WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Wednesday, August 31, 2016

KUTEMBEA NA YESU NI FURAHA



August 31

Luka 10:41-42

Tafakari yetu leo tunaangalia umuhimu wa kutembea na Yesu katika kila hatua ya maisha yetu; dhana ya kutembea ni kitu cha kawaida katika maisha yetu; na tunapotembea katika maisha yetu ya kila siku mara nyingi watu wanaotuzunguka wanatuangalia jinsi tunavyotembea; na hata wakti mwingine wanakuwa na maoni tofauti kuhusiana na matembezi au kutembea kwetu; hii ni tofauti unapomkaribisha Yesu aje kutembea nawe; tukiwa tunatembea na Yesu tofauti yake kubwa ni kuwa uwe unaangaliwa na watu; au matembezi yako yana furaha au ugumu; hiyo haijarishi la msingi tunatakiwa kukumbuka kuwa kutembea na Yesu kunahitaji hatua tofauti kabisa na umakini mkubwa: tukisoma Waefeso 2:8-10  Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.  inatukumbusha kuwa kutembea na Yesu kunahitaji neema ya Mungu;

Tafakari yetu tukiangalia na kusoma Waefeso 4:1-3  Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. tunatambua kuwa Mtume Paulo anaainisha jinsi tunavyotakiwa kutembea na Yesu kwa kuzingatia vipau mbele hivi; uvumilivu; unyenyekevu; ubinadamu; upole; kuvumiliana;kupendana;kuimarisha umoja wa waamini kwa kufanya kazi kwa bidii; tukiweza kuzingatia haya kutembea kwetu na Yesu ni rahisi sana na tutakufurahia sana; kama tutaweza kutembea katika msingi huu kinachotokea hapa ni kuwa watu wengine watapata nafasi ya kwanza katika kila kitu unachofanya;watathaminiwa zaidi , watapendwa, wata saidiwa hivyo ndivyo Yesu anavyotamani iwe;

Tafakari yetu msisitizo yatupasa kufanya nini ili tuweze kufurahia kutembea kwetu na Yesu; Waefeso 3:20-21 Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele Amina. Ili kuweza kutimiza ndoto hii lazima tuweze kujitambua na kukua kiroho; Kukua kiroho kunaendana na kutimiza vipau mbele vyote ambavyo Paulo ameviainisha;

Tafakri yetu inatukumbusha somo nzuri kutoka kwa injili ya Luka 10:38-40 Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.  Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Tunachojifunza hapa kuwa kati ya hawa ndugu wawili mmoja aliamua kutembea na Yesu katika matendo yake na Mwingine alikuwa bado anahangaika na maisha ya dunia; sio kwamba mambo aliyokuwa anayafanya yalikuwa hayafai lakini sio katika kipau mbele cha maisha ya kiroho; kama anavyofundisha Luka 10:41-42 Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa;

Tafakari yetu basi inatufundisha kuwa kwa habari hii njema wewe leo hii ni nani kati ya Mariamu au Martha; Je uko karibu na Yesu kwa kiasi gani? Je unaweza kujihesabu kuwa unatembea na Yesu katika kila hatua ya Miasha yako? Hili ni swali la msingi katika tafakari yetu ya leo, hatujechelewa kumkaribisha Yesu katika maisha yetu; Amina

Emmanuel Turuka





No comments:

Post a Comment