June 19
Ezekieli: 22:30
Tafakari yetu ya leo inalenga katika kushukuru kwa baraka ya Baba kama Mzazi kiongozi; Mtazamo sahihi mbele ya Mungu:
Zaburi ya 111:10 kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana
akili njema, sifa zake zakaa milele. Tukisoma Marko 12:30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na
kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwan nguvu zako zote. Yohana
14:15 mkinipenda, mtazanishika amri zangu. Yakobo 4:7 Basi mtiini Mungu.
Mpigeni Shetani, naye atawakimbia. Mtazamo wetu lazima heshima, utii, upendo, uaminifu, unyenyekevu,
utii, worshipful, na sala.
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuiangalia upya tena wajibu wa
Baba katika familia hasa katika malezi na makuzi ya Taifa ambalo tugemeo letu
ni vijana ambao lazima watokane na malezi Bora ya familia ambayo ndio msingi wa
familia bora. Tukisoma kitabu cha Ezekieli 22:30 kinatukumbusha kuwa Nami nikatafuta
mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali
palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Mungu
anaonyesha Kiongozi bora wa familia na jamii anayemtaka ambaye atasimama kati
yake na nchi; je wewe leo kama baba wa familia uko tayari kuchukua haya
majukumu?
Tafakari yetu inatuonyesha
kuwa baba hodari; Baba mwema; baba
anayekubalika mbele ya Mungu, lazima awe tayari kuyabeba majukumu kama baba;
anatekeleza wajibu wake kama baba; anafikiri kama baba; anatenda kama baba;
aliyejaa upendo na msamaha; akitekeleza haya
yote anapata sifa ambazo Mungu ameziweka kwa Kiongozi wa familia; lakini
bibilia inatukumbusha kuwa Baba hodari lazima awe ni mtu mzuri, na mtu mzuri ni
Yule ambaye anafuata mafundisho na maandiko ya bibilia na kuweza kuwalea watoto
katika misingi mizuri ya kiimani. Kama Mithali 3:5 inavyotukumbusha kuwa jukumu kubwa la Baba liwe; Mtumaini Bwana
kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zake
zote tunawajibu kama Baba kukiri na kuomba mwongozo katika malezi ya watoto
wetu, tukumbuke kuwa hakuna kisichowezekana mbele ya Mungu wajibu wetu ni
kusimamia imani yetu.
Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa sisi kama
baba wa familia tujue kuwa kwa imani tumekombolewa, na imani ili iweze kuwa
dhabiti utiifu ni lazima; Kama baba tunatakiwa kuonyesha mfano mzuri ndani ya
familia na kwa kufanya hivyo hata malezi ya vijana wetu yatakuwa rahisi sana
Waefeso 2:8-9. Sisi kama wanaume (Baba) tuna tabia ambayo tunataka daima kuwa
juu na kutoa maamuzi na wengine wote wayafuate hata bila kukaribisha ushiriki wa mawazo mengine toka ndani ya
familia. Tunatakiwa tujifunze kutoka kwa Mama zetu ambao kwa maumbile yao na
busara zao ni rahisi sana kujikabidhi kwa kila wananchokifanya katika mikono ya
Mungu. Yesu kwa kutambua ubabe wa sisi wanaume ndipo aliposema Mathayo 18:3 akasema,
Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika
ufalme wa mbinguni. Watoto na wanawake
wana tabia ya kuamini na kutegemeana.
Tafakari yetu leo
inaendelea kutukumbusha kuwa kwa wanaume kama watatekeleza majukumu yao kwa
utaratibu ambao unatakiwa Mungu atakeleza haya kwetu: tukisoma Isaya 40:30-31 Hata vijana watazimia na kuchoka, na
wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa
kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala
hawatazimia. Hiyo ni ahadi ya Mungu kwetu kama tunasima kwenye mstari sahihi;
wakati waraka wa Paulo kwa Wafilipi 4:19 unatukumbusha kuwa ya Na Mungu wangu
atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu,
ndani ya Kristo Yesu. Wagalatia 5:16-18 inatukumbusha kuwa Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho
kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya
mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
Tafakari yetu
inatukumbusha kuwa jukumu la baba ni kuleta matumaini ndani ya familia; Kuleta
upendo; amani ; umoja; heshima; uwajibikaji wa kila mtu ndani ya familia;
bibilia inatukumbusha kupitia Wakolosai 3:21 kuwa Ninyi akina baba, msiwachokoze
watoto wenu, wasije wakakata tama. Huu ni ujumbe mzuri sana ambao tunatakiwa
kuuzingatia ili kuleta matumaini ndani ya familia yetu na umoja wa
familia. Ujumbe huu kutoka Wakolosai 3:
15-20 ni muhimu sana katika siku hii ya leo Na amani ya Kristo iamue mioyoni
mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi
ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo,
na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa
tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu
katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana. Ni ujumbe ambao umetoa mwongozo mzuri sana
katika kusherekea siku hii ya leo ya Kumbukumbu ya Akina baba
Hii ndio tafakari yetu ya leo Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment