June 6
ZABURI 102:6-7
Tafakari ya leo
tunaangalia tatizo nzima la kuwa pekee kwa maneno mengine tatizo la upweke;
swali la msingi ambalo tunatakiwa kujiuliza katika tafakari yetu je wewe ni
mpweke? Tunafahamu kuwa kuna aina nyingi za upweke na Upweke kwa mtazamo
mwingine ni tatizo moja kubwa sana katika jamii yetu; Lakini tukumbuke kuwa
ukiwa na Yesu huwezi kuwa mpweke kwani
yeye atakupa faraja unayohitaji; tukisoma bibilia tunajifunza kuwa Yesu
amekuwa rafiki mzuri wa wale wote ambao waliluwa wapweke ndani ya jamii tukisoma Yohana 5: 5-9 Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi
muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa
hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia
birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka
mbele yangu. Yesu
akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima,
akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.
Tafakari yetu inaonyesha kuwa kwa miaka 38 alikuwa mpweke
hana rafiki wa kumsaidie ili aweze kupona lakini Yesu alipomwona alimsaidia ili
aweze kupona. Hapa yesu ametuonyesha kuwa yeye ndiye rafiki Bora. Tunajua kuwa
upweke huleta maumivu ndani ya mwili wetu na huweza kusababisha madhara makubwa
sana. Upweke huleta woga; huleta huzuni; mara nyingi tunajaribu kutafuta faraja
kutoka kwa wenzetu ndani ya jamii yetu lakini mara chache tunaweza pata faraja
ya kweli; lakini faraja ya kweli ya upweke inapatika kutoka kwa Yesu tu; Yohana
11:11 akawaambia,
Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha. Yohana 11: 25-26 Yesu
akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.
Hivyo hata katika mauti yetu tunaye rafiki ambaye ni Yesu.
Tafakari yetu inatukumbusha kuhusu tatizo la
upweke linalotokana na dhambi; Upweke ambao ni mbaya sna ni ule unaotokana na
kuwa mbali na Mungu. Upweke ambao unaozungumzwa hapa sio ule wa kushindwa
kwenda kanisani; unaweza kuwa unakwenda kanisani na kuhudhuria ibada zote na
kuwa mtu maarufu katika kanisa lako; lakini tatizo kwa undani kabisa bado
humjui Yesu na misingi yake ya Maisha ambayo anataka wewe uishi au kuyafuata;
hebu tuyaangalie maisha ya Adam na Hawa walifanya uamuzi mbaya sana wa kumgeuka
Mungu wakati Hawa alivyofanya uamuzi mbaya sana; makosa yao na dhambi yao
tumerithiswa sisi na hatuwezi kuikwepa hukumu hiyo kama hatutaamua kumfanya
Yesu kuwa rafiki yetu mwema na Kuishi kulingana na maagizo yake;
Tafakari yetu inatukumbusha kuwa Upweke dhambi inatufanya sisi
tuendelee kuwa wapweke kwa maana inatutenga na Mungu; na hakuna kitu kibaya kwa
mtu ambaye anatamka kwa kinywa chake kuwa anamjua yesu lakini ndani ya moyo na
matendo yake anafanya matendo ambayo yanpingana na mafundisho ya Yesu; na
wakati mwingine upweke wetu unatokana na jinsi ambavyo tunatamani kupata vyote;
mguu moja ndani ya mambo ya kimungu na mguu mwingine katika mambo ya kidunia;
lakini tukumbuke mambo ya kidunia ambayo yako kinyume na mafundisho ya Mungu
hutuweka sisi katika wakati mgumu;
Tafakari yetu inatukumbusha kuhusu mama Msamalia kisimani ambaye
alikuwa mpweke alikuwa na wanaume kadhaa; lakini hakuridhika; hakuwa na amani;
hakuwa na furaha; yesu alipokwenda kisimani na kupata nafasi ya kuongea naye na
kumsamehe dhambi zake alijisikia furaha kama tunavyosoma katika Yohana 4:29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia
mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Hivyo katika maisha ya yesu
ametujengea urafiki ulio bora na wa kudumu; Tatizo letu nado tunakuwa wagumu
kutambua kuwa Yesu ni rafiki wa kweli ambaye ndiye pekee anayeweza kutuondolea
Upweke katika maisha yetu; Tukitimiza mafundisho yake kamwe hatuwezi kuwa
wapeke hivyo kuendelea kuwa au kukaa katika mazingira ya upweke ni jambo la
kujitafutia wenyewe.
Hii ndio tafakari yetu ya Leo-Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment