WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Friday, April 7, 2017

TAFAKARI: TUJIFUNZE KUTOKUHUKUMU KWA HISIA KATIKA KIPINDI HIKI CHA MFUNGO:



Petro aligeuka na kumwona yuke mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa akimpenda sana; akumuuliza je na huyu vipi? Je kama mimi nataka kumwacha huyu mpaka nitakaporudi wewe inakuhusu nini? Wewe nifuate mimi Yohana 21:21-22. Tafakari yetu juma hili Yesu anatukumbusha umuhimu wa kuwa na kiasi katika kutaka kujua mambo ya watu wengine; Tunatakiwa kuwa watu wenye hekima na kujali Zaidi mambo yetu, tufanye kile ambacho yatupasa sisi kufanya; 1Wateselonike 4:11 tena mjitahidi kutulia na kutenda shughuli zenu,na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe kama tulivowaagiza.

Tunakumbushwa sana kujitathimini na kuacha kuingilia maisha ya watu wengine; kwa msingi huu kwamba  tukiangalia sana wale ambao wako sana katika maisha ya watu wengine; basi hawana thamani kabisa hata katika maisha yao ya kila siku; wako tayari kunena ya watu wengine na kutoa hukumu ambayo imejaa hisia kulingana na wao wanavyotaka iwe; kwa maneno mengine wanaweza kuwa chanzo cha mafarakano katika maisha ya  watu wengine katika jamii kwa ujumla. 2 Watesolonike 3:11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine;

Lakini wale ambao siku zote wao wako katika maisha ya Kimungu  Luka 2:49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? hawatakuwa na muda wa kutumia muda wao katika mambo ya watu wengine, daima watakuwa wakitembea katika busara ya Mungu na kutenda mambo yao kwa haki na uadilifu wa pekee. Wakorinto 4:5 basi ninyi msihukumu jambo kabla ya wakati wake; tukumbuke kuwa kila mtu  anatakiwa kuwa tayari kuhangaika na mambo yanayomhusu yeye  mwenyewe; Katika jamii yetu, tukumbuke kuwa kuna watu ambao wao kazi yako kubwa ni kulaumu na kukosoa tu hawawezi kuona kitu au jambo nzuri lolote kutoka kwa wengine; na pengine ukibahatika kuona nini kinaendelea katika maisha yao utashangaa kwa nini wako msitari wa mbele kuhukumu wenzao; pengine maisha yao na hukumu ambazo wanazitoa kwa wengine hazilingani kabisa.

Tafakari yetu leo inaendelea kutukumbusha kuwa  tunapoteza muda wa kufanya mambo yetu mazuri yampendezayo Mungu kwa kujihusisha  na mambo ya watu wengine; lakini utagundua kuwa jinsi kuwahukumu wengine katika mambo ambayo hayana msingi ndivyo tunavyowasaidia wao kufanikiwa Zaidi na kuwa karibu na Mungu na kufanikiwa Zaidi. Tunatakiwa kuanza kusafisha nyumba zetu kabla hujeanza kuona uchafu katika nyumba ya wengine kwa kutumia ulimi wetu.

Na pale tunapogundua  kuwa maisha hayako vizuri yarekebishe na tuyasimamie na sio kutumia muda mwingi katika kuhangaika na maisha ya watu wengine. Kwa nini uwe na uchungu na maisha ya watu wengine? La msingi ni vizuri tukajifunza kutilia mkazo maisha yetu na kuziondoa changamoto zetu za maisha. Ni rahisi kwetu kuona Kibanzi katika jicho la wenzetu na kushindwa kuona boriti katika jicho lako au langu;

Kwa kweli wakati mwingine inatakiwa tuamue kufunga masikio na kuziba macho ili tuweze kusonga mbele; chochote ambacho tutafanya hakitaweza kumridhisha kila mtu na kila mtu atatoa hukumu yake; kama tusipokuwa makini hao ni waharibifu wa safari yako ya maisha; midomo yetu  imejaa masengenyo na majigambo; midomo yetu inapinga uumbaji wa Mungu dhidi ya wenzetu; maneno kama mbaya, hana elimu ya kutosha; hana kazi nzuri; mwone kwanza: je haya maneno yanaashiria nini katika uumbaji wa Mungu; Je Yesu alipokuja kutukumbo sisi kutoka katika misha ya dhambi aliangalia vitu hivyo? Jibu hapana alitukomboa sisi kulingana na njisi tulivyo bila kuangalia ukubwa au uwingi wa dhambi zetu; na jambo njema pamoja na mapungufu yetu sote tumepokea kipimo sawa.

Tukisoma Injili ya Mathayo 7:5 Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.  inatukumbusha kuwa sisi tuko makini sana katika kuhakiki maisha ya watu wengine na mapito yake; swali la kujiuliza je sisi tunafanikiwa vipi na kupata kibali cha kuwahukumu wengine? Au nasi tumekuwa katika kundi la wanafiki kwa kupenda tu kuhukumu? Tunatakiwa kuwa kioo cha matendo yetu na busara yetu kuwa mfano kwa wengine? Tusome sana neno la mungu;

Tukisoma kitabu cha Zakaria 4:10 Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.  katika maisha vitu vinakuwa taratibu havilipuki tu kutoka kusikojulikana. Kila mafanikio yanahitaji uwajibikaji na uvumilivu. 

je unaona raha gani kuongelea  mambo mabaya juu myu mwingine? kwa nini usiongelee mazuri au pale alipokosea usimrekebishe kwa upole na kwa busara iliyojaa unyenyekevu? itakuwa ni jambo la kufurahia kwa wakati huu wa mfungo na toba ni kujifunza kutenda kila jambo kwa haki kama Yesu alivyotutendea na uthibitisho wa hili ni kitendo cha kukubali kufa msalabani kwa wokovu wetu;

ushauri wangu kama unatenda jambo njema na unahukumiwa ni wakati wa kushukuru sana kwani  unafanya jambo nzuri ambalo linawaumiza na wanataka kukurudisha nyuma; kumbuka ukiwaruhusu na kuwapa nafasi ya kukukatisha tamaa ujue kuwa  nawe mwisho wako utakuwa umefika. Kama Yesu angesikiliza kelele zote za walimu wa sheria na wayahudi ambao walikuwa wanampinga; sisi tusingeweza kupata wokovu wetu huu ambao tunaufurahia leo. La msingi ukikabiliwa na mtihani wa aina hii simama kidete na ujipanga vizuri kwani ushindi wako unakaribia. Methali 18:21 mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; na wao waupendao watakula matunda yake.

Inasikitisha sana leo kuona jamii na jumuia zetu zinatawaliwa na nguvu ya masengenyo; wivu na undumila kuwili . hivyo kwa kweli kama tunapenda kufurahia maisha mazuri lazima tujiepushe sana kuutumia ulimi wetu katika kusema mambo mabaya juu ya wenzetu. Metali 6:17 mambo ambayo yanamchukiza sana bwana Macho ya kiburi, ulimu wa uongo na mikono imwagayo damu isiyo na hatia.

Tukumbuke kuwa tunapokuwa tuko midumo juu tayari kuwahukumu na kuwalaumu na kuwahukumu wenzetu, Mungu kamwe hana muda wa kutusikiliza yeye wakati huu anafanya kama hatusikii na utuandalia adhabu,  mfano wa Yesu na kundi la watu waliompelekea mwanamke alifumaniawa katika tendo la unzinzi. Pamoja na kufafanua sheria zote kuhusiana na kosa hilo Yesu alikaa kimya kama vile hawasikii, aliponyanyuka aliwauliza swali kama kuna mmoja wenu asiye na dhambi awe wa kwanza kumrushia  mama huyu; Yohana 8:7. Fundisho hapa ni moja tu hukumu kama wewe hujetenda dhambi yeyote ile; tujenge upendo wa kweli kati yetu upendo ambao huubagui; hii ndio tafakari yetu ya wiki hii.

Amina                   Amina            AMINA

Emmanuel Turuka

2017


Thursday, April 6, 2017

DARAJA LA TABASAMU, UPENDO NA MATUMAINI LILILO MALIZA KAZI KWA USHINDI;




Tafakari ya wiki hii ya Kwaresma tunakumbuka maisha ya Mama yetu Anna Michaeli Kinunda aka Mbuya; tunayakumbuka maneno ya Yesu tukisoma Yohana 19:27 kisha akamwambia yule Mwananfunzi ;Tazama Mama Yako;Je kunasiri gani Yesu alikuwa akimwonyesha yule Mwanafunzi: Nguvu ya akina mama katika misha yetu ni kubwa sana. Upendo wao hauna mipaka;

Leo tunajikumbusha maisha ya mama Anna Kinunda (Mbuya) ambaye Mwenyezi Mungu alimwita katika makao yake ya milele tarehe 13 December 2016. Mama ambaye alikuwa amejaa furaha na Amani ya Bwana ukiondoa ubinadamu wetu ambao ni zao la kila mmoja wetu; Mama Anna alikuwa Mtu mwenye nia thabiti juu ya Mungu wake; alimtumikia Mungu kwa moyo wake wote na hakukatishwa tama na mtu au kitu chochote alisimamia kile ambacho alikuwa anakiamini; Pamoja na ukweli kuwa kifo kamwe hakizoeleki daima kinageuka kuwa ni jambo la kutisha na ambalo halizoeleki; Mama Anna alikuwa tayari kwa kifo chake na alikisubiri na kukipokea kwa unyenyeku siku ya jumatano tarehe 13 december huku akiwa akiendelea na sala zake katika kumshukuru Mungu; alikutwa akiwa amepiga magoti huku akiwa amefunga mikono yake katika ibada yake na Mungu wake; hivyo alikufa katika unyenyekevu; na furaha kubwa;


Tukisoma kitabu cha wakorinto 2 : 5 : 1-5  hofu na woga mkubwa sana ambao hugusa mioyo ya binadamu ni woga wa kifo; kifo kinatujengea  woga wa kiwango cha juu katika maisha ya binadamu kuliko woga wa kitu kingine chochote. Tunaogoapa kufa; tunaogopa  kifo pamoja na mafundisho yote ya ahadi zilizo jaa faraja ambazo tumeandaliwa baada ya Kifo; bado tumekuwa wagumu kukipokea kifo kwa unyenyekevu; bado tunakuwa na mashaka juu ya kifo; tunakuwa na imani haba na kuamini kuwa hatujui nini  kitatokea baada ya kifo; kifo kimekuwa ni tatizo la msingi sana katika maisha ya binadamu; hata wachungaji ambao wamekuwa wakihubiri kuhusu maisha yetu ya kifo ni mbinguni na yatakuwa maisha yaliyojaa furaha lakini nao wanaogopa sana kifo ; Ili tufurashie hiyo furaha ya milele lazima tufe na kifo ndio njia pekee ya kutupeleka Mbinguni  lakini sio njia ambayo tuko tayari kuipokea ; Mama yetu Anna  alikipokea kwa upendo mkubwa bila woga na alikisubiri bila mashaka yeyote.

Tukisoma kitabu cha Yakobo 4:14 14 kinatukumbusha kwa ufupi walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Na mzaburi 90:5-6 naye anatukumbusha kuwa  Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. 6 Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka. 

Kama ilivyoelezwa katika mazingira tofauti kuwa hakuna kitu cha uhakika zaidi ya kifo, na hakuna ambaye anaweza kukwepa kifo “ Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.   Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa;” Lakini tukisoma 2 Wakorinto 5: 1-2 Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni. 2 Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni; maandiko haya ya Paulo kwa wakorinto tunaelewa nini kipo mbele yetu, ukweli wote ambao uko mbele yetu, matumaiani pamoja na mtafaruku wote wa kifo. Tukumbuke kwa Mungu alishatowekea ushuhuda ambao hata kifo chenyewe hakiwezi vunja. Wafilipi 1:21 Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. 



Tukiamini katika imani tunagundua kuwa tunapokuwa katika khali ya kifo ni tendo lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu ukilinganisha ni viumbe vingine vyovyote; tendo la viumbe au mimea kufa linakuwa limekamilika na kufikia mwisho wake;  lakini kwetu sisi kama binadamu tunapoteza tu uwezo wa kutambua kibinadamu, hatuhisi chochote kulingana na ubinadamu tuliokuwa tumeuzoea; na tunakuwa hatuko tena katika ulimwengu huu wa kidunia lakini sasa maisha yetu ya kiroho yananza kulingana na matendo yetu hapa duniani. Hatuishi kwa ajili yetu wenyewe bali maisha yetu yanakuwa katika daraja jipya; ni maisha ya  kumsifu na kumshangilia Mungu siku zote; ndio wale ambao tunawashangilia kuwa wamemaliza kazi katika utukufu wa Kimungu. Maisha yao yote na malengo katika maisha yao ni kuishi katika utukufu wa Kimungu. Ndio wale ambao wananungana na Mtume Paulo aliposema Warumi 14: 7-8  Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. 8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. 

Yesu katika mafundisho yake alikuwa akisisitiza sana matendo mema; Imani ili iweze kufanya kazi yake inahitaji matendo. Imani bila matendo hakuna wokovu. Tunaamini kuwa kila muumini ambaye anaamini na anaishi kulingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu amekombolewa katika dimbwi la dhambi;

Mama Anna alikuwa ni  mwanamke aliyejaa matendo mema na kwa sadaka alizozitoa. 1 Timoteo 7-9 Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; 8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. 9 Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Mathayo 6:26-27 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. 26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 




Tunafundishwa kuwa hatutakiwi kusoneneka kwa kukosa thawabu za Kimungu kwa matendo yetu mabaya Yuda alisikitika kwa kumsaliti Yesu kwa vipande 30 vya Pesa; je wewe kabal ya kifo chako unahuzunika kwa jambo gani? Je matendo yako yanakupa njia sahihi ya Kufurahia utukufu wa Mungu? Je baada ya kifo wapendwa wako utawaacha katika khali gani ya furaha au unyonge kufuatia maisha na matendo yako?
Mama Anna daima alikuwa akisema kuwa nimemaliza kazi na maisha yangu kama Mkristo, nimetimiza wajibu wangu na nimewaonyesha njia kama Mkristo, na sasa niko tayari kwenda kupumzika kwa Baba. Hakuwa na mashaka wala woga wa kufa kwani alikuwa akiendelea kujiandaa kila siku na kuomba huduma za kiroho kila siku. Kwake kila siku mpya ilikuwa ni siku ya Maombi. Daima alikuwa akijiuliza mimi ni nani? Kwa nini mimi nimezaliwa? Na ninakwenda wapi? Je nimetimiza majukumu yangu kama Mkristo?

Zaburi ya 37:28-29 Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa. 29 Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. 



Mithali 3: 12 Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye. 13 Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. 14 Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. 15 Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. 16 Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. 17 Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. 18 Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.


Mithali 16: 6-7 Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu. 7 Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye. 8 Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu. 9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake. Mama Anna aliishi katika Imani yake thabiti huku akiwa akifanya matendo ya huruma ; nyumba yake ilikuwa ni nyumba ya mayatima , nyumba ya wahitaji; alikuwa anatimiza ili amri kubwa ya kumpenda Mungu na jirani:  aliishi kwa Imani  na uaminifu  ule uliokuwa unampendeza Mungu wetu: hii ni njia pekee ambayo itatusaidia sisi kujihakikishia, uzima wa milele na furaha ya milele tukikumbuka kuwa yeye ni tegemeo letu na kimbilio letu; yeye ni kielelezo cha msamaha  katika maisha yetu tunayoishi hapa dunia ikiwa ni sehemu ya safari ya milele;


Upedo sio maana yake tu kupenda lakini ina maana kubwa zidi ya kuweza kuweka vipao mbele vyako katika kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Kama kama utaweza kufanikiwa katika hili ndipo imani yako, matumaini upendo wa kweli utakuwa unatwala maisha yako 1 Wakoritho 13:13 Jambo ambalo wengi wanaweza kujifunza kutoka kwako hasa baada ya maisha ya hapa dunia ni kupima je vita yako ya imani uliipiganaje? Ulitimiza makukumu yako kama Kristo alivyoagiza katika mafundisho yake? Yohana 13:34 na 2 Timotheo 4:7.

Mama Anna alikuwa tayari yeye asiwe na kitu lakini Jirani yake aweze kula na kushiba au kuvaa vizuri; daiama aliyafanya hayo kwa matendo na mafundisho; daima alikuwa akitufundisha jinsi ya kuishi kwa upendo na mashirikiano mazuri; kwa msingi huu yeye na Mume wake Marehemu Mzee Alois waliweza saidia watu wengi sana kwa kuwajengea misingi mizuri ya shule; waliweza kuishi na watoto wengi ambao hakuwa na uwezo wa kwenda shule bali wao waliwachukua na kuishi nao kama watoto wa familia moja.

Je wewe na mimi tukifa tutacha nini cha kujifunza kwa watoto wetu na jumuia inayotuzunguka? Je kile tutakacho kiacha kitakuwa kimejaa , upendo, matumaini na imani? Kama vile mtume Paulo alivyo waambia watu wakoritho fanyeni kila kitu katika upendo wa Kristo; kwa hiyo; urithi ulio bora hauwezi kupatika kama hatutamwogopa Mungu; amebarikiwa mtu Yule ambaye anamwogopa Mungu na kutumainia njia zake na amri zake; Zaburi ya 112:1-2. Tukumbuke kuwa kizazi cha wamuuchao bwana kitabarikiwa.


Mama Anna aliweza kufuata mfano wa Yesu; Tunajua kuwa Yesu alikuwa mtu maarufu sana; sio tu kwa sababu aliwalisha wale watu elfu tano pale mlimani, au alifanya miujiza mingi na kuwaponya wengi; au kwa sababu alikuwa Bwana wa Mungu; bali alikuwa na vitu vingine vingi ambavyo viliweza kuendana kabisa na maisha ya sisi binadamu wa kawaida; Yesu alikuwa akiwahudumia watu wote kwa utu na ubinadamu; mfano tu mdogo wakati ule kule Yerusalemu wasamaria na wanawake walikuwa wakionekana kama daraja la pili watu ambao hawana thamani katika jamii yao. Lakini Yesu aliwa hudumia wote sawa kabisa sawa na wayahudi wengine;

Yesu alikuwa msikilizaji mzuri; tunatakiwa kujifunza kuwa wasikilizaji wazuri; na hiyo inasaidia kujua shida na jinsi ya kusaidia kwa urahisi, kwani tutakuwa katika nafasi nzuri ya kusaidia. Yesu alikuwa sio mtu wa kukimbilia kuhukumu wengine  alikuwa akiongea nao na kuwaelimisha daima alikuwa kama kiongozi na rafiki; Yesu alikuwa akipatikana kwa urahisi bila masharti au ukiritimba wowote, mtu yeyote ambaye alitamani kuongea naye alipata nafasi ya kuongea naye, na hata Yule ambaye alikuwa hawezi kuongea naye kwa sababu yeyote ile aliweza pia hata kwa kumwita tu akiwa akipita na wengi walipata msaada waliokuwa wakihitaji. Hakuwa na masharti yeyote hivyo ndivyo alivyokuwa Mama Anna aliweza kuwa karibu na kila mtu bila kujali khali yake. Jukumu kubwa ambalo liko mbele yetu tunatakiwa kuendelea kuwa makini katika matendo yetu juu ya Mungu wetu; tukumbuke kuwa tunaokolewa kwa neema na kamwe kwa nguvu zetu wenjewe; Waefeso 2:8




Nilichojifunza katika maisha ya Mama Yangu katika uhai wake wote ni Upendo wake kwa kila mtu, Imani yake ambayo haikuyumba kwa wakati wote wa maisha yake, imani ya kumpenda Mungu, na kuishi kulingana na mafundisho ya Yesu na kumtumikia kwa moyo wake wote; hata pale alipotukanwa au kudharauliwa kamwe hakufanya kiburi wala kinyongo; nilichojifunza kwake kama Mithali 22:6 leo mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapo kuwa mazee; ilikuwa ni wajibu wake mkubwa kwetu ilikuwa kuturisisha umuhimu wa imani; kwetu sote na kumtanganza Kristo kupitia amri kuu ya Upendo; muhimu zaidi amekuwa Mama ambaye ameishi sana katika ukweli na ameweza kupata thawabu ya kweli kabisa mwisho wa safari yake hapa duniani; Wafilipi 2: 16 mkishika neno la uzima, nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya kristo, ya kuwa sikujitaabisha bure;




Mama Ana hakuwa anategemea sifa za kupendwa kutoka kwa wanadamu bali alikuwa akitegemea sifa kutoka kwa Mungu. Alikuwa ni mtu Yule,aliyependa kutoa zaidi kuliko kutegemea kupata zaidi; alikuwa akitekeleza zaidi amri ya upendo na kuamini kuwa maisha yake lazima ayatoe kwa watu wengine wanaomzunguka na ambao wanamahitaji msaada zaidi;

Mama Anna alikuwa mama Mwema; ambaye daima alikuwa akizungukwa na tabasamu la upendo; pamoja na mapungufu ya kibinadamu bali alijitahidi kuishi maisha ya  kutimiza amri ya upendo; alikuwa Mama ambaye daima hakujikweza bali alikwezwa kwa matendo yake; maishani mwake alitamamni kila mtu aishi maisha ya upendo na kuwajali wengine; Mama Anna hukua tayari kuona unaishi maisha mabaya ya kumchukiza Mungu; alikuwa msahauri wa mabadiliko; alitamamni sote tuishi wa upendo kama Yesu alivyofundisha; na alitamani sote tutekeleza majukumu ya upendo yanayompendeza Mungu hapa duniani.

Alikuwa Mama wa kawaida tu; na daima alikuwa akitosheka na kile ambacho alikuwa akipata; Alikuwa na Mama ambaye alikuwa akiishi kwa kuwaMfano Bora wa wa mkiristo anavyopasa aishi; alitosheka na maisha ya kawaida ambayo yampendezayo Mungu; Mama ambaye aliyatoa maisha yake sadaka ya uwakilishi wa kweli kwetu sisi kujifunza. Aliitambua imani,alitembea katika imani; alikuwa Mwamba katika imani yake; alitembea na Mungu ndio maana leo hii Mwenyezi Mungu amempumzisha kwa amani kabisa; nasi leo tunakila sababu ya kumwita mbarikiwa kwani amepata kifo chema kilichompendeza Mungu;

AMA KWELI MAMA ANNA KINUNDA(MBUYA) AMEKUWA DARAJA LA TABASAMU, UPENDO NA MATUMAINI LILILO MALIZA KAZI KWA USHINDI;


Raha ya milele mpe bwana na mwanga wa milele umwangazie apumzike katika usingizi wa Amani na wa ufufuo wa Mungu;

Amina               AMINA                               Amina                                


Emmanuel Turuka
2017