NINI TUMEJIFUNZA TOKA KWA HAYATI REMMY ONGALA aka DOCTOR?
Wapenzi wa muziki wa dansi na Muziki wa Injili tumepokea kwa masikitiko habari za kifo cha mkongwe wa muziki/Injili doctor Remmy Ongala ambacho kimetokea tarehe 13/12/2010.
Swali la msingi kwa nini kifo chake kimewagusa wengi? Majibu ya swali hili ni mengi sana kulingana na kila mtu na mtazamo wake na kwa namna ambavyo alikuwa anamfahamu na Doctor Remmy kupitia nyimbo na maisha yake mengine ya kawaida na kwa namna ambavyo aligusa hisia zetu.
Kwa upande wangu nitazungumzia hasa URITHI gani ambao Remmy ametuachia sisi kama wananchi wa Tanzania. Marehemu Remmy ametuachia jambo moja kubwa la kuwa wakweli katika katika kutekeleza majukumu yetu bila kumwogomba mtu yeyote Yule; ni Mwenyezi Mungu tu wa kuogopewa. Remmy alikuwa mkweli, muungwana na mwelimishaji wa aina yake.
Aliweza kukitumia kipaji chake katika kuwatetea wanyonge kwa kupitia musiki wake, alikuwa anajitahidi sana kutoimba sana nyimbo za mapenzi na badala yake kuimba zaidi nyimbo zilizokuwa zinagusa na kueleza matatizo ya wanyonge watu wa kipato cha chini, ambao hawana sauti amabyo wakiitumia inaweza kuwasaidia kutatua mataizo yao.
Aliwahi kusema huko nyuma kuwa dunia hii ni gereza wanyonge ambao hawana uwezo wa kuyafurahia maisha kwa vile hawana uwezo hivyo wao ni wakuamuriwa tu nini wafanye ni sawa na wafungwa. Mafanikio ya wanyonge lazima yatokane na furaha ya matajiri ambao furaha yao ndio nafuu ya wanyonge na hasira yao ni kiyama kwa wanyonge.
Doctor Remmy kwa kweli Alifanikiwa sana kueleza ukweli wa maisha wa wanyonge kama umasikini, tatizo la ukimwi na namna ya kujikinga na maambukizo, ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu, rushwa mapenzi na uvumilivu kwa kupitia muziki wake; ndio maana kumbi zake zilikuwa zinawapenzi wengi wa Muziki.
Nakumbuka sana ule wimbo wake wa Mambo kwa soksi ambao ulikuwa unahamasisha sana watu watumie kondom katika swala la mapenzi ili kujikinga na maambukizo ya ukimwi; wimbo huu ulionekana kupingana na maadili kwa wakati huu, lakini ukweli Doctor Remmy ulikuwa miongoni mwa elimishaji wa ngono salama kwa jamii. Aliitumia sanaa yake kuwa kweli ni kioo cha jamii katika kutatua tatizo. Hatukuwa tayari kuukubali ukweli huu, tukitumia kigezo ujumbe huu ulikuwa umewasilishwa kunyume na utamaduni wetu. Bila kuogopa ukweli huu Remmy aliuweka bayana, je leo hii Jamii yetu tunaielimisha vipi? Tukubali au tukatae myonge myongee lakini haki yake mpe Remmy alikuwa ameona mbali na alikuwa anawaonyesha wanyonge haki hiyo ya gharama nafuu kwa usalama wa maisha yao;
Yako mengi ya kusema la msingi tu muziki ambao ulikuwa ukipigwa na kutungwa na Doctor Remmy ulikuwa na hisia kali za kuelimisha kulingana na mazingira; tutamkumbuka sana kupitia nyimbo zake; tutamkosa kwa sababu hatutapata tena mashairi na na uimbaji wa hisia kwama wake;
Mwenyezi Mungu amempa Baraka za maisha yake kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia kwa kumuwezesha kutumia muda wake wa kutosha kabla ya kifo chake kumwimbia yeye; na kwa kulisoma neno lake kwa utulivu zaidi na kwa makini ampaka pale alipowita kwake katika mapumziko ya milele; kama wengi walivyosema tumempenda sana mpendwa wetu Remmy lakini Mungu amempenda zaidi; Yeye alitoa na Yeye Ametwaa, jina lake na lihimidiwe milele Amin
No comments:
Post a Comment