WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Wednesday, June 8, 2016

MWENYE MASIKIO NA ASIKIE



June 8

Marko 4:23

Tafakari yetu leo tuangalie kwa makini maneno ambayo Yesu aliwaambia wafuasi wake Mwenye Masikio na asikie. Ni jambo nzuri sana Yesu alitaka sisi tujifunze kuhusu kusikia na sio tu kusikia bali kusikia Neno la Mungu. Nafahamu kuwa wajibu mmoja wa Mkristo ni kuhudhuria ibada au mijumuiko ya neno la Mungu; lakini wasiwasi mkubwa wa Yesu ulikuwa kuwa hatujui jinsi ya kusikiliza na kufuata maelekezo ya mafundisho hayo kwa sababu tunasikiliza vitu tofauti kabisa; Kama hatutakuwa makini katika kusikiliza basi hata lile neno la Mungu litakalo fundishwa kwetu litakuwa linagonga tu ukuta na kurudi bila faida yeyote; Tukiwa na mioyo migumu tutambue kuwa hata neno la Mungu halitaweza kupenya katika masikio yetu kwani tayari Moyo unakuwa umeshafunga hata Ngoma za masikio. Tukiwa na moyo wa mashaka tunaweza kupokea neno la mungu lakini hatutaweza kabisa kuliishi tutaanguka tu; tukiwa na Moyo uliogawanyika neno la Mungu halitakuwa na nafasi kwani masikio yetu yatakuwa yamegawanyika katika kufuatilia vitu vingi ambavyo havina faida; Lakini tukiwa na Moyo safi moyo imara hufungua ngoma za masikio katika kusikiliza Neno la Mungu na neno litazaa matunda bora kwa maisha yote.

Tafakari yetu inatuonyesha kuwa Yesu anasisitiza jinsi ambavyo tunatakiwa kusikiliza Luka 8:18 Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho. Yatupasa kufungua Mioyo yetu ili tuweze kusikia vyema na kulielewa na kasha kuliishi neno la Mungu. Tukumbuke kuwa wote tumejaliwa neema ya kuwa na masikio; wote tumepewa neema ya kuuelewa ukweli lakini kupitia masikio yetu ni dhahiri kuwa sio kila mtu anapata huu utukufu. Sio kila mtu ananamini; anakuwa tayari kuupenda utukufu wa Mungu; na kinachotufanya kuwa karibu au kuupokea utukufu huu ni neema ya masikio na bahati mbaya sio kila mwenye masikio na anasikia sauti ya Mungu; Masikio mengine ni sawa na mapambo tu katika kulisikiliza neno la Mungu.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa tunatakiwa kusikiliza kwa utii na utulivu; tujuwe kuwa hili ni jukumu letu la msingi tutake tusikate tunatakiwa kusikiliza kwa unyenyekevu na utii; ili tuweze kulielewa na kuliishi; Tunatakiwa tuwe kama mwanga tunavyosikiliza Neno la Mungu; mwanga hufungua mengi; mwanga huweka wazi vitu vingi; mwanga huongoza; ndivyo itupasavyo kufungua masikio yetu tusikilizapo neneo la Mungu; tunachotakiwa kuendelea kufanya ni kuendelea kuomba neema ya Mungu ili kujenga misingi mizuri ya kusikia na kusikiliza neno la Mungu na kuondoa vikwazo katika kusikia neno la Mungu.

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa imani inakuja kutokana na kusikia. Warumi 10:13 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Hata tukisoma waraka wa Yakobo 1:19. Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;  hivyo tukijua kusikiliza kama itupasavyo tutakuwa wanyenyekevu katika maamuzi yetu Mengi; na tutatumia busara ile ile Yesu aliitumia alivyoishi duniani. Tukiwa wasikilizaji wazuri itatupunguzia mashaka mengi sana; na ni kweli kuwa wengi wetu tunakuwa tayari tunamambo mengi tayari katika akili zetu kutokana na mazingira yanayotuzunguka na hata hatutoi nafasi inayotupasa katika kusikiliza neno la Mungu; hivyo ni wajibu wetu sasa tuanze kubadilika na kutoa nafasi ya kutosha katika kusikiliza neno la Mungu.

Hii ni tafakari yetu ya leo Amina

Emmanuel Turuka





No comments:

Post a Comment