawetu, na hivyo tuhitaji upatanisho. Siyo hayo tu, pia huyo binadamu huwa amejitenga na binadamu wenzake anayeishi na kushirikiana naye. Kwa hiyo jambo la tatu analopaswa kulifanya mtu yule mwenye kufanya toba ni kufanya matendo mema, yaani kutoa sadaka kwa ajili ya maskini na wale ambao ni wanyonge katika jamii yetu.

Ni matumaini yetu kuwa Mfungo huu wa Kwaresima utakuwa ni wenye manufaa kabisa kwa Waumini wenyewe binafsi, lakini pia kwa ndugu na marafiki wote. Tukumbuke kuwa hasira ya Mungu itatulizwa tu ikiwa waumini tunafunga na kujinyima mambo mbalimbali. Tukiwa na imani tunasadiki kuwa kwa mfungo huo wa waumini wakristo utasaidia kabisa kwa kutuletea neema.

Jambo jingine ambalo Waumini Wakristo wanapaswa kulizingatia ni kwamba imewapasawa kutoa sadaka zao kwa moyo wa ukarimu. Wakati huu wa Mfungo ni wakati hasa wa kutenda matendo mema na kuacha uchoyo na ubinafsi. Waumini wanapaswa kuwa wema zaidi, na kuwa wakarimu zaidi. Hivyo ndivyo inavyowapasa wale wote ambao wameamua kufunga na kumrudia Mwenyezi Mungu.

Tukumbuke kuwa Kweresma inatupasa itubadilishe kuwa waumini bora kabisa sisi tu kwa siku 40 bali kwa amsiah yetu yote mpaka tunakufa mfungo, utusaidie kutubadilisha kabisa kutoka ndani ya mioyo yao. Tunaweza kusema kuwa lengo la Mfungo ni kumbadilisha binadamu, ni kufanya mageuzi ya ndani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Mfungo mtukufu ni kipindi cha kubadilika kutoka ndani na kuwa binadamu aliye mwema na mkarimu zaidi. tunanatakiwa kuonyesha upendo wao kwa maskini.Basi tunaomba kwa njia hii ya Mfungo mtukufu waumini wazidi kujipatanisha na Muumba wao, na pia wajenge mahusiano mema na ndugu zao wanaoishi nao. Kwaresima ni mabadiliko, Kwaresima ni mageuzi, Kwaresima ni kuwa na upendo zaidi wenye ukarimu zaidi. Kwaresima ni kuahidi kuacha mabaya na kuzingatia mema na hivyo Kwaresima ni kuwa watu wapya waliojaa huruma na upendo kwa Mungu na jirani.
  
Nawatakieni kwaresma njema ya mwaka 2017

Emmanuel Turuka

Kalamazoo Michigan