June 8
Marko 4:23
Tafakari yetu leo
tuangalie kwa makini maneno ambayo Yesu aliwaambia wafuasi wake Mwenye Masikio
na asikie. Ni jambo nzuri sana Yesu alitaka sisi tujifunze kuhusu kusikia na
sio tu kusikia bali kusikia Neno la Mungu. Nafahamu kuwa wajibu mmoja wa
Mkristo ni kuhudhuria ibada au mijumuiko ya neno la Mungu; lakini wasiwasi
mkubwa wa Yesu ulikuwa kuwa hatujui jinsi ya kusikiliza na kufuata maelekezo ya
mafundisho hayo kwa sababu tunasikiliza vitu tofauti kabisa; Kama hatutakuwa
makini katika kusikiliza basi hata lile neno la Mungu litakalo fundishwa kwetu
litakuwa linagonga tu ukuta na kurudi bila faida yeyote; Tukiwa na mioyo migumu
tutambue kuwa hata neno la Mungu halitaweza kupenya katika masikio yetu kwani
tayari Moyo unakuwa umeshafunga hata Ngoma za masikio. Tukiwa na moyo wa
mashaka tunaweza kupokea neno la mungu lakini hatutaweza kabisa kuliishi
tutaanguka tu; tukiwa na Moyo uliogawanyika neno la Mungu halitakuwa na nafasi
kwani masikio yetu yatakuwa yamegawanyika katika kufuatilia vitu vingi ambavyo
havina faida; Lakini tukiwa na Moyo safi moyo imara hufungua ngoma za masikio
katika kusikiliza Neno la Mungu na neno litazaa matunda bora kwa maisha yote.
Tafakari yetu
inatuonyesha kuwa Yesu anasisitiza jinsi ambavyo tunatakiwa kusikiliza Luka
8:18 Jiangalieni
basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu
atanyang'anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho. Yatupasa kufungua
Mioyo yetu ili tuweze kusikia vyema na kulielewa na kasha kuliishi neno la
Mungu. Tukumbuke kuwa wote tumejaliwa neema ya kuwa na masikio; wote tumepewa
neema ya kuuelewa ukweli lakini kupitia masikio yetu ni dhahiri kuwa sio kila
mtu anapata huu utukufu. Sio kila mtu ananamini; anakuwa tayari kuupenda
utukufu wa Mungu; na kinachotufanya kuwa karibu au kuupokea utukufu huu ni
neema ya masikio na bahati mbaya sio kila mwenye masikio na anasikia sauti ya
Mungu; Masikio mengine ni sawa na mapambo tu katika kulisikiliza neno la Mungu.
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa tunatakiwa
kusikiliza kwa utii na utulivu; tujuwe kuwa hili ni jukumu letu la msingi
tutake tusikate tunatakiwa kusikiliza kwa unyenyekevu na utii; ili tuweze
kulielewa na kuliishi; Tunatakiwa tuwe kama mwanga tunavyosikiliza Neno la
Mungu; mwanga hufungua mengi; mwanga huweka wazi vitu vingi; mwanga huongoza;
ndivyo itupasavyo kufungua masikio yetu tusikilizapo neneo la Mungu;
tunachotakiwa kuendelea kufanya ni kuendelea kuomba neema ya Mungu ili kujenga
misingi mizuri ya kusikia na kusikiliza neno la Mungu na kuondoa vikwazo katika
kusikia neno la Mungu.
Tafakari yetu inatukumbusha kuwa imani inakuja
kutokana na kusikia. Warumi 10:13 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na
kusikia huja kwa neno la Kristo. Hata tukisoma waraka wa Yakobo 1:19. Hayo
mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si
mwepesi wa kusema; wala kukasirika;
hivyo tukijua kusikiliza kama itupasavyo tutakuwa wanyenyekevu katika maamuzi
yetu Mengi; na tutatumia busara ile ile Yesu aliitumia alivyoishi duniani. Tukiwa
wasikilizaji wazuri itatupunguzia mashaka mengi sana; na ni kweli kuwa wengi
wetu tunakuwa tayari tunamambo mengi tayari katika akili zetu kutokana na
mazingira yanayotuzunguka na hata hatutoi nafasi inayotupasa katika kusikiliza
neno la Mungu; hivyo ni wajibu wetu sasa tuanze kubadilika na kutoa nafasi ya
kutosha katika kusikiliza neno la Mungu.
Hii ni tafakari yetu ya leo Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment