June 12
Ezekieli: 22:30
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa
kuiangalia upya tena wajibu wa Baba katika familia hasa katika malezi na makuzi
ya Taifa ambalo tugemeo letu ni vijana ambao lazima watokane na malezi Bora ya
familia ambayo ndio msingi wa familia bora. Tukisoma kitabu cha Ezekieli
22:30 kinatukumbusha kuwa Nami nikatafuta
mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali
palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Mungu
anaonyesha Kiongozi bora wa familia na jamii anayemtaka ambaye atasimama kati
yake na nchi; je wewe leo kama baba wa familia uko tayari kuchukua haya
majukumu?
Tafakari yetu inatuonyesha kuwa baba hodari; Baba
mwema; baba anayekubalika mbele ya Mungu, lazima awe tayari kuyabeba majukumu
kama baba; anatekeleza wajibu wake kama baba; anafikiri kama baba; anatenda
kama baba; aliyejaa upendo na msamaha; akitekeleza haya yote anapata
sifa ambazo Mungu ameziweka kwa Kiongozi wa familia; lakini bibilia
inatukumbusha kuwa Baba hodari lazima awe ni mtu mzuri, na mtu mzuri ni Yule
ambaye anafuata mafundisho na maandiko ya bibilia na kuweza kuwalea watoto
katika misingi mizuri ya kiimani. Kama Mithali 3:5 inavyotukumbusha kuwa
jukumu kubwa la Baba liwe; Mtumaini Bwana
kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia
zake zote tunawajibu kama Baba kukiri na kuomba mwongozo katika malezi ya
watoto wetu, tukumbuke kuwa hakuna kisichowezekana mbele ya Mungu wajibu wetu
ni kusimamia imani yetu.
Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa sisi kama
baba wa familia tujue kuwa kwa imani tumekombolewa, na imani ili iweze kuwa
dhabiti utiifu ni lazima; Kama baba tunatakiwa kuonyesha mfano mzuri ndani ya
familia na kwa kufanya hivyo hata malezi ya vijana wetu yatakuwa rahisi sana Waefeso
2:8-9. Sisi kama wanaume (Baba) tuna tabia ambayo tunataka daima kuwa juu na
kutoa maamuzi na wengine wote wayafuate hata bila kukaribisha ushiriki wa mawazo mengine toka ndani ya
familia. Tunatakiwa tujifunze kutoka kwa Mama zetu ambao kwa maumbile yao na
busara zao ni rahisi sana kujikabidhi kwa kila wananchokifanya katika mikono ya
Mungu. Yesu kwa kutambua ubabe wa sisi wanaume ndipo aliposema Mathayo 18:3
akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe
katika ufalme wa mbinguni. Watoto
na wanawake wana tabia ya kuamini na kutegemeana.
Tafakari yetu leo inaendelea kutukumbusha kuwa kwa wanaume kama
watatekeleza majukumu yao kwa utaratibu ambao unatakiwa Mungu atakeleza haya
kwetu: tukisoma Isaya 40:30-31 Hata
vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda
juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu,
wala hawatazimia. Hiyo ni ahadi ya Mungu
kwetu kama tunasima kwenye mstari sahihi; wakati waraka wa Paulo kwa Wafilipi
4:19 unatukumbusha kuwa ya Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa
kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Wagalatia 5:16-18
inatukumbusha kuwa Kwa sababu mwili
hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi
zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
Tafakari yetu inatukumbusha kuwa jukumu la baba ni kuleta
matumaini ndani ya familia; Kuleta upendo; amani ; umoja; heshima; uwajibikaji
wa kila mtu ndani ya familia; bibilia inatukumbusha kupitia Wakolosai 3:21 kuwa Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije
wakakata tama. Huu ni ujumbe mzuri sana ambao tunatakiwa kuuzingatia ili kuleta
matumaini ndani ya familia yetu na umoja wa familia. Ujumbe huu kutoka Wakolosai 3: 15-20 ni muhimu sana
katika siku hii ya leo Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa
katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na
likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa
zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni
mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina
la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika
Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na
uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi
wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana. Ni ujumbe ambao umetoa mwongozo mzuri sana katika
kusherekea siku hii ya leo ya Kumbukumbu ya Akina baba
Hii ndio tafakari yetu ya leo Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment