WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Sunday, February 28, 2016

MAJIRA YA MUNGU NI YA AJABU





February 28
Tafakari ya leo naendelea kusisitiza kuhusu ukuu wa majira ya Mungu kama yanavyoelezwa pia katika wimbo huu- Amina

BWANA UMENITOA MBALI

February 27
Tafakari ya leo tumshukuru Mungu kwani ametutoa mbali sana mpaka hapa tulipo leo hii. Katika Mazingira gani ambayo tupo bado tunatakiwa kumshukuru Mungu. Neno shukrani litawale maisha yetu - Amina

Friday, February 26, 2016

WAKUABUDIWA

February 26
Tafakari ya leo tujikumbushe wimbo huu , ambao unatuonyesha kuwa Mungu peke yake ndiye wa kuabudiwa wakati wote wa maisha yetu. Amen

Thursday, February 25, 2016

NENO AMINA LINATUKUMBUSHA NINI?





February 25

Katika tafakari ya leo tunajikumbusha ukuu wa neno Amina: Neno AMINA linalotumika sana katika maswala ya imani,  ni neno lenye maana nzito kwani ni neno ambalo limetumiwa sana katika bibilia na katika sala na ibada zetu za kila siku.

Neno Amina linaashiria  umoja wetu  katika kuamini kile ambacho kimesemwa au kuombwa kwa Mwenyezi Mungu: Neno Amina linatuunganisha sote katika sala au maombi na kukubalina katika umoja wetu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kwa ufupi ni neno linaloashiria “na iwe hivyo”; “tunakubaliana katika hili tunaloliomba”;  “tunaamini katika uhakika au kuwa na uhakika wa kile tunachokiomba au kukisifu”.

Tunasema neno Amina wakati wote wa ibada zetu za kila siku, katika sala zetu; Katika mijadala yetu; kwa ujumla Neno Amina linahitimisha sala na maombi yetu ikiwa ni  kielelezo cha makubaliano yetu na MUNGU.

Tukisoma kutoka katika kitabu cha kumbukumbu la Torati 27:16 inasomeaka hivi na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina. Hii inamaanisha kuwa wote wanakubaliana na laana hii kwa umoja wao.

Tafakari ya leo inatuonyesha kuwa Amina inamaanisha kuwa tunakubaliana na Baraka zote, ikiwa ni katika kuzipokea; Zaburi ya 72: 19 inasema kuwa jina lake tukufu na lihimidiwe milele; Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina, Amina

Tafakari ya leo inatuonyesha jinsi Yesu alivyosema neno Amina katika mafundisho na mahubiri yake kuliko mwalimu mwingine yeyote katika Bibilia. Katika John 3:3 Yesu akajibu Amina amina nakuambia Mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Katika majibu na mafundisho ya Yesu alikuwa anatuonyesha kuwa yale aliyokuwa akiyafundisha na yawe hivyo. Hapa tunajifunza kuwa neno amina linaonyesha uthibitisho katika kukabiliana Na yale ambayo yamesemwa au kufundishwa.

Somo muhimu leo ni kuwa "Amina ," tunasema , wakati wowote na tunamthibitishia Mungu kuwa  toka imara na tuamini kuwa kile tunachokiomba tunaomba tupate Baraka kutoka kwa Mungu.

Neno Amina tukilisema kwa dhati  Mungu atatimiza ahadi ya maombi yetu na kupata  neema na baraka tuziombazo tukumbuke kuwa ahadi zote za Mungu tunazipata tukiamini na kushukuru kwa kutumia neno lenye nguvu Amina. Kila kitu ambacho Mungu ameamwahidi  mwanadamu, atatimiza. Tukumbuke kuwa Yesu wakati anasulubuwa tukisoma Luka 23: 43 akamwambia Amina nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.
 
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa neno AMINA lina nguvu sana, kwani tunalitumia mwishoni mwa sala zetu, tukiwa na maana kubwa ya asante kwa Mungu kwa kupokea maombi yetu. Hivyo Amina inatufungulia kila ahadi ya baraka, amani , utoaji , faraja , msamaha, uzima, na utakatifu  tukiendelea kutambua kuwa yeye ni mwenye utukufu na nguvu, milele na milele. Amina. 





ZABURI YA 23: BWANA NDIYE MCHUNGAJI WANGU



February 24

Tafakari ya leo hebu pamoja tutafakari Zaburi ya 23 ambayo inasema: Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 
2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. 
3 Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 
4 Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. 
5 Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika. 
6 
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele

Zaburi hii ya 23 inatuomyesha uhusiano ambao uko kati ya Mungu na sisi waja wake; tunatambua kuwa kondoo hana sauti na mahitaji yake; lakini mchungaji ndiye anayefanya maamuzi ya mahitaji yake na natakiwa ayajue na awatekelezee; ndio maana Mwenyezi  Mungu anajua mahitaji yetu kabla hata sisi hatujemwomba.  Mwenyezi Mungu ametujalia sisi malisho mazuri na salama kupitia Bwana wetu yesu Kristo kwa kifo chake ametusafishia njia ya malisho mazuri, wajibu wetu sisi ni kufuata maelekezo yake. Ndio maana hataki sisi kama kondoo  wake tunywe maji katika chanzo ambacho sio salama, kama maji yanayotembea kwa kasi kwani sio salama bali ametutuyarishia tunye maji katika kisima  kilicho tulia na salama.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa sisi hatuna uwezo wa kumshinda shetani bila msaada wa Mungu. Tukizingatia tabia yetu ya udhaifu ambayo tunayo toka kuumbwa kwa dunia. Tabia hii ndiyo inayotupelekea sisi kuanguka katika dhambi mara kwa mara; Hatutakiwi kumwachia nafasi shetani hata kidogo na pale tunapoanguka katika dhambi tunatakiwa kuomba msamaa kwa Mungu wetu; Na kuomba ulinzi mzuri kutoka kwa Mchungaji Mwema ambaye alikufa Msalabani   kwa ajili ya wokovu wetu Amina.


Tuesday, February 23, 2016

Tafakari ya Heri wenye kuleta Amani





 February  23

Katika Tafakari ya leo tunaendelea kuungana na Mtumishi wa Mungu Dr. Aba Mpesha Ambaye anatukumbusha umuhimu wa kudumisha amani katika maisha yetu ya kila siku;

Tafakari  ya Heri wenye Upole inanikumbusha maneno ya Bwana Yesu kuhusu AMANI. Yesu alisema: Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu (Matayo 5:9).

Ukitafakari kwa kina, wito wa Yesu kwa wafuasi wake ni kueneza Amani.  Wote walioitwa na Yesu, walikutana na Amani – Yesu ambaye ni mfalme wa Amani. Kwa hiyo, Yesu ndiyo Amani yao.

Kusema kweli, wafuasi wa Yesu hawakuiitwa kuwa na Amani tu, pia walipaswa kuleta Amani. Wangeitwa kuwa na Amani bila kupata agizo la kuleta Amani, wangekuwa watu wa ubinafsi. Kwa sababu hawakuitwa wawe na ubinafsi, waliagizwa kukana vurugu na malumbano. Vurugu na malumbano havisaidii kutimiza lengo ya Yesu la kuleta Amani. Ufalme wa Yesu ni wa Amani tele. Ndiyo maana wote walio kwenye jumuiya ya Yesu Kristo husalimiana na busu la Amani.

Wanafunzi wa Yesu malisisitiza kudumisha Amani kwa kuchagua kuteseka badala ya kufanya wangine wateseke. Hata Petro alijifunza hilo kutoka kwa Yesu usiku ule Yesu alivyokamatwa, Petro katika kumtetea Yesu, alimkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu. Ebu sikiliza Yesu alisemaje. “Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamizwa kwa upanga.” (Matayo26:52).

Ni kweli wafuasi wa Yesu wanapaswa kuhifadhi jamii, wakati dunia inavunja jamii. Wanapaswa kukana kujitutumua binafsi na kukaa kimya wakikumbana na chuki na dhuluma.
Ni kwa njia hii wafuasi wa Yesu ushinda  uovu na wema.

Ebu jiulize, jamii yetu ambayo imelea utamaduni wa vurugu na malumbano, ingekuwaje kama watu wote wangekana vurugu na malumbano, na badala yake wakatekeleza utamaduni wa Amani. Ni kweli tutaitwa watoto wa Mungu na kuirithi nchi tuliyopewa na Mungu, kwa sababu Amani itatawala.

NAAMINI HII NI DUNIA TUNAYOILILIA.  


BASI TUMWOMBE MUNGU ATUPATIE SHAUKU YA KUTAKA KULETA AMANI HAPA DUNIANI, NDIPO TUTAITWA WATOTO WA MUNGU. Hii ni tafakari ya leo toka kwa mtumishi Aba Mpesha.

Monday, February 22, 2016

HERI WENYE MOYO MPOLE




February 22
Leo tuungane na Mtumishi wa Mungu Dr. Aba Mpesha ambaye anatuletea tafakari ya leo tukiwa tunatimiza sikuya 12 ya  Kwaresma: Heri wenye Upole maana hao watairithi nchi (Matayo 5:5)
 Nilipofikiria mstari huu, swali lililonijia ni hili: Nani anaweza kukana haki zake zote kwa ajili ya Yesu Kristo? Nilipochunguza na kutafakari vizuri zaidi, niligundua  upole aliouzungumza Yesu katika mstari huu alimaanisha yafuatayo: 
1.  Mtu akidharauliwa ananyamaza.
2.  Mtu akifanyiwa fujo, anastahimili.
3.  Mtu akikataliwa anakubali.
4.   Mtu ambaye hatashtaki ili apate haki yake.
5.   Mtu asiyepiga kelele akinyimwa haki yake.
Ni yule asiyetaka haki kwa ajili yake mwenyewe, bali anataka haki kwa ajili ya wengine – mara nyingi anataka haki kwa ajili ya wanyonge, walala hoi, wajane, maskini, wasiojiweza, watoto, viwete, na watu kama hao.
 Katika tafakari hii nimejiuliza swali hili:
Je watu ninaokutana nao na wakasikia maneno au kuona matando yangu, wanamwone Yesu?
 Nilisita kutoa jibu kwa sababu upande wangu lilkuwa ni la!
 Ndipo nikamlilia Yesu na nikamwomba, Bwana Yesu niumbie UPOLE ili niweze kuirithi nchi.

Hii ndio tafakari yetu ya leo, Amina

Sunday, February 21, 2016

KESHO YETU IKO MIKONONI MWA NANI?

February 21



Kuna wimbo mmoja wa zamani ambao una maneno haya namjua anayeishikilia kesho na anayeshikilia mikono yangu. Tunatakiwa tujiulize swali moja kama hatuna mamlaka na kesho kwanini bado tunaendelea kupanga kuhusu maisha yetu ya kesho? Mungu ndiye anayeendesha maisha yetu na hatima yetu ya kesho na anajua kesho yetu itakuwaje la msingi sifa na utukufu uwe juu yake

Hata viongozi wa siasa pamoja na jitiada zao za kuongoza nchi bado hawana mamlaka na nguvu ya kuiona au kuishi kesho; mipango yetu yote inaishia leo, hivyo kesho yetu ni kwa kudra ya Mwenyezi Mungu. Hivyo hakuna kiongozi yeyote zaidi ya Mungu ambaye ndiye anayeijua hatima yetu ya kesho.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa sisi ni wanadamu tunaoishi leo huo ndio ukweli mtupu tupende kuamini au kuwa na kiburi cha kutoamini hivyo.

Mwenyezi mungu anajetoa ahadi kwetu kuhusu kesho; kama mwenjili Mathayo 6:34 anavyosema basi msisumbukie kesho kwa kuwa kesho itaisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake. Au tukisoma kitabu cha Yakobo 4: 13-16 haya basi ninyi msemao leo au kesho tutaingia katika mji Fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida: walakini hamjui yatayo kuwa kesho. Uzima wenu ni ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo kasha kutoweka. Baada ya kusema Bwana akipenda tutakuwa hai na kufanya hivi na hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisisfu kotekwa namna hii ni kubaya.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa tunatakiwa kumtamamini mungu zaidi katika kila jambo tulifanyalo kwani katika mikono yake ndipo neema yote ya maisha yetu imo. Hivyo ni Mungu tu ambaye anajua na anamiliki kesho yetu; ndio maana hatujui hata mbingu inafanana vipi, kwani kesho yetu imejaa utukufu wa ajabu na amani ya kweli sio kama leo yetu ambayo tunaishi iliyojaa kila aina ya tabu na uozo.

Lakini kesho yetu ili iweze kuwa katika mikono yetu lazima tujijengea tabia ya kuwa na imani dhabiti. Kwani kwa imani tunakuwa na hakika ya mambo ambayo hayaonekani lakini yanatarajiwa nasi. Na kuwa na imani ni kinyume cha kuwa na woga. Je tunawoga kuhusu kesho? Tujikumbushe kuwa kuwa ukiwa mwoga katika maamuzi yako na katika maisha yako ni wazi kuwa huna imani na Mungu hutegemea sana dunia hii.

Tafakari yetu ya leo inatukumbusha kuwa kama hujui kesho yako wewe mwamini Mungu yeye ndio mwenye haki miliki ya kesho. Tuondoe wasiwasi  na kujihakijishia kuwa Mungu atandenda yote kwa ajili yetu; ni muhimi kwetu kutekeleza majukumu yetu nay eye atafany sehemu yake;

Tukumbuke kuwa tunatakiwa kumwamini na kufuata maelekezo ya Mungu ili tuweze fanikiwa ili kuweza kuifikia kesho , na njia pekee ni kwa maombi sala ni salaha pekee ambayo itatufungulia njia ili tuweze ifikia kesho yetu. Tukisoma 1 Wathesalonike 5: 17-18 ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika kristo yesu.

Tafakari yetu ya leo inatukumbusha maneno yaliyoandikwa na Mwenjili Mathayo 6: 33 -34 Basi utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbuke kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Hivyo wapendwa hatuna sababu ya kuhofu kuhusu kesho kama tumejikabidhi wenyewe katika mikono ya Mungu. Hatuna sababu ya kuhofu kwani tunajua kuwa Mungu ndio tegemeo letu na yeye peke yake ndio mwenye hati miliki ya  kesho yetu. Amen



Saturday, February 20, 2016

RAFIKI YUPI NI BORA KATIKA MAISHA YAKO

February 20

Tafakari ya leo tujitathimini kuhusu urafiki wetu ambao mwisho wa maisha yetu hapa dunia utatupa sisi thawabu kubwa zaidi; Je rafiki yako bora ni yupi? hili ni swali ambalo tunapaswa kulizingatia kwa nafasi ya aina yake ili tuwe na amani ya kudumu ndani ya maisha yetu ya sasa na hapo baadae. Amina

ILI TUWEZE KUTAFAKARI VYEMA TORATI YA MUNGU TUONDOE KIBURI MOYONI MWETU



February 19
Tafakari ya leo tuangalie agizo la Mungu kwa wana wa Israeli wakati wa uongozi wa Nabii Joshua: Mungu alimwagiza Joshua kwa kuwaambia kuwa Joshua 1:8 kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
Huu ni ujumbe mzuri katika tafakari yetu ya leo; kwani maagizo haya yanatufundisha kuwa jukumu letu ni kutekeleza maelekezo ya Mungu na kwa kufanya hivyo Mwenyezi Mungu wetu atakuwa yuko juu ya maisha yetu. Tukitafakari na kufuata mwongozo kupitia nukuu hii ni wazi kuwa tutapatiwa chochote tunachohitaji, iwe utajiri, mafanikio katika maisha yetu, ndani ya familia zetu, sehemu zetu za kazi na ndani ya jumuia zetu.
Lakini tunakazi kubwa ya kufanya ili kufikia mafanikio haya ukumu letu kubwa ni kusoma kuelewa na kutafakari neno mungu na kisha kuishi kulingana na neno hilo siku zote za maisha yetu; sio jambo la mara moja. Tafakari ya leo inataka sisi tujenge mazoea ya kulitafakari neno na sheria za mungu siku zote za maisha yetu.
Ni ukweli amabo pengine hatuuelewi kuwa Mungu hajetuahidi sisi kuwa atatupa busara, lakini anajua kama tutasoma na kuelewa yaliyoandikwa na kuagizwa katika kitabu cha torati tutaweza kuishi na kufanya mambo yetu au maamuzi yetu kwa busara kubwa sana.
Tujue kuwa neno lisiondoke kinywani mwetu linatufanya sisi kuwa karibu sana na Yesu. Na agizo hili litakuwa ni chachu ya sisi kujua kuhusu ukweli wa Mungu na miujiza yake kwetu, na ukweli ambao hatuwezi kuujua kuhusu yeye kama hatutakuwa tayari kusoma na kuelewa na kutafakari kitabu hiki.
Je sisi wafuasi wa Kristo tunatimiza wajibu wetu kulingana na kitabu cha Torati? Tu wakweli kwa kiasi gani? Wawajibikaji kwa kiasi gani, tunazingatia sheria za Mungu na za nchi kwa kiasi gani? Je tunakumbuka ahadi ya Mungu kuwa tukitimiza ahadi zake tutapata neema ndani ya maisha yetu; siri kuwa ya mafanikio kulingana na kitabu hiki cha Torati ni UTII: Tukumbuke kuwa utii huleta amani, utii ni ufunguo pekee ambao Mwenyezi Mungu Kupitia Bwana wetu Yesu Kristo ametufungua milango yote ya baraka kwetu. Je tunatumia funguo hii ipasanyo?
Tafakari ya leo inatuonyesha kuwa tunashindwa sana kutimiza maelekezo ya Mungu kuhusu utii na kutufanya tukose baraka nyingi sana. Je wewe na mimi utii wetu kwa Mungu uko kwa kiwango gani? Maagizo ambayo Mungu alimpa Joshua yanatusaidiaje sisi leo? 
Je tunatafakari neno la Mungu Mchana na Usiku? Au maisha yetu ya kila siku yamechukua nafasi ya kwanza ndani ya maisha hivyo hatuna muda kabisa wa  muda wa kutafakari Torati ya Mungu  kwa dhati kabisa? 
Kama tunafanya hivyo bado tunaendekeza kiburi chetu ndani ya mioyo yetu jambo ambalo Mwenyezi Mungu alipendi sisi tufanye. Ondoa kiburi chako na tuanze kutafakari neno la Mungu.

Hii ndio tafakari yetu ya leo; Amina

Thursday, February 18, 2016

ASANTE MUNGU KWA UKARIMU WAKO KWETU:

February 18;

Tafakari ya leo inatuelekeza katika kumshukuru Mungu kwa wema wake wote juu yetu; Mwenyezi Mungu kupitia Mwanae yesu Kristo anatupenda sana na tunatakiwa tuendelee kumshukuru sana kwa kadiri alivtotutendea sisi waja wake; Mungu ni mwema kwetu; Tuna kila sababu ya kumshukuru kwa wema wake hivyo tuendelee kumtolea matoleo yetu ya kushukuru Amina.

Wednesday, February 17, 2016

WAJIBU WETU NI NINI KWA MUNGU KATIKA MIJUMUIKO YETU?


February 17,

Tafakari ya leo hebu tuangalie dhana ya  mijumuiko wa wakati wa kumwabudu Mungu. Kanisa linawajumuisha wapendwa katika kutimiza wajibu mmoja mkubwa kwa kumwabudu, kumsifu na kumshukuru Mungu; hata yale makanisa ya kwanza kabisa katika mijumuiko yake yalikuwa na lengo moja kubwa kumsifu Mungu, kwa sala na nyimbo na neno la shukrani.

Tafakari yetu ya leo inatumbusha kuwa makanisa ua mijumuiko yetu ya imani iwe na lengo la kutenda haki ya kumsifu Mungu, kumshangilia Mungu na kwa Baraka zake kupitia mikusanyiko yetu tumepewa uwezo wa kuwaombea wenye shida mbalimbali, za magonjwa, vipato na maisha mema yenye kibali cha Mungu. Tuanajua katika makanisa yetu tuna washiriki ambao wanauwezo wa kifedha kuliko uwezo wa kanisa. Kamwe tusiwageuze hao kuwa miungu watu wetu, kaw kuwasifu wao zaidi kukiko Mungu kwa vile wao tunawaona.

Tukisoma kitabu cha 2 Wakorinto 4:15  kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ilineema hiyo ikiongezwa sana kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe . Kuishi kwa imani. Tukumbuke kuwa Mungu ndiye atupaye sisi mkate wetu wa kila siku, ni yeye pekee awezaye kutupa sisi mbegu  na mazao yetu yakaongezeka mara dufu.

Hii inatakiwa kuwa ni sehemu ya maisha yetu sisi wakristo kwa kuendelea kumpa sifa na mtukufu Mungu wetu kila siku; kama 2 wakorinto 9: 11 inavyotuambia mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Hivyo hili linatakiwa kuwa ni jukumu letu la kila siku. Tukumbuke kuwa sio tu tunapata wokovu toka kwake bali tunapata kila kitu toka kwake. Kama sio Mungu unapata wapi jeuri ya afya njema?

Paulo katika kitabu cha Waefeso 5:3 anasisitiza kuwa  lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wotewa kutamani, kama iwastahilivyo wakatakatifu. Wala aibu wala maneno ya upuuzi wala ubishi; hayo hayampendezi bali afadhali kushukuru. Hivyo Tafakari ya leo unasisitiza katika kushukuru, kushukuru kushukuru. Tunapofungua midomu yetu tujiepushe na maneno yote mabaya, machafu ambayo hayampendezi Mungu au jirani yako. Bali tufunguapo midomo yetu imiminike kwa maneno ya shukrani. Tuombe kujazwa na Roho wa bwana kwani yeye ndiye kioo cha shukrani atatupa maneno mazuri ya shukrani.

Sala na kushukuru iwe ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, tunatakiwa tuanze sana kujijengea utamaduni wa kushukuru na kutoa shukrani kwa kila kitu na kwa wakati wowote; tukianza  kujenga utamaduni wa aina hii hata maisha ndani ya Jumuia zetu yatabadilika na tutabarikiwa sana, kwani katika Kristo unakaa utimilifu wote wa mungu kwa jinsi ya kimwili.

Paulo alipokuwa akiongea na Wakolosai 3: 15, 17 aliwaambia Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Na kila mfanyalo kwa neno au kwa tendo, fanyeniyote katika jina la bwana yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa tuendelea kusali bila kuchoka ikiwa ni sehemu ya muhimu ya maisha yetu katika kusifu na kushukuru kwa Mungu wetu. Sala ni kitu ambacho kinatakiwa kuwa cha furaha daiam na unafurahia kufanya hivyo, lakini kama wewe wakati unapomshukuru Mungu kwa sala  unakuwa huna furaha ujuwe kuwa bado unatawaliwa na kumilikiwa na mambo ya ulimwengu huu. Hivyo ukijikuta katika wakati huu inatakiwa umwombe roho Mtakatifu akubadilishe na atakupa furaha ya kweli wakati unasali.


Tafakari ye leo wakati tunaendelea na kipindi hiki cha toba tunatakiwa kufurahi kila wakati, tusali kila wakati, na tumtolea Mungu shukrani kila wakati.  Mungu anatupenda san asana na anataka sote tushiriki naye katika karamu ya mwisho tukiimba na kusifu pamoja naye hii ndio tafakari yetu ya leo.

Tuesday, February 16, 2016

KATIKA KIPINDI HIKI CHA TOBA TUMWIMBIE BWANA ALELUYA


February 16

Tafakari ya leo tunatakiwa kuendelea kumwimbia Mungu na kumpa sifa wakati wote: Ni jukumu letu kuomba msamaha wa njia zetu mbaya na dhambi zetu na kisha kumsifu yeye, katika raha na mateso, na wakati wote wa maisha yetu;

Utukufu na sifa apewe yeye sasa na hata milele yote amina. 

Monday, February 15, 2016

Asante Mungu kwa Kunibariki Mimi Zaidi KULIKO mimi ninanyostahili;

Februari 15

Tafakari ya leo tumshukuru Mungu kwa njia ya sala:

Asante Bwana kwa Baraka zako zote na isitoshe  kwa mwongozo ulionijalia   kwa kipindi cha miaka hii yote ya maisha yangu. Asante Mungu kwa kunibariki mimi zaidi kuliko mimi ninavyostahili. Najua mimi nastahili kidogo lakini wewe umenipa mimi zaidi kuliko mimi nina stahili kwa sababu  hiyo nina kila  sababu ya kushukuru kwa upendo wako wote.

Asante Mungu kwa ajili ya kunikinga, kunirekebisha na kunibadilisha mimi kuwa mtu bora kulingana na ,matakwa yako: Naomba unisaidie kutambua kuwa wakati wewe unafunga mlango mmoja ambao nimeuzoea kumbe wakati huu huo unanifungulia mlango  mwingine ambao unataka mimi kutembea kwanye  njia hiyo kuelekea kwenye huu mlango mpya. Naomba nisaidie mimi pia kutambua kwamba nitakavyo mimi inaweza kuwa sivyo wewe ulivyo nipangia mimi kuwa au namna bora kwangu. Labda itasababisha mimi kuwa mbali na mpango wako ambao ni mkubwa kwa ajili maisha yangu.

Bwana, basi mimi kukubali kila siku ninayojaliwa maisha ni kama zawadi. Basi naomba unisaidie kufuata njia ya kuchagua kilicho bora  kwa ajili yangu. Naomba nisaidie mimi kuwa mtu wa  shukurani kwa kile wewe baba umenijalia na si kuwa na wasiwasi kuhusu mahitaji yangu. Naomba nikumbushe mimi kuwa wajibu wangu ni kuwahudumia wengine ambao wanahitaji msaada wangu.

2 Mambo ya Nyakati 7:14 Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia kutoka mbinguni, na kuwasamehe dhambi zao na kuiponya nchi yao.

 Mungu, Mimi nimejawa na woga leo. Maisha yanaonekana kuwa si ya  uhakika na nje ya udhibiti. Nakumbuka kwamba Biblia inaniambia upendo hufukuza wasiwasi. Wewe peke yako ni Upendo, hivyo nina imani kuwa utatoa hofu ninayojisikia na badala utanipa nguvu na tumaini na kujiamini katika Bwana wetu yesu Kristo aliyekamilika katiak kila kitu.

Mungu, natoa mikono yangu ili iweze kufanya kazi yako; mimi natoa miguu yangu ili niweze kwenda njia yako; mimi natoa macho yangu ili niweze kuona kwa kadiri ambayo unataka mimi kuona; mimi natoa ulimi wangu ili niweze kusema maneno yako kulingana na nguvu ya Roho Mtakatifu; mimi natoa mawazo yangu ili kwamba Unaweza kufikiri ndani yangu; mimi natoa roho yangu kwamba Unaweza kuomba katika mimi.

Zaidi ya yote, mimi nakupa moyo wangu upate upendo ndani yangu yaani  upendo wa Baba na upendo wa wote wanadamu. Mimi natoa nafsi yangu nzima, Bwana  naomba  ukua ndani yangu, hivyo na Wewe anaishi ndani yangu na matendo yangu yalingane na dhumuni langu hapa duniani.

Bwana unajua kila kivuli cha mateso yangu; Wewe unaishi kwa ajili yangu na baba yako kamili:;Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote na si juu ya akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako;(Mithali 3:5-6).

Bwana wetu Yesu naomba nisaidia, kwani unajua unataka mimi niwe. Basi naomba nipe nguvu, imani na tumaini, na zaidi ya yote, nipe mwongozo kila mmoja na kila siku. Mimi basi kwenda na kukupa udhibiti. Katika jina la Yesu, Yesu alisema,;Yeye ambaye ni wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu ;(Yohana 8:47).Hakika mkono wa Bwana si mfupi hata usiweze kuokoa, wala sikio lake pia wepesi kusikia Lakini maovu yako [dhambi] yamewafakanisha sisi na Mungu;. Na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone hata yeye hataki kusikia; ( Isaya 59:1-2).

Kama wewe kubaki ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni chochote unataka na itakuwa aliyopewa na wewe (Yohana 15:07).

Kila siku mimi naja kwako Wewe Bwana hasa siku hii ya leo, sina haja ya baadhi ya ziada naomba uniimarishe kupitia uso wako bila wewe mimi si chochote naomba bwana uwe karibu yangu niweze kuimarisha nguvu ya kifanya kulingana na matendo yako na kuniondolea hofu yangu.


Naomba uniimarishe, ili niweze kushinda hofu ambayo iko mbele yangu; kwa nguvu zangu mwenyewe, mimi siwezi kukabiliana na  changamoto iliyombele yangu, najua Kuna wakati binadamu tunatumia maarifa iliyotujalia lakini hayasaidii bila uwepo wako;hivyo tunahitaji nguvu kutoka kwako  itusaidie kubeba kile ambacho kipo mbele yetu. Hii ni Tafakari yetu ya leo Amina

Sunday, February 14, 2016

ZABURI 133:1: TUWE WAMOJA

February 14 



Tafakari ya leo tunaagalia Tazama! Jinsi ilivyo vyema na jinsi inavyopendeza  Ndugu kukaa pamoja kwa umoja:

Je katika maisha yetu tunafurahia faraja ya kukaa pamoja kama ndugu: iwe ni ndugu wa kuzaliwa au ni ndugu tuliounganishwa na imani kuwa sisi ni wamoja na tumezaliwa ili tuweze saidiana;

Je kwa mwelekeo wa jamii yetu ambayo imetawaliwa na maasi, mauaji, ubakaji, rushwa, na mengine mengi je bado tunanafasi ya kuishi kulingana na Zaburi hii;

Je ni katika wakati gani tunaunganishwa zaidi katika katika umoja huu? Tukumbuke kuwa watu wote upendo mambo mazuri , bila kujali hayo mambo mazuri wanayapataje; ni vyema tukayapata haya mambo mzazuri kama bibilia inavyotufundisha kupitia njia za Mungu kwa kadiri ya mafundisho yake.

Tafakari katika zaburi ya leo ni kuwa inatuhamasisha sisi kujenga umoja na upendo, tunajua kuwa sisi kama binadamu sio viumbe tulio kamilika lakini tusitumie udhaifu wetu katika kuvunja mafundisho na amri za Mungu ili tujipatie maisha mazuri kwa njia ambazo sio sahihi na kuvunja umoja, kuharibu amani ndani ya jamii yetu na kuleta mafarakano kupitia matendo yetu yasiyo faa.

Tukumbuke kuwa umoja wetu uliojengwa juu ya Kristo yesu ni bora kuliko kitu kingine chochote kile. Tukumbuke kuwa Mungu ni Kisima cha Umoja wetu na upendo wetu. Tukitaka kuwa na furaha ya ajabu lazima twende kwake.

Tafakari ya leo kutoka katika hii zaburi inatukumbusha mambo matatu, mosi ni jambo njema wapendwa wanapoishi kwa kupendana na kuwa na kauli moja katika maamuzi, jinsi ya kunagalia mambo katika kutekeleza majukumu ya jumia yao na pale wanapokuwa wote wakifikiri katika mlengo mmoja wenye kheri na ukweli kwa manufaa yao na jamii inayowazunguka.

Pili wanapokuwa pamoja katika upendo wa kweli na sio wa kinafiki japo kiakili kila mtu anaouwezo wa kufikiri toufauti lakini wakakubalia katika upendo maamuzi yao. Ni jambo ambalo tunatakiwa kulitekeleza kila siku katika maisha yetu na hii itatusaidia kuwa na Jamii inayo mpenda na Kumwogopa Mungu kwa kukuaji wake.
Tatu ni Baraka ya pekee kwetu tukiwa wamoja, tukisali, katika kazi zetu, katika mijumuiko ya furaha au tabu kama Mtume Paul 2 Wakorinto 6:1 anavyotukumbusha Nasi tukitenda kazi Pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Tunapofanya kazi pamoja hatufanyi peke yetu tunafanya pamoja na Mungu; hivyo ni rahisi katika umoja wetu kupinga dhambi.

Mungu anapenda umoja wetu, ni jambo linamfurahisha sana hasa umoja wenye amani, upendo na ukweli: Mungu huchukia umoja unaoleta mafarakano, matabaka katika jamii. Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa Umoja ni zao jema kwetu hutuletea furaha ya kweli na ustawi wa jamii zetu.

Kwa hiyo Umoja ni kitu kizuri kwa sababu kinatutakatifusha sisi na tunaitwa watu wa Mungu. Umoja ni kitu kizuri kwa sababu kinatuuisha sisi kwani inatupa nafasi ya kutenda mambo yetu kama watu wa Mungu. Umoja ni kitu kizuri kwa sababu ni mapenzi ya Mungu sisi kuwa wamoja


Hii ndi tafakari yetu ya leo Jamii yetu tukiweza kuishi kwa umoja na upendano na ukweli hatutahangaika na matendo yote mabaya yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Amina

TUMEPATA WOKOVU KWA DAMU YA YESU MSALABANI

February 13


Tafakari ya leo tujikumbushe kuwa Yesu, alikubali kufa msalabani kwa ajili ya maondoleo ya dhambi zetu; Alikubali mateso yote kwa ajili ya sisi kukubalika tena mbele ya macho ya bwana baada ya kumwasi na kuishi maisha ambayo yalikuwa hayampendezi Mungu.

Basi tutafakari wimbo huu na kukubali kuacha njia zetu mbaya. Amina


Friday, February 12, 2016

TOSHEKENI NA MISHAHARA YENU:



February 12

Tafakari ya leo tufungue mioyo yetu na tusikie "Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake.  Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa.  Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu."`

"Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?  Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu”.

Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?  Akawajibu, Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo. Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini?  Naye akawaambia, Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa. 

Nao askari wakamwuliza, "Na sisi tufanye nini?  Naye akawajibu, Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu."

Tafakari ya leo natamani kulizungumzia neno hili  Toshekeni na mishahara yenu:

Neno  hili ni zito japo lilizungumzwa kipindi kirefu nyuma lakini tunaendelea kulishuhudia leo tunapowaangalia watendaji wetu katika serikali zetu; Neno hili linatufundisha uadilifu, uwajibikaji kulingana na maadali  na kanuni za kazi ambazo zinatulazimu sisi kama watendaji wa Taifa kuweka mbele matakwa ya Taifa na sio masihahi binafsi;

Najiuliza tena  Neno hili linamaana gani kwa taifa letu? 
Kama nchi na wananchi wake tunahitajii uhuru wa kiuchumi ambao unatokana na viongozi wetu waridhike na mishahara yao; kinyume chake kama hawataridhika na mishahara yoa na kuweka mbele masilahi yao vitendo vya  rushwa na ufisadi ambao unarudisha maendeleo ya Taifa nyuma sana vitadhidi kuendelea.

Tafakari itukumbushe sisi  Kama Taifa na kama Raia na watendaji ambao tumekula kiapo cha utii na maadili bora ya uwajibikaji kwa Taifa letu kuwapa wananchi wanyonge zawadi kubwa ya  uhuru  wa kiuchumi  ni ili kila mmoja wetu aweze kuyafurahia  zawadi pekee rasilimali  ambayo Mungu amelijalia Taifa hakuna atayepingana name kuwa  nchi yetu imefurikakwa  asali na maziwa tazo ni wachache tu ambao wanafaidi kwa kutoridhika na mishahara yao. 

kwa kipindi kirefu tumeona kuwa nchi yetu  Tanzania iliyokuwa ikifurika neema  ya rasilimali sasa imegeuka; kwa wengine imekuwa ni nchi inayofurika machungu; matendo yaleyale ya kifisadi, ya ukandamizaji, ya unyanyasaji ambao  Farao aliwatendea wana wa Israeli huko misri miaka hiyo; lakini kwa kuangalia falsafa hiyo ya matendo ya Farao ndio tunaona Namna watendaji wetu walikokabidhiwa dhamana ndani ya Taifa letu  ambao sio waadilifu wananyatenda sasa yanaenda kinyume na uhuru tuliopewa kama zawadi kuto kwa Mungu ambao kila mmoja anastahili kufurahia na kufaidi asali na maziwa yanayofurika katika nchi hii. Na sio kwa kikundi kidogo cha watu.

Yohane Mbatizaji a usitadhi kabisa anayafafanua makundi yaliyokusanyika uwiano sahihi wa toba. Kulingana na Yohane matajiri wanaotakiwa kuangalia haki ya maskini, "Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo."(Lk 3,11), kwa watoza ushuru waepuke rushwa na matendo ya kifisadi "Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa."(Lk 3,13) na kwa maaskari wazingatie haki "Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo.
Toshekeni na mishahara yenu."(Lk 3,14).

Leo hii ndani ya Taifa vitendo hivi vimeshamiri tena kwa kiasi kikubwa katika jamii yetu, na pengine kila mmoja ameshiriki kwa namna moja au nyingine katika uovu huu, moja kwa moja au kwa kutokuwajibika ipasavyo katika eneo lake la kazi na hivyo kusababisha mianya katika kukua kwa matendo haya maovu. Tafakari ya leo inatuasa  sisi kama Taifa inatupasa tubadilike na kuhakikisha haki na upendo vinashamiri katika jamii yetu.

Kama tutafanikiwa kuishi kwa ujumbe huu wa Yohani Mbatizaji kuwa tutosheke ni mishahara yetu mimi naamini kuwa tukiweka mbele maslahi ya nchi, nchi itasonga mbele. TUKUMBUKE KAULI YA YOHANA MBATIZAJI KWA WALE ASKARI kuhusu dhuluma:
TOSHEKENI NA MISHAHARA YENU, watu wana madaraka makubwa mishahara mikubwa na masurufu manono lakini bado wanaiibia nchi.

Je watendaji wetu wako tayari kutoa hesabu za utendaji wao siku watakapotakiwa na Mwenyezi Mungu tukiamini kuwa kazi zote hutoka kwa Mungu “Sisi tunajielewa kuwa ni watenda kazi wa saa ya kumi-na-moja katika shamba la Bwana la siku za mwisho, na kwamba ingawa mishahara yetu haijulikani  mapema, lakini hatuna mashaka kwa sababu Bwana wetu ni mkarimu”.

Tafakari hii  inatufundisha kitu kingine kipya kuwa tunatakiwa kujihadhari na tabia ya kupenda fedha, na yatupasa toshekeni na vipato tulivyo navyo kwa sababu Mungu mwenyewe alisema,

Tukisoma Ebr 13:5,6 Kwa vyovyote sitakupungukia kabisa, wala sitakutelekeza na kukuacha bila msaada. Kamwe, kamwe, sitakuacha hata kwa kiwango kidogo, kukuacha bila msaada, au kukuacha, au kukuangusha, au kulegeza mkono wangu kwako. Hakika sitafanya hivyo! Kwahiyo tunafarijika na kutiwa moyo, na kwa uhakika na ujasiri twathubutu kusema, ‘Bwana ndiye anisaidiaye.

Kwa kutosheka na mishahara yetu na kwa kuamini kuwa sisi ni wachache ambao tumechaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa saidia wengine ili waweze kupata ridhiki zao; au kufurahia asali na maziwa kwa vipaji vyetu kwa kutimiza wajibu wetu tutakuwa tunatekeleza ujumbe huu wa Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na hivi vitu vingine vyote mtapewa kwa maelefu.

Tukitenda kila kitu kwa haki kamwe hatutakosa chochote tunachohitaji unachohitaji ambacho kitakuwa ziada. Mwenyezi Mungu atakupa namna yauta kila uchokihitaji zaidi.

Imani yangu ni kama ile ya Paulo kama tutatosheka na mishahara yetu,na kuwajali wanyonge katika Kupata Riziki
zao, Na Mungu wangu atawajazeni na kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu. Hivyo tunawaomba  watendaji wetu kutosheka na mishahra yao na hivyo kutawapa muda wa kulisaidia Taifa na kuacha kuhangaika na  shughuli binafsi ambazo ziko nje ya maadili ya utumishi wao kwa msingi bora wa kimungu.


"Mungu hatakosa kuwajaza wale wote wanaoifanya kazi yake sawasawa na mapenzi yake" hii ndio tafakari yetu ya leo -amina

Thursday, February 11, 2016

SIKU 40 ZA TOBA ZIAMBATANE NA NENO MSAMAHA KWA VITENDO


February 11

Tafakari ya leo itukumbushe kuwa kwa hakika mwanandamu anahitaji upeo mkubwa wa nuru ya kiroho ambayo itaweza kumfanya azike tamaa zake na hisia zote za kulipiza kisasi; tunatakiwa kuwa na uwezo wa kujizuia na hasira, kuzikandamiza hasira, chuki kwa moyo mpana na kujenga daraja la msamaha.  Kusamehe mtu ambaye amekukosea, kuwapenda ndugu na jamaa ambao wameukata uhusiano pamoja nawe, na kuwa mkarimu kwa yule ambaye aliwahi kukunyima, kukutukana, kukusababishia hasira,kukudharau, kukudhalilisha na kadhalika sio jambo rahisi. Tumewaona hata watumishi wa Mungu ambao wanaielewa sana bibilia wakishindwa kabisa kuktekeleza kanuni hii.

Kumsamehe yule aliyekutendea yasiyo sahihi hutusaidia kutupatanisha na Muumba wetu; vile vile msamaha hudumisha mshikamano wa udugu ambao umeharibiwa. Kwa kusamehe tunaandaa njia ya kumwendea Mungu; Lakini  pasipo  imani  haiwezekani  (Waebrania 11:6). Inatufundisha kuwa mtu  amwendeaye Mungu  lazima  aamini  kwamba  yeye  yuko,  na  kwamba  huwapa  thawabu wale wamtafutao,”. Msamaha hutujengea wa kumwendea na Kuishi na Mungu katika Imani.

Kama ilivyoandikwa hakuna mwenye haki, hata mmoja” (Warumi 3:10). Mungu yuko tayari na anasubiri kumsamehe mtu anaye omba msamaha imeelezwa katika Zaburi 86:5 "Kama wewe Bwana u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao". Daudi aliweka wapi tumaini lake la msamaha? Tukisoma Zaburi 51:1 "Ee Mungu unirehemu sawasawa na fadhili zako kiasi cha wingi wa rehema zako uyafute makosa yangu. Mathayo 6:14-15 Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba wenu wa mbinguni atawasamehe ninyi bali msipowasamehe watu makosa yao wala Baba yenu hatawasamehe makosa yenu." Wale wamesamehewa husamehe. imeandikwa Waefeso 4:32 "Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma ninyi mkasameheane kama na Mungu katika kristo alivyowasamehe ninyi."

Kusamehe kwa kweli hakuhesabu makosa. imeandikwa Mathayo 18:21-22 "Kisha petero akamwendea akamwambia Bwana ndugu yangu anikose mara ngapi nami ni msamehe? hata mara saba? Yesu akamwambia sikwambii mara saba bali hata saba mara sabini." Katika kusamehe Yesu ametukomboa kutoka kwa dhambi na mshahara wa dhambi. Wakolosai 2:13-14 inatueleza kuwa "Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu aliwafanya hai pamoja naye akisha kutusamehe makosa yote akisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake iliyo kuwa na uwadui kwetu akiondoa isiwepo tena akaigongomea msalabani."
Zaburi 51:7-12 "Unisamehe nami nitakuwa safi, unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko dheluji unifanye kusikia furaha na shangwe, mifupa ilio ponda ifurahi. usitiri uso wako usitazame dhambi zangu uzifute hatia zangu zote Ee Mungu uniumbie moyo safi uifanye upya roho iliyo tulia ndani yangu usinitenge na uso wako wala roho wako mtakatifu usiniondolee unirudishie furaha ya wakovu wako unitegemeze kwa roho ya wepesi."
Zaburi 32:1-6 "Heri aliyesamehewa dhambi na kusitiriwa makosa yake heri Bwana asiyemhesabia upotovu, ambaye rohoni mwake hamna hila niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa kwa kuugua kwangu mchana kutwa na kwa maana mchana na usiku mkono wako ulinilemea jasho langu likakauka hata nikawa kama nchi kavu wakati wa kaskazi nalikujulisha dhambi yangu wala sikuuficha upotovu wangu nalisema nitayari maasi yangu kwa Bwana naweukanisamehe uoptovu wa dhambi yangu kwa hiyo kila mtu mtauwa akuombe wakati unapopatikana hakika maji makuu yafurikapo hayatamfikia yeye."
Wale walio wanyonge moyo wako mbele ya Mungu na wala kutambua hatia yangu, haijafika hali ya kwanza ya kukubalika. Tunahitaji kuokolewa kutoka katika aina zote za tabia zetu mbaya pamoja na misukumo ya ndani inayotushurutisha kufanya mambo fulani mabaya: kama vile, kusema uongo, hasira inayomfanya mtu atukane watu, tamaa mbaya za mwili, uchungu, kutaja machache tu.
Hatuwezi kujiokoa wenyewe kutoka katika dhambi au kuigeuza tabia yetu kwa kujitegemea wenyewe kama vile Simba asivyoweza kuamua awe mwana-kondoo (Warumi 7:18). Dhambi ina nguvu nyingi kuliko nia yetu ya kufanya yale tuyatakayo. Lakini Kristo anaweza kukufanya wewe uwe "imara kwa uweza wake, kwa kazi ya Roho wake katika utu [wako] wa ndani" (Waefeso 3:16). Anafanya kazi yake ili kuondoa tabia zetu ziletazo uharibifu na mahali pake kuweka tabia hizi nzuri: upendo, amani, furaha, upole, uwezo wa kujitawala (Wagalatia 5:22,23). Kristo anaishi maisha yake kupitia ndani yetu, kisha tunapokea uponyaji wa kiroho, tunarejeshwa katika maisha mapya, na kuwezeshwa kuishi maisha hayo mapya.
Hakuna dhambi ambayo ni ya kutisha sana asiyoweza kuisameka Yesu anatamani sana kwamba kila mmoja wetu hatimayeawe na uhusiano mzuri na Yule aliyemkosea na kumsababishia majeraha ambayo yamejenga chuki ambayo inahitaji msamaha. Yesu anataka tupokea msamaha na utakaso wa Mungu ni; katika  imani jambo ni  rahisi na la maana sana kama tunavyofurahia kumpokea motto mdogo aliyezaliwa na kumkumbatia. Lakini kutokana na ubinadamu wetu, majivuno, kiburi, masengenyo inatuwia vigumu sana kutoa msamaha wa kweli pale tunapokosewa, tunakuwa na kiburi ambacho kinatufanya kuona kuwa Yule aliyetukosea hastaili msamaha wetu; lakini kama tunayafuata mafundisho ya yesu na mifano ambayo ametutolea katika Bibilia Takatitifu tunatakiwa tuondoe ugumu katika mioyo yetu na kuuvaa unyenyekevu kama yeye alivyovaa unyenyekevu na kuuvua Umungu kwa ajili ya makosa yetu, na alikuja kukaa nasi na ametutengenezea daraja la msamaha ambalo kila mwanadamu lazima alipite ili kuweza kukamilisha safari yake ya kwenda mbingu.

Hebu jitafakari kwa nini umekuwa na kiburi cha kushindwa kabisa kumsamehe, jirani yako, ndugu yako ambao wamekukosea kutokana na ubinadamu wao, usijali amekukosea mara ngapi angalia je wewe uko tayari kumsamehe wakati wowote ule?
Hii ni Tafakari ya leo Amina