WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Wednesday, December 13, 2017

KUMBUKUMBU YA MWAKA MMOJA: DARAJA LA UPENDO NA TABASABU LILILOMALIZA KAZI KWA USHINDI:




Leo tunatimiza mwaka mmoja toka mama yetu mpendwa mama Anna kinunda aka Mbuya atangulie mbele ya haki; furaha yetu kubwa ilikuwa jinsi ambavyo aliweza kuipiga vita yake kwa ushindi mkubwa; na kufanikiwa kushinda Tuzo na huku kuendelee kuilinda imani yake mpaka mwisho wa safari yake kama vile Mtume Paulo alivyoandika katika waraka 2 Timotheo 4: 5-8.

Mwaka mmoja unatukumbusha jinsi yeye alivyoyaweka maisha yake katika mwongozo wa Mungu akijua kuwa mapambano ambayo alikuwa akipitia na kuyafanya yalikuwa ni juu yake na Muumba wake na hakuna mtu mwingine yeyote ambaye angeweza kumzuia na kumshawishi tofauti ndio maana aliamini kuwa imani ameilinda: Silaha yake katika ushindi wake ilikuwa ni kutimiza amri kuu ya upendo, ambayo ukiitimiza vizuri utaishi maisha ya uaminifu; hivyo hakukuwa tayari kumpa shetani nafasi kwani aliishi maisha yake ili kumtumikia Mungu na sio maisha ya kujilinganisha na mtu au watu wengine: aliishi vile Mungu alitaka sisi tuishi:

Daima alikuwa akimpendeza Mungu zaidi; na sio kuwafurahisha watu wengine katika mambo ambayo sio ya kimungu; aliishi maisha ya kuwasaida sana wahitaji wale ambao walikuwa wakihitaji msaada; alikuwa tayari kujinyima yeye kwa faida ya taifa la Mungu hasa watoto na wazee ambalo lilikuwa likihitaji msaada; 

Mbuya Anna aliishi maisha ya kutimiza wajibu wake kama mkristo kwa kumpigania Kristo: alitukumbusha wakati wote tusikae chinina kusoneneka na kujilaumu kwa makosa ya jana wajibu wetu daima ni kuomba msamaha na msaada wa Mungu; amakweli Mbuya yeye alichagua fungu lililo sahihi kama Mary katika  Luka 10:41-42 : je wewe na mimi ni akina Martha tunahangaika sana na mambo ya kupita na ya Muda mfupi ya dunia hii?



Tukumbuke kuwa utawala wa Mungu kamwe hautapotea au kufa  kwani juu ya mwamba atalijenaga kanisa lake na hakuna nguvu ya kuzimu ambayo inaweza kulishinda Mathayo 16:18;Mbuya alijua kuwa neema ya Mungu na thamani ya Mungu ilikuwa kuwa zaidi katika maisha yakendio maana aliipigania kwa nguvu zote; je wewe na mimi tunamsimamo gani? Ni wakati wetu sasa wa kusimama imara kumwambia shetani sasa ondoka mbele yangu; umepoteza furaha; upendo wangu; amani yangu na nuru ya uzima wa milele sasa nimesimama na kumwomba anisamehe kwani mimi narudi katika njia iliyo sahihi aipendezayo Mungu; tumwombe Mungu Msamaha kama Daudi alivyofanya katika zaburi ya 51

Tuwe kama Mwana mpotevu aliyetambua makosa yake na kuamua krudi kwa baba na kuomba msamaha wa makosa yake:Mwenyezi Mungu anafurahi pale tunaporudi kwake na kuomba msamaha ili tuweze kushiriki karamu nzuri ya mwana kondoo aliyechinywa kwa ajili yetu;




Raha ya milele mpe bwana na Mwanga wa Milele uendelee kuyangaza maisha yake katika nuru ya Kimungu kwani ameipigana vita vilivyo: Tuzo amepata; na Imani aliilinda na sasa amevikwa Taji lile ambalo alikuwa ameandaliwa pamoja na wale wote ambao wametimiza wajibu wao wa kuishi maisha yaliyompendeza Mungu 

            AMINA                                      AMINA



 

Sunday, November 5, 2017

KAA NASI BWANA JUA LINATUA.

Nilikuwa natafakari kuhusu dhana nzima ya ujumbe huu wa kumwomba bwana akae nasi kwani jua linatua. Nimejiuliza maswali mengi ya kisalfasa. Kwa nini tumwombe Mungu akae nasi. Kwa nini tusiwaombe watu mashuhuri, wenye akili nyingi? Watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha ambao dunia inawaheshimu. Kwa nini tusiwa ombe watu mashuhuri ambao wanaongoza madhehebu tofauti ambao Wana nguvu katika dunia hii? Wasiwasi wetu unatokana na nini wakati jua linatua? Kuna siri gani kati ya jua kutua na kuomba Masada wa Mungu?

Kwa nini tunakuwa wepesi wa kumkimbilia Mungu katika mashaka yetu, na wakati wa furaha tunasahau uwepo na nguvu ya Mungu?
Kwa nini bado tunawsogopa na kuwajali wenye pesa na kusahau kuwa bila uhai ambao unatoka kwa Mungu hawa wote tunawaona muhimu katika dunia hii Si chochote.

Hii ni tafakari katika siku ya Leo,  je wewe ni miongoni wa wanaokimbilia Masada na huruma ya  Mungu? Au wanaokimbilia watu maarufu katika dunia hii.

Basi kama jibu ni ndio kimbilia huruma ya Mungu na Mungu atakaa nawe wakati jua likitua. Amina

Friday, April 7, 2017

TAFAKARI: TUJIFUNZE KUTOKUHUKUMU KWA HISIA KATIKA KIPINDI HIKI CHA MFUNGO:



Petro aligeuka na kumwona yuke mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa akimpenda sana; akumuuliza je na huyu vipi? Je kama mimi nataka kumwacha huyu mpaka nitakaporudi wewe inakuhusu nini? Wewe nifuate mimi Yohana 21:21-22. Tafakari yetu juma hili Yesu anatukumbusha umuhimu wa kuwa na kiasi katika kutaka kujua mambo ya watu wengine; Tunatakiwa kuwa watu wenye hekima na kujali Zaidi mambo yetu, tufanye kile ambacho yatupasa sisi kufanya; 1Wateselonike 4:11 tena mjitahidi kutulia na kutenda shughuli zenu,na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe kama tulivowaagiza.

Tunakumbushwa sana kujitathimini na kuacha kuingilia maisha ya watu wengine; kwa msingi huu kwamba  tukiangalia sana wale ambao wako sana katika maisha ya watu wengine; basi hawana thamani kabisa hata katika maisha yao ya kila siku; wako tayari kunena ya watu wengine na kutoa hukumu ambayo imejaa hisia kulingana na wao wanavyotaka iwe; kwa maneno mengine wanaweza kuwa chanzo cha mafarakano katika maisha ya  watu wengine katika jamii kwa ujumla. 2 Watesolonike 3:11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine;

Lakini wale ambao siku zote wao wako katika maisha ya Kimungu  Luka 2:49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? hawatakuwa na muda wa kutumia muda wao katika mambo ya watu wengine, daima watakuwa wakitembea katika busara ya Mungu na kutenda mambo yao kwa haki na uadilifu wa pekee. Wakorinto 4:5 basi ninyi msihukumu jambo kabla ya wakati wake; tukumbuke kuwa kila mtu  anatakiwa kuwa tayari kuhangaika na mambo yanayomhusu yeye  mwenyewe; Katika jamii yetu, tukumbuke kuwa kuna watu ambao wao kazi yako kubwa ni kulaumu na kukosoa tu hawawezi kuona kitu au jambo nzuri lolote kutoka kwa wengine; na pengine ukibahatika kuona nini kinaendelea katika maisha yao utashangaa kwa nini wako msitari wa mbele kuhukumu wenzao; pengine maisha yao na hukumu ambazo wanazitoa kwa wengine hazilingani kabisa.

Tafakari yetu leo inaendelea kutukumbusha kuwa  tunapoteza muda wa kufanya mambo yetu mazuri yampendezayo Mungu kwa kujihusisha  na mambo ya watu wengine; lakini utagundua kuwa jinsi kuwahukumu wengine katika mambo ambayo hayana msingi ndivyo tunavyowasaidia wao kufanikiwa Zaidi na kuwa karibu na Mungu na kufanikiwa Zaidi. Tunatakiwa kuanza kusafisha nyumba zetu kabla hujeanza kuona uchafu katika nyumba ya wengine kwa kutumia ulimi wetu.

Na pale tunapogundua  kuwa maisha hayako vizuri yarekebishe na tuyasimamie na sio kutumia muda mwingi katika kuhangaika na maisha ya watu wengine. Kwa nini uwe na uchungu na maisha ya watu wengine? La msingi ni vizuri tukajifunza kutilia mkazo maisha yetu na kuziondoa changamoto zetu za maisha. Ni rahisi kwetu kuona Kibanzi katika jicho la wenzetu na kushindwa kuona boriti katika jicho lako au langu;

Kwa kweli wakati mwingine inatakiwa tuamue kufunga masikio na kuziba macho ili tuweze kusonga mbele; chochote ambacho tutafanya hakitaweza kumridhisha kila mtu na kila mtu atatoa hukumu yake; kama tusipokuwa makini hao ni waharibifu wa safari yako ya maisha; midomo yetu  imejaa masengenyo na majigambo; midomo yetu inapinga uumbaji wa Mungu dhidi ya wenzetu; maneno kama mbaya, hana elimu ya kutosha; hana kazi nzuri; mwone kwanza: je haya maneno yanaashiria nini katika uumbaji wa Mungu; Je Yesu alipokuja kutukumbo sisi kutoka katika misha ya dhambi aliangalia vitu hivyo? Jibu hapana alitukomboa sisi kulingana na njisi tulivyo bila kuangalia ukubwa au uwingi wa dhambi zetu; na jambo njema pamoja na mapungufu yetu sote tumepokea kipimo sawa.

Tukisoma Injili ya Mathayo 7:5 Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.  inatukumbusha kuwa sisi tuko makini sana katika kuhakiki maisha ya watu wengine na mapito yake; swali la kujiuliza je sisi tunafanikiwa vipi na kupata kibali cha kuwahukumu wengine? Au nasi tumekuwa katika kundi la wanafiki kwa kupenda tu kuhukumu? Tunatakiwa kuwa kioo cha matendo yetu na busara yetu kuwa mfano kwa wengine? Tusome sana neno la mungu;

Tukisoma kitabu cha Zakaria 4:10 Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.  katika maisha vitu vinakuwa taratibu havilipuki tu kutoka kusikojulikana. Kila mafanikio yanahitaji uwajibikaji na uvumilivu. 

je unaona raha gani kuongelea  mambo mabaya juu myu mwingine? kwa nini usiongelee mazuri au pale alipokosea usimrekebishe kwa upole na kwa busara iliyojaa unyenyekevu? itakuwa ni jambo la kufurahia kwa wakati huu wa mfungo na toba ni kujifunza kutenda kila jambo kwa haki kama Yesu alivyotutendea na uthibitisho wa hili ni kitendo cha kukubali kufa msalabani kwa wokovu wetu;

ushauri wangu kama unatenda jambo njema na unahukumiwa ni wakati wa kushukuru sana kwani  unafanya jambo nzuri ambalo linawaumiza na wanataka kukurudisha nyuma; kumbuka ukiwaruhusu na kuwapa nafasi ya kukukatisha tamaa ujue kuwa  nawe mwisho wako utakuwa umefika. Kama Yesu angesikiliza kelele zote za walimu wa sheria na wayahudi ambao walikuwa wanampinga; sisi tusingeweza kupata wokovu wetu huu ambao tunaufurahia leo. La msingi ukikabiliwa na mtihani wa aina hii simama kidete na ujipanga vizuri kwani ushindi wako unakaribia. Methali 18:21 mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; na wao waupendao watakula matunda yake.

Inasikitisha sana leo kuona jamii na jumuia zetu zinatawaliwa na nguvu ya masengenyo; wivu na undumila kuwili . hivyo kwa kweli kama tunapenda kufurahia maisha mazuri lazima tujiepushe sana kuutumia ulimi wetu katika kusema mambo mabaya juu ya wenzetu. Metali 6:17 mambo ambayo yanamchukiza sana bwana Macho ya kiburi, ulimu wa uongo na mikono imwagayo damu isiyo na hatia.

Tukumbuke kuwa tunapokuwa tuko midumo juu tayari kuwahukumu na kuwalaumu na kuwahukumu wenzetu, Mungu kamwe hana muda wa kutusikiliza yeye wakati huu anafanya kama hatusikii na utuandalia adhabu,  mfano wa Yesu na kundi la watu waliompelekea mwanamke alifumaniawa katika tendo la unzinzi. Pamoja na kufafanua sheria zote kuhusiana na kosa hilo Yesu alikaa kimya kama vile hawasikii, aliponyanyuka aliwauliza swali kama kuna mmoja wenu asiye na dhambi awe wa kwanza kumrushia  mama huyu; Yohana 8:7. Fundisho hapa ni moja tu hukumu kama wewe hujetenda dhambi yeyote ile; tujenge upendo wa kweli kati yetu upendo ambao huubagui; hii ndio tafakari yetu ya wiki hii.

Amina                   Amina            AMINA

Emmanuel Turuka

2017


Thursday, April 6, 2017

DARAJA LA TABASAMU, UPENDO NA MATUMAINI LILILO MALIZA KAZI KWA USHINDI;




Tafakari ya wiki hii ya Kwaresma tunakumbuka maisha ya Mama yetu Anna Michaeli Kinunda aka Mbuya; tunayakumbuka maneno ya Yesu tukisoma Yohana 19:27 kisha akamwambia yule Mwananfunzi ;Tazama Mama Yako;Je kunasiri gani Yesu alikuwa akimwonyesha yule Mwanafunzi: Nguvu ya akina mama katika misha yetu ni kubwa sana. Upendo wao hauna mipaka;

Leo tunajikumbusha maisha ya mama Anna Kinunda (Mbuya) ambaye Mwenyezi Mungu alimwita katika makao yake ya milele tarehe 13 December 2016. Mama ambaye alikuwa amejaa furaha na Amani ya Bwana ukiondoa ubinadamu wetu ambao ni zao la kila mmoja wetu; Mama Anna alikuwa Mtu mwenye nia thabiti juu ya Mungu wake; alimtumikia Mungu kwa moyo wake wote na hakukatishwa tama na mtu au kitu chochote alisimamia kile ambacho alikuwa anakiamini; Pamoja na ukweli kuwa kifo kamwe hakizoeleki daima kinageuka kuwa ni jambo la kutisha na ambalo halizoeleki; Mama Anna alikuwa tayari kwa kifo chake na alikisubiri na kukipokea kwa unyenyeku siku ya jumatano tarehe 13 december huku akiwa akiendelea na sala zake katika kumshukuru Mungu; alikutwa akiwa amepiga magoti huku akiwa amefunga mikono yake katika ibada yake na Mungu wake; hivyo alikufa katika unyenyekevu; na furaha kubwa;


Tukisoma kitabu cha wakorinto 2 : 5 : 1-5  hofu na woga mkubwa sana ambao hugusa mioyo ya binadamu ni woga wa kifo; kifo kinatujengea  woga wa kiwango cha juu katika maisha ya binadamu kuliko woga wa kitu kingine chochote. Tunaogoapa kufa; tunaogopa  kifo pamoja na mafundisho yote ya ahadi zilizo jaa faraja ambazo tumeandaliwa baada ya Kifo; bado tumekuwa wagumu kukipokea kifo kwa unyenyekevu; bado tunakuwa na mashaka juu ya kifo; tunakuwa na imani haba na kuamini kuwa hatujui nini  kitatokea baada ya kifo; kifo kimekuwa ni tatizo la msingi sana katika maisha ya binadamu; hata wachungaji ambao wamekuwa wakihubiri kuhusu maisha yetu ya kifo ni mbinguni na yatakuwa maisha yaliyojaa furaha lakini nao wanaogopa sana kifo ; Ili tufurashie hiyo furaha ya milele lazima tufe na kifo ndio njia pekee ya kutupeleka Mbinguni  lakini sio njia ambayo tuko tayari kuipokea ; Mama yetu Anna  alikipokea kwa upendo mkubwa bila woga na alikisubiri bila mashaka yeyote.

Tukisoma kitabu cha Yakobo 4:14 14 kinatukumbusha kwa ufupi walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Na mzaburi 90:5-6 naye anatukumbusha kuwa  Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. 6 Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka. 

Kama ilivyoelezwa katika mazingira tofauti kuwa hakuna kitu cha uhakika zaidi ya kifo, na hakuna ambaye anaweza kukwepa kifo “ Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.   Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa;” Lakini tukisoma 2 Wakorinto 5: 1-2 Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni. 2 Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni; maandiko haya ya Paulo kwa wakorinto tunaelewa nini kipo mbele yetu, ukweli wote ambao uko mbele yetu, matumaiani pamoja na mtafaruku wote wa kifo. Tukumbuke kwa Mungu alishatowekea ushuhuda ambao hata kifo chenyewe hakiwezi vunja. Wafilipi 1:21 Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. 



Tukiamini katika imani tunagundua kuwa tunapokuwa katika khali ya kifo ni tendo lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu ukilinganisha ni viumbe vingine vyovyote; tendo la viumbe au mimea kufa linakuwa limekamilika na kufikia mwisho wake;  lakini kwetu sisi kama binadamu tunapoteza tu uwezo wa kutambua kibinadamu, hatuhisi chochote kulingana na ubinadamu tuliokuwa tumeuzoea; na tunakuwa hatuko tena katika ulimwengu huu wa kidunia lakini sasa maisha yetu ya kiroho yananza kulingana na matendo yetu hapa duniani. Hatuishi kwa ajili yetu wenyewe bali maisha yetu yanakuwa katika daraja jipya; ni maisha ya  kumsifu na kumshangilia Mungu siku zote; ndio wale ambao tunawashangilia kuwa wamemaliza kazi katika utukufu wa Kimungu. Maisha yao yote na malengo katika maisha yao ni kuishi katika utukufu wa Kimungu. Ndio wale ambao wananungana na Mtume Paulo aliposema Warumi 14: 7-8  Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. 8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. 

Yesu katika mafundisho yake alikuwa akisisitiza sana matendo mema; Imani ili iweze kufanya kazi yake inahitaji matendo. Imani bila matendo hakuna wokovu. Tunaamini kuwa kila muumini ambaye anaamini na anaishi kulingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu amekombolewa katika dimbwi la dhambi;

Mama Anna alikuwa ni  mwanamke aliyejaa matendo mema na kwa sadaka alizozitoa. 1 Timoteo 7-9 Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; 8 ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. 9 Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Mathayo 6:26-27 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. 26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 




Tunafundishwa kuwa hatutakiwi kusoneneka kwa kukosa thawabu za Kimungu kwa matendo yetu mabaya Yuda alisikitika kwa kumsaliti Yesu kwa vipande 30 vya Pesa; je wewe kabal ya kifo chako unahuzunika kwa jambo gani? Je matendo yako yanakupa njia sahihi ya Kufurahia utukufu wa Mungu? Je baada ya kifo wapendwa wako utawaacha katika khali gani ya furaha au unyonge kufuatia maisha na matendo yako?
Mama Anna daima alikuwa akisema kuwa nimemaliza kazi na maisha yangu kama Mkristo, nimetimiza wajibu wangu na nimewaonyesha njia kama Mkristo, na sasa niko tayari kwenda kupumzika kwa Baba. Hakuwa na mashaka wala woga wa kufa kwani alikuwa akiendelea kujiandaa kila siku na kuomba huduma za kiroho kila siku. Kwake kila siku mpya ilikuwa ni siku ya Maombi. Daima alikuwa akijiuliza mimi ni nani? Kwa nini mimi nimezaliwa? Na ninakwenda wapi? Je nimetimiza majukumu yangu kama Mkristo?

Zaburi ya 37:28-29 Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa. 29 Wenye haki watairithi nchi, Nao watakaa humo milele. 



Mithali 3: 12 Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye. 13 Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu. 14 Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. 15 Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye. 16 Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. 17 Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani. 18 Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.


Mithali 16: 6-7 Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu. 7 Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye. 8 Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu. 9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake. Mama Anna aliishi katika Imani yake thabiti huku akiwa akifanya matendo ya huruma ; nyumba yake ilikuwa ni nyumba ya mayatima , nyumba ya wahitaji; alikuwa anatimiza ili amri kubwa ya kumpenda Mungu na jirani:  aliishi kwa Imani  na uaminifu  ule uliokuwa unampendeza Mungu wetu: hii ni njia pekee ambayo itatusaidia sisi kujihakikishia, uzima wa milele na furaha ya milele tukikumbuka kuwa yeye ni tegemeo letu na kimbilio letu; yeye ni kielelezo cha msamaha  katika maisha yetu tunayoishi hapa dunia ikiwa ni sehemu ya safari ya milele;


Upedo sio maana yake tu kupenda lakini ina maana kubwa zidi ya kuweza kuweka vipao mbele vyako katika kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Kama kama utaweza kufanikiwa katika hili ndipo imani yako, matumaini upendo wa kweli utakuwa unatwala maisha yako 1 Wakoritho 13:13 Jambo ambalo wengi wanaweza kujifunza kutoka kwako hasa baada ya maisha ya hapa dunia ni kupima je vita yako ya imani uliipiganaje? Ulitimiza makukumu yako kama Kristo alivyoagiza katika mafundisho yake? Yohana 13:34 na 2 Timotheo 4:7.

Mama Anna alikuwa tayari yeye asiwe na kitu lakini Jirani yake aweze kula na kushiba au kuvaa vizuri; daiama aliyafanya hayo kwa matendo na mafundisho; daima alikuwa akitufundisha jinsi ya kuishi kwa upendo na mashirikiano mazuri; kwa msingi huu yeye na Mume wake Marehemu Mzee Alois waliweza saidia watu wengi sana kwa kuwajengea misingi mizuri ya shule; waliweza kuishi na watoto wengi ambao hakuwa na uwezo wa kwenda shule bali wao waliwachukua na kuishi nao kama watoto wa familia moja.

Je wewe na mimi tukifa tutacha nini cha kujifunza kwa watoto wetu na jumuia inayotuzunguka? Je kile tutakacho kiacha kitakuwa kimejaa , upendo, matumaini na imani? Kama vile mtume Paulo alivyo waambia watu wakoritho fanyeni kila kitu katika upendo wa Kristo; kwa hiyo; urithi ulio bora hauwezi kupatika kama hatutamwogopa Mungu; amebarikiwa mtu Yule ambaye anamwogopa Mungu na kutumainia njia zake na amri zake; Zaburi ya 112:1-2. Tukumbuke kuwa kizazi cha wamuuchao bwana kitabarikiwa.


Mama Anna aliweza kufuata mfano wa Yesu; Tunajua kuwa Yesu alikuwa mtu maarufu sana; sio tu kwa sababu aliwalisha wale watu elfu tano pale mlimani, au alifanya miujiza mingi na kuwaponya wengi; au kwa sababu alikuwa Bwana wa Mungu; bali alikuwa na vitu vingine vingi ambavyo viliweza kuendana kabisa na maisha ya sisi binadamu wa kawaida; Yesu alikuwa akiwahudumia watu wote kwa utu na ubinadamu; mfano tu mdogo wakati ule kule Yerusalemu wasamaria na wanawake walikuwa wakionekana kama daraja la pili watu ambao hawana thamani katika jamii yao. Lakini Yesu aliwa hudumia wote sawa kabisa sawa na wayahudi wengine;

Yesu alikuwa msikilizaji mzuri; tunatakiwa kujifunza kuwa wasikilizaji wazuri; na hiyo inasaidia kujua shida na jinsi ya kusaidia kwa urahisi, kwani tutakuwa katika nafasi nzuri ya kusaidia. Yesu alikuwa sio mtu wa kukimbilia kuhukumu wengine  alikuwa akiongea nao na kuwaelimisha daima alikuwa kama kiongozi na rafiki; Yesu alikuwa akipatikana kwa urahisi bila masharti au ukiritimba wowote, mtu yeyote ambaye alitamani kuongea naye alipata nafasi ya kuongea naye, na hata Yule ambaye alikuwa hawezi kuongea naye kwa sababu yeyote ile aliweza pia hata kwa kumwita tu akiwa akipita na wengi walipata msaada waliokuwa wakihitaji. Hakuwa na masharti yeyote hivyo ndivyo alivyokuwa Mama Anna aliweza kuwa karibu na kila mtu bila kujali khali yake. Jukumu kubwa ambalo liko mbele yetu tunatakiwa kuendelea kuwa makini katika matendo yetu juu ya Mungu wetu; tukumbuke kuwa tunaokolewa kwa neema na kamwe kwa nguvu zetu wenjewe; Waefeso 2:8




Nilichojifunza katika maisha ya Mama Yangu katika uhai wake wote ni Upendo wake kwa kila mtu, Imani yake ambayo haikuyumba kwa wakati wote wa maisha yake, imani ya kumpenda Mungu, na kuishi kulingana na mafundisho ya Yesu na kumtumikia kwa moyo wake wote; hata pale alipotukanwa au kudharauliwa kamwe hakufanya kiburi wala kinyongo; nilichojifunza kwake kama Mithali 22:6 leo mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapo kuwa mazee; ilikuwa ni wajibu wake mkubwa kwetu ilikuwa kuturisisha umuhimu wa imani; kwetu sote na kumtanganza Kristo kupitia amri kuu ya Upendo; muhimu zaidi amekuwa Mama ambaye ameishi sana katika ukweli na ameweza kupata thawabu ya kweli kabisa mwisho wa safari yake hapa duniani; Wafilipi 2: 16 mkishika neno la uzima, nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya kristo, ya kuwa sikujitaabisha bure;




Mama Ana hakuwa anategemea sifa za kupendwa kutoka kwa wanadamu bali alikuwa akitegemea sifa kutoka kwa Mungu. Alikuwa ni mtu Yule,aliyependa kutoa zaidi kuliko kutegemea kupata zaidi; alikuwa akitekeleza zaidi amri ya upendo na kuamini kuwa maisha yake lazima ayatoe kwa watu wengine wanaomzunguka na ambao wanamahitaji msaada zaidi;

Mama Anna alikuwa mama Mwema; ambaye daima alikuwa akizungukwa na tabasamu la upendo; pamoja na mapungufu ya kibinadamu bali alijitahidi kuishi maisha ya  kutimiza amri ya upendo; alikuwa Mama ambaye daima hakujikweza bali alikwezwa kwa matendo yake; maishani mwake alitamamni kila mtu aishi maisha ya upendo na kuwajali wengine; Mama Anna hukua tayari kuona unaishi maisha mabaya ya kumchukiza Mungu; alikuwa msahauri wa mabadiliko; alitamamni sote tuishi wa upendo kama Yesu alivyofundisha; na alitamani sote tutekeleza majukumu ya upendo yanayompendeza Mungu hapa duniani.

Alikuwa Mama wa kawaida tu; na daima alikuwa akitosheka na kile ambacho alikuwa akipata; Alikuwa na Mama ambaye alikuwa akiishi kwa kuwaMfano Bora wa wa mkiristo anavyopasa aishi; alitosheka na maisha ya kawaida ambayo yampendezayo Mungu; Mama ambaye aliyatoa maisha yake sadaka ya uwakilishi wa kweli kwetu sisi kujifunza. Aliitambua imani,alitembea katika imani; alikuwa Mwamba katika imani yake; alitembea na Mungu ndio maana leo hii Mwenyezi Mungu amempumzisha kwa amani kabisa; nasi leo tunakila sababu ya kumwita mbarikiwa kwani amepata kifo chema kilichompendeza Mungu;

AMA KWELI MAMA ANNA KINUNDA(MBUYA) AMEKUWA DARAJA LA TABASAMU, UPENDO NA MATUMAINI LILILO MALIZA KAZI KWA USHINDI;


Raha ya milele mpe bwana na mwanga wa milele umwangazie apumzike katika usingizi wa Amani na wa ufufuo wa Mungu;

Amina               AMINA                               Amina                                


Emmanuel Turuka
2017


Wednesday, March 29, 2017

TAFAKARI: WOGA KATIKA MATENDO YETU UWE SILAHA YA USHINDI




Tafakari yetu ya juma hili tunaangalia dhana ya woga katika maisha yetu; woga ni kielelezo kuwa kuna kitu kimesimama katika njia mbayo tunastahili kupita; lakini pengine kwa mantiti ya ukweli kabisa hakuna kitu cha namna hii; woga huleta wasiwasi na kutufanya kushindwa kufanikiwa malengo yetu; woga hutupotezea kabisa uwezo wetu wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi wa kufikia malengo ambayo ndio lengo la mafanikio yetu;

Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa vizuizi kama woga visiwe kikwazo katika maisha yetu hasa ya kiroho tunakumbushwa hata tukijikwaa kwenye ukuta  ni lazima tukubali kuwa kujikwaa sio mwisho wa safari. Woga ambao husabibisha akili zetu kudumaa lazima upate ufumbuzi ndani ya akili zetu. Akili zetu lazima zijue kuwa kushindwa kunakutokana na woga hatupaswi kutoa  nafasi kwani bibilia inatukumbusha kuwa neema yake inatosha katika shida zetu. Woga utupe sisi ujasili wa kupata ushindi; kushindwa kunakosababishwa na woga kuwe sehemu ya ushindi; Yesu alipokuwa akitembea juu ya maji wafuasi wake walishituka na kujawa na woga wakifikiri kuwa wameona ni jini; walipomtambua kuwa alilikuwa Yesu Petro akamwambia Yesu bwana nami naomba nitembee juu ya maji Yesu alimwita akamwambia njoo, alianza vizuri lakini kwa vile alileta silaha ya woga akaanza kuzama.

Je woga wetu hutoka wapi? Woga katika maisha yetu huletwa na watu wengine, pengine tunatamani kumpendezesha kila mtu, au kuishi kwa matarajio ya maisha ya watu wengine na kwa macho yao  hivyo kwa kuishi katika maisha ya namna hiyo huweza kutupa sisi wakati mgumu sana; lazima kutakuwa na vizingiti vingi sana lakini bado hatutakiwa kukubali kuwa vikwazo vituzuea katika maisha yetu. Tunatakiwa kuwa tayari kuruka vihunzi, na daima macho yetu yawe yanangalia mpira ili tuweze kushinda na sio kuwa watu ambao tumejaa woga. Tukiwa na mawazo ya kushindwa sio sehemu ya ushindi; kushindwa ambako kunatokana na woga ni ishara ya kutuambia sisi kuwa hatuko sawa;

Najua kabisa hatuwezi kuepuka woga lakini woga usitawale maisha yetu, hata Yesu alitawaliwa na woga alipokuwa katika bustani kabla ya safari ya mateso yake lakini kwa ujasiri mkubwa aliushinda woga na kuweza kubeba kikombe cha mateso kwa ujasiri mkubwa hatimaye kuleta ukombozi kwetu sote kwa damu yake pale msalabani.

Tukiendekeza woga basi tumeshajiwekea sisi wenyewe dalili kubwa ya kushindwa;woga unatakiwa utufundishe sisi na kutuletea mageuzi na kutufanya kuwa watu bora zaidi. Tunaposoma kuhusu maisha ya jehanamu tunajawa na woga; basi Woga huu unatakiwa utusaidie sisi tuyafuate maelekezo ya mungu katika kuishi maisha bora ambayo yanampendeza Mungu wetu. Hivyo woga utujengee sisi ushindi kama Yesu alivyofanya na leo tumekombolewa kupitia damu yake takatifu sisi sana kwa ukombozi huu jukumu letu  ni kufanya matendo mema ambayo yanampendeza Mungu.


 Ni jambo nzuri ambalo sisi binadamu tumewekewa Mwenyezi Mungu alijua uzaifu wetu kuwa kwa kushindwa kwetu ambako kunatokana na woga awetu tumewekewa namna ya kuweza kuomba msamaha. Ndio maana  ya kipindi hiki cha toba, kipindi hiki ni alama tu ambayo tunatakiwa kuishi kwa namna hii katika maisha yetu yote. Natukiweza kuishi katika namna hii tutakuwa tumefanikiwa sana sana. Kristo ametuonyesha mfano kuwa yeye aliweza kusimama kidete katika kutuonyesha mfano maisha yale ambayo Mwenyezi Mungu anataka sisi tuishi; tumepewa nafasi ya pili ya kujirekebisha na kuishi bila kutanguliza woga mbele bali kutanguliza ushujaa wa kumpigania Yesu; tunatakiwa tutambue udhaifu wetu na kupata nguvu za kuukabili udhaifu huo; tubadilishe tabia zetu; 

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa pamoja na kukabiliwa   maisha wakati mwingine yanakuwa magumu sana; kupitia kipindi hiki cha mfungo na kumrudia Mungu tumepata nafasi nyingine nzuri sana na ya ajabu sana; Mungu anaendelea kutujalia sisi siri kubwa ya ushindi wa maisha yetu na mbinu za kumshinda shetani; lazima tukubali kuendelea kujifunza na kuwa tayari kubadilika; maisha ya ushindi ni magumu na kuwa mwoga haitasaidia kushinda vikwazo ambavyo vinachelewesha ukamilifu wa safari yetu hapa duniani bali lazima tusimame imara na kuamini kuwa bila nguvu za kristo ndani yetu sisi wenyewe hatuwezi kuipigana vita hii kwa ushindi mkubwa; woga wetu utaendelea kuwako bali tukimpokea Kristo woga hauna na nafasi hata kidogo. Maisha yatendelea kuwa mazuri kwa wale wanaomwamini kristo na wako tayari kufa pamoja naye. Woga wako ukimtegemea kristo hauna nafasi kabisa na utakuwa huru; tufunge na Kristo na tufe naye msalabani kwa kuishi maisha yale ambayo kristo aliishi na kuwa alama ya ukombozi wetu ;

Huu ndio ujumbe wetu wa wiki hii ya kwaresma.

Amina            Amina            Amina

Emmanuel Turuka
2017



Friday, March 10, 2017

TAFAKARI: TUNAIPOKEAJE ZAWADI KUTOKA KWA MUNGU?


·        KWA MOYO WA SHUKRANI NA UNYENYEKEVU?
·        KWA MOYO WA MALALAMIKO?


Katika kipindi hiki cha Kwaresma tafakari yetu ya wiki hii inatuuliza swali moja je sisi ni watu wa kushukuru au ni watu ambao tumejaa malalamiko tunavyoyakabili maisha yetu ya kila siku?

Tujikumbushe kuwa Mungu wetu ni Mungu aliyejaa huruma na ni Mungu ambaye ni mtoaji; lakini sisi kama wana wake je tunatambua ukuu wa mungu katika maisha yetu? Je zawadi zote ambazo Mwenyezi Mungu anatujalia sisi tunazipokeaje, tunazipokea kwa moyo uliojaa shukrani au tunazipokea kwa kuturidhika na kwa malalamiko? Tatizo letu tunasahau haraka sana zawadi ambazo Mungu anatujalia katika maisha yetu, na daima tunaishia kuwa watu ambao tunakuwa wa kulalamika zaidi na sio kushukuru na kuomba bila kuchoka.

Lakini tunabahati kubwa pamoja na malalmiko yetu Mwenyezi Mungu bado anaendelea kutupenda na kutujalia sisi mahitaji yetu. Tukumbuke jinsi wana wa Israeli walivyokuwa wakilalamika lakini kila siku mpya Mwenyezi Mungu aliendelea kuwalinda na kuwapa mahitaji ambayo walikuwa wakihitaji kwa siku hiyo.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima tuendelee kufunga na kusali tukiomba msamaha kwa kosa hili kubwa la kulalamika hata pale tunapotendewa mema. Tunatakiwa kupokea kila zawadi tunayojaliwa katika mikono ya shukrani. Tukumbuke kuwa mbele ya Mungu malalamishi sio kitu cha kujivunia. Unyenyekevu, moyo wa shukrani ndio vitu vya kujivunia mbele ya wenzetu na Mungu.

Tukumbuke kuwa wakati mwingine Mungu anatupa sisi zawadi ambazo hatustahili kabisa. Je kuna zawadi gani kuwa zaidi ya Kumtoa mwanaye aje ulimwenguni ateseke na kufa kifo cha aibu kwa ajili ya dhambi zetu ili sisi nasi tufurahie utukufu wa Mungu Mbinguni. Kwa kuja kwake sisi tumekombolewa.

Tunavyo kumbuka mateso ya Yesu, tujikumbushe kuwa mateso yake yamekuwa ufunguo ambao umetufungulia sisi uzima wa milele. Yesu ameweza kutusaidia sisi kukata kiu ya kufurahia maisha maisha yetu ya baadae; kwani tukiweza kuishi ndani yake kwa matendo kamwe hatuwezi kuogopa kifo; kwani uchungu na ugumu wa Kifo Yesu ameshauondoa.

Kwaresima hii itukumbusha kuwa Yesu ndio mkate kweli wa uzima ambao unasafisha kabisa njaa, wajibu wetu ni kuendelea kuishi kulingana na mafundisho yake. Na kubwa ambalo tunakumbushwa leo tuache kulalamika bali tupokee zawadi zote tunazopewa kwa upendo na kwa moyo wa shukrani ili neema ya mungu ibaki juu yetu.

Ili kuweza kuijiimarisha katika zawadi hii Yesu anataka sisi leo kuendelea kujifunza umuhimu wa zawadi zote ambazo tunazipata leo kupitia watumishi wake ambao wamepewa uwezo wa uwakilishi wa Kristo katika maisha yetu. Wao ni binadamu kama sisi bali ni chombo kilichobarikiwa katika kutekeleza mafundisho ya kutuelimisha sisi umuhimu wa kupokea zawadi zetu kwa moyo mkunjufu uliojaa upendo na shukrani na sio kujijengea tabia  ya kulalamika  na kuona kuwa Mungu anatuchukia;

Tukiweza kupokea zawadi hii ndipo tunapotambua ukuu wa neema ya mungu juu yetu; Mungu anatujenga sisi katika imani kubwa kama tutaweza kuacha kabisa malalamiko, tutakuwa tumekomaa katika imani. Katika tafakari yetu ya wiki hii tumpe asante mungu kwa upendo wetu kwetu kwa kutujalia sisi ridhiki yetu ya kila siku na tunamshukuru kwa kutujalia sisi pia mkate wa uzima jambo la msingi ambalo ndilo linalotawala tafakari yetu je sisi tunapokeaje hii zawadi kubwa ya ukombozi wa maisha yetu?



Emmanuel Turuka

Wednesday, March 1, 2017

SIKU 40 NI KIPINDI CHA KUTENDA MEMA (KWARESMA/LENT)





Kwaresma ni kipindi ambacho tunakumbuka maisha ya Mwokozi wetu Yesu kristo na kazi yake ya ukombozi wa maisha yetu katika safari ya maisha yetu baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa maneno mengine Kwaresma ni kipindi maalum ambacho wakristo
Wanatakiwa wayaelekeze maisha yao zaidi katika sala, kufunga na kuwasaidia wale ambao wanahitaji masaada. Ni kipindi zaidi cha kutafakari na kufanya toba na kumrudia Mungu.

Kipindi cha Kwaresma  kinajumuisha siku arobaini za toba na shukurani kwa Mungu. Tukisoma katika maandiko matakatifu tunaweza kuona jinsi  watumishi wa Mungu manabii ambao Mungu aliwapa majukumu mazito baada ya kufunga na kusali kwa siku 40; Walitakiwa kutubu kabla ya maombi au ahadi ambazo Mwenyezi Mungu aliwaandaa kuzipokea kwa faida ya watu wao.  Musa alifunga siku 40 kabla ya kupokea amri kumi za Mungu “Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.” (Kutoka 34:28). Nabii Eliya alifunga siku 40 kabla ya kuonana na Mungu kwenye mlima Orebu: “Akainuka, akala akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu mlima wa Mungu.(I Wafalme 19:8)

Kipindi cha kwaresma siku 40 kwa mfuasi mtiifu wa kristo lazima atapambana na mitihani mingi; kwa vile shetani naye anakuwa kazini kupinga mema ambayo unataka kufanya lazima utakutana chaweza taabu, wasiwasi, uzuzu, woga, kukosa msimamo au mwelekeo.

Tukumbuke maisha ya Yesu kabla ajeanza utume wake Katika Agano jipya, Yesu alifunga siku 40 (jangwani) akipambana na majaribu kabla ya kuanza kazi yake. Alijaribiwa na shetani mara tatu; lakini aliyashinda majaribu ya shetani;

Tukumbuke kuwa Kufunga ni jambo linalomsaidia mtu kutafakari kuhusu mambo ya kiroho na kumkumbusha kwamba kuna mambo muhimu maishani kuliko mali na chakula. Funga inatusaidia sana sisi kujenga uhusiano mzuri pamoja na Mungu. Na kubwa zaidi funga inatusaidia sana sisi tuaminio  katika kutimiza ahadi ya kumshukuru Mungu na kuonyesha kwamba mtu amejitoa kwake. Ninafunga kwa sababu ninampenda Mungu.

Yesu alitoa taadhari ambayo sisi tunapotekeleza Kwaresima hii ya mwaka 2017 tujiepushe kujiona kuwa sisi ni bora zaidi; mimi ni mwadilifu zaidi kuliko mwenzangu; Tuondoe dhana ya kuhukumu; hii ni sawa na kujisifia mwenyewe wakati hujui mwenzako pia amefanya nini ambacho kimempendeza Mungu. Tumkumbuke Yule farisayo mwenye kiburi aliyejiona kuwa bora kuliko wengine kwa sababu alifunga kwa ukawaida, unaonyesha wazi kwamba Mungu anakataa mtazamo kama huo. Yesu anatukumbusha kuwa tendo la kufunga ni tendo jema lakini ni tendo linalohusisha nafsi yako na Mungu na hupaswi kuwaambia wengine kwamba umefunga.

Wote wakitambua hali yao ya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu hutumia wakati huo katika kutubu, kuungama na kukiri makosa yao mbele ya Mwenyezi Mungu. Toba hiyo hufanyika kwa njia mbalimbali. Licha ya kufanya hiyo toba, pia wanashauriwa kusali zaidi wakati huo wa toba. Tunavyofahamu sala ni mahusiano ya karibu sana ya binadamu na Muumba wake. Hapo hutoa sala za kushukuru, sala za kuabudu, sala za kumsifu Mwenyezi Mungu, sala za kumtukuza, sala za kuomba msamaha kwa dhambi mbalimbali tulizomkosea Mwenyezi Mungu na pia zile ambazo tumewakosea binadamu wenzetu.

Maisha yetu sisi kama binadamu maisha yetu yamejaa matendo maovu; hivyo kipindi cha kwaresima ni wakati mzuri wa  kujipatanisha na Mungu kwani kwa kutenda dhambi sisi tunajifarakanisha na Muumbawetu, na hivyo tuhitaji upatanisho. Siyo hayo tu, pia huyo binadamu huwa amejitenga na binadamu wenzake anayeishi na kushirikiana naye. Kwa hiyo jambo la tatu analopaswa kulifanya mtu yule mwenye kufanya toba ni kufanya matendo mema, yaani kutoa sadaka kwa ajili ya maskini na wale ambao ni wanyonge katika jamii yetu.

Ni matumaini yetu kuwa Mfungo huu wa Kwaresima utakuwa ni wenye manufaa kabisa kwa Waumini wenyewe binafsi, lakini pia kwa ndugu na marafiki wote. Tukumbuke kuwa hasira ya Mungu itatulizwa tu ikiwa waumini tunafunga na kujinyima mambo mbalimbali. Tukiwa na imani tunasadiki kuwa kwa mfungo huo wa waumini wakristo utasaidia kabisa kwa kutuletea neema.

Jambo jingine ambalo Waumini Wakristo wanapaswa kulizingatia ni kwamba imewapasawa kutoa sadaka zao kwa moyo wa ukarimu. Wakati huu wa Mfungo ni wakati hasa wa kutenda matendo mema na kuacha uchoyo na ubinafsi. Waumini wanapaswa kuwa wema zaidi, na kuwa wakarimu zaidi. Hivyo ndivyo inavyowapasa wale wote ambao wameamua kufunga na kumrudia Mwenyezi Mungu.

Tukumbuke kuwa Kweresma inatupasa itubadilishe kuwa waumini bora kabisa sisi tu kwa siku 40 bali kwa amsiah yetu yote mpaka tunakufa mfungo, utusaidie kutubadilisha kabisa kutoka ndani ya mioyo yao. Tunaweza kusema kuwa lengo la Mfungo ni kumbadilisha binadamu, ni kufanya mageuzi ya ndani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Mfungo mtukufu ni kipindi cha kubadilika kutoka ndani na kuwa binadamu aliye mwema na mkarimu zaidi. tunanatakiwa kuonyesha upendo wao kwa maskini.Basi tunaomba kwa njia hii ya Mfungo mtukufu waumini wazidi kujipatanisha na Muumba wao, na pia wajenge mahusiano mema na ndugu zao wanaoishi nao. Kwaresima ni mabadiliko, Kwaresima ni mageuzi, Kwaresima ni kuwa na upendo zaidi wenye ukarimu zaidi. Kwaresima ni kuahidi kuacha mabaya na kuzingatia mema na hivyo Kwaresima ni kuwa watu wapya waliojaa huruma na upendo kwa Mungu na jirani.
  
Nawatakieni kwaresma njema ya mwaka 2017

Emmanuel Turuka

Kalamazoo Michigan