June 10
Matendo ya Mitume 2:38
Tafakari ya leo
inatukumbusha umuhimu wa kufanya Toba ya kweli; Kufanya toba maana yake ni
kufanya mageuzi katika akili yako na katika tabia yako. Toba mara nyingi
inahusisha mageuzi ya kuacha dhambi na kumrudia Mungu. Hapo tunatakiwa
kubadilisha akili zetu jinsi tunavyofikiri na kutenda; kubadili mtazamo wetu na
hivyo itatusaidia kubadilisha tabia zetu ambazo kabla ya Toba zilikuwa mbaya.
Ni mabadiliko ya jinsi tunavyoishi kutoka katika njia ambayo sio sahihi ambayo
inakwenda kinyume na maagizo ya mungu. Kwa maneno rahisi kabisa Toba ni
kuyaweka maisha yetu chini ya ulinzi wa Mungu na kutenda na kuishi kadiri ya
maelekzo yake na maagizo yake. Matendo ya Mitume 3:19 Tubuni basi,
mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako
kwake Bwana;
Tafakari yetu
inatukumbusha kuwa tukiangalia
mafundisho ya Yohana Mbatizaji tunaona jinsi gani alikuwa anafundisha kuhusu
kutubu na kubadilisha tabia zetu za kibinadamu ili ziendane na Tabia za Kimungu.
Tukisoma Luka 3: 10-14 Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu
mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa,
wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia,
Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao
wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala
msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu. Tabia za kidunia
tunajifikia sana sisi wenyewe na kusahau kabisa kuwafikiria wenzetu; hatuweki
masihahi mapana ya jamii yetu tunaangalia zaidi faida gani mimi nitapata sasa.
Tafakari yetu leo inaturudisha katika mstari wa
kuishi vyema ili kuweza kuyafurahia maisha yetu sio sasa tu bali na hata
baadae. Tumwangalie mfalme Daudi alitenda dhambi kubwa sana lakini alimrudia
Mungu akamwomba msamaha kwa makosa yake na kuahidi kubadilisha tabia yake. Kwa
Kufanya toba ya kweli Mungu alimsamehe. Ni fundisho kwetu Mungu wetu ni mwepesi
sana kusamehe. Unamkumbuka Yule mtu wa mataifa alipokwenda kusali hakuinua hata
kichwa chake alikiri dhambi zake na kuomba msamaha. Na Mungu alimsamehe;
tunakumbuka kisa cha mwana mpotevu alijua makosa yake alijua kuwa tabia yake
ilikuwa mbaya na ilikuwa haipendezi Mungu; akaamua kurudi nyumbani na kuomba
msamaha wa kweli mbele ya Mungu na baba yake na akasamehewa;
Tafakari yetu inatukumbusha kuwa Mungu
alimwondoa Adamu kutoka katika bustani ya Eden kwa kufanya dhambi moja; sasa je
sisi leo kama hatutafanya toba ya kweli tunafikiri tutaweza kushiriki furaha ya
milele kwa dhambi zetu nyingi zinazotuzunguka? Mara nyingi tuna sikia watu
wakisema mimi sina dhambi ya kuomba msahaha au kufanya toba; je wewe ambaye
unasoma tafakari hii huna kitu ambacho umefanya kinyume na utaratibu wa Mungu
ambao unahitaji msamaha? Jitatimini mwenyewe na ujipime kama kweli hutitaji
toba ya jambo lolote lile ulilomkosea Mungu; nafikiri kuwa tunatakiwa kuwa watu
wa Toba kila wakati;
Tafakari yetu leo bado inatukumbusha kuwa toba
inaleta mabadiliko ndani mwetu na hasa katika akili zetu na kukubali kuacha
dhambi na kuyaendea maisha ya utakatifu; Toba ya kweli inakwenda sambamba na
Imani; Imani ya kweli huzaa toba ya kweli hivyo ni wajibu wetu kuendelea
kuimarisha imani yetu na kwa imani tutaweza kuyagundua matendo ambayo yanahitaji
Toba ya kweli.
Hii ndio Tafakari yetu ya leo-Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment