WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Monday, March 14, 2016

TUNAUTUMIAJE MUDA/WAKATI WETU?





March 14

Zaburi ya 90
Tafakari ya leo tuangalie jinsi ambavyo tunatumia muda wetu. Je tunautumiaje muda wetu na kwa faida ya nani? Tukumbuke kuwa tunatakiwa kutumia muda wetu vizuri hasa tunapofahamu kuwa hapa dunia tuko katika mpito wa maisha yetu; na mbele ya Mungu hakuna dakika wala sekunde ambazo tunaweza kuzirudisha nyuma. Tukumbuke kuwa Mbele ya Mungu kila siku inafungua ukurasa mpya tunapaswa kuwa makini jinsi ambavyo tunatumia muda wetu. Tunaaswa  kuwekeza ili tuweze kupata furaha na mafanikio ya kweli.
Tunaishi kwa kufuata majira kwa kujua kuwa muda ni muhimu katika maisha yetu hivyo hatutakiwi kucheza nao. Katika mahangaiko yetu mara nyingi tunapigana sana na wakati tukikimbizana huku na huku na pengine bila mafanikio yeyote. Lakini tunamwona Bwana wetu yesu Kristo yeye pamoja na kuwa na kazi kubwa ya ukombozi wetu kamwe muda haukuwa tatizo kwake; alikuwa anajua kuwa ana muda mfupi wa kutimiza kazi ambayo alikuwa amepewa na Mwenyezi Mungu, bado alikuwa  na muda wa kuwawekea mikono na kuwabariki watoto; Muda ulikuwa rafiki kwake.
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa Mungu anaishi katika wakati wote yeye ndiye aliyeumba muda huu ambao sisi leo hii unatuendesha mbio. Lakini tukisoma bibilia kwa makini tutajua namna ya kuutumia muda ili uwe rafiki na sio adui. Mwenyezi Mungu anatukumbusha kuwa tunatakiwa kuthamini muda na kuufanya kuwa kitu muhimu sana katika misha yetu. Kila siku ipitayo ina maana kubwa sana kwetu.
Je tunajua thamani ya mwaka mzima katika maisha yetu? Kipimo rahisi cha kupima wakati kwa mwaka mmoja, tunaweza kupima kwa kumuuliza mwanafunzi ambaye amefeli katika masomo yake na ameshindwa kuendelea na shule;
je tunajua thamani ya  saa moja tumuulize mfanya biashara ambaye ndege yake ilicheleweshwa na akakosa mkutano wa kibiashara na akaishia kupata hasara kubwa katika biashara zake.
Je dakika moja ina thamani gani tunaweza kujifunza kwa mtu ambaye amepata shida ya Moyo na maisha yake yakaokolewa na wafanyakazia wa dharura;  
na je sekunde ina faida gani muulize mtu ambaye amekoswa koswa kugongana uso kwa uso na gari nyingine. Hawa wote watakusimulia nini maana ya kujali wakati: na wangeweza kupata nafasi mpya wangeutumia wakati vizuri sana.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa  jana ni historia, kesho haiko mikononi mwetu; muda ambao tunao ni sasa ambao ni zawadi; muda upo jinsi ulivyo sisi tunatakiwa tujibadilishe ili kwenda sambamba na muda huo lakini kamwe hautungoji sisi; muda ni kitu ambachohakibadiliki;

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa pamoja na mbio zetu zote za maisha bado tuna nafasi nzuri ya kuweza kuratibu Muda wetu; kama nafasi ya kwanza tutampa Mungu na nafasi ya pili kwa ajili ya familia zetu; tukikumbuka kuwa kila dakika ni zawadi kutoka kwa Mungu hivyo tunapasa kuitumia vizuri. Hivyo wajibu wetu sio kuhangaika Kuutawala muda bali tunatakiwa kujitawala wenyewe na kuutumia muda vizuri. Kama waefeso 5:14 -15 Hivyo husema, Amka wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na Krsito atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima. Tunatakiwa kutembea kama watu wenye hekima sio wapumbafu.
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa kama hatutaweza kutumia vizuri muda wako hivyo mtu mwingine atakusaidia kuutumia muda wako vizuri. Muda ambao tumepata uko sawa kwa wote hivyo hakuna mtu ambaye amepata muda mwingi zaidi. Bibilia kupitia Luka 12:34 kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapo kuwapo na mioyo yenu.
Tujikumbushe hadithi ya  Mariamu na Martha:  Mariamu aliyeketi miguuni pake yesu, akasililiza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema Bwana huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Mwambie anisaidie. Bwana akamjibu akamwambia Martha, Martha, unasumbuka na Kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi. Lakini kinatakiwa kitu kimoja tu: Mariamu amelichagua fungu lililo jema ambalo hataondolewa.

Yesu anatufundisha hapa kuwa Imani na kazi ni vitu vinavyo tegemeana na vyote ni muhimu kwa ukuaji wetu wa mwili na kiroho. Lakini tunatakiwa kutumia muda wetu mwingi katika katika kutafuta ufalme wa Mbinguni; ndilo fungu ambalo Mariamu alichagua; hili ni fungu sahihi kwetu sote. Bibilia inatufundisha kuwa matumizi yetu ya muda na maisha yanakwenda sambamba. Tunatakiwa kuwa makini na matumizi ya Wakati ili ulete faida ya kweli mwisho wa maisha haya tunayoishi.

Tafakari ya leo inatukumbusha Wakati huu tulio nao ndio haswa wakati wa kumtumikia Mungu. Kama 2 Wakorinto 6:2 kwa maana anasema, wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndio sasa tazama siku ya wokovu ndiyo sasa. Tukumbuke kuwa Mungu ametupa sisi wakati mzuri wa kumjua Yesu kama mwokozi wetu na kupitia yeye tufurahie maisha ya mbinguni lakini tunatakiwa kutumia wakati wetu vizuri.
Nahitimisha tafakari yetu ya leo kwa kutoa ushauri kuwa wakati ni huu wa kumtumikia Mungu; tukiangalia hivi sasa jinsi migongano mingi inavyoikabili dunia; tukumbuke mafundisho ya ya bibilia kuwa, mwisho wa dunia utakavyokaribia kutakua na vita, tetesi za vita, kusalaitiana; mauaji; majeshi kuasi; tauni na balaa la njaa kila mahali; tunatakiwa kutumia muda wetu vizuri tusije chelewa kama  Mithali 1:28 inavyosema ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; watanitafuta kwa bidii wasinione. Leo ndio siku yetu wa wakovu kwani Mwenyezi Mungu yuko tayari kusikia sauti yetu na kilio chetu. Wakati ni huu wa kumrudia  na kumtumikia Mungu wetu.

Hii ndio  Tafakari  yetu ya leo Amina.

Emmanuel Turuka







No comments:

Post a Comment