March 14
Zaburi ya 90
Tafakari ya leo
tuangalie jinsi ambavyo tunatumia muda wetu. Je tunautumiaje muda wetu na kwa
faida ya nani? Tukumbuke kuwa tunatakiwa kutumia muda wetu vizuri hasa
tunapofahamu kuwa hapa dunia tuko katika mpito wa maisha yetu; na mbele ya
Mungu hakuna dakika wala sekunde ambazo tunaweza kuzirudisha nyuma. Tukumbuke kuwa
Mbele ya Mungu kila siku inafungua ukurasa mpya tunapaswa kuwa makini jinsi
ambavyo tunatumia muda wetu. Tunaaswa kuwekeza ili tuweze kupata furaha na mafanikio
ya kweli.
Tunaishi kwa kufuata
majira kwa kujua kuwa muda ni muhimu katika maisha yetu hivyo hatutakiwi
kucheza nao. Katika mahangaiko yetu mara nyingi tunapigana sana na wakati
tukikimbizana huku na huku na pengine bila mafanikio yeyote. Lakini tunamwona
Bwana wetu yesu Kristo yeye pamoja na kuwa na kazi kubwa ya ukombozi wetu kamwe
muda haukuwa tatizo kwake; alikuwa anajua kuwa ana muda mfupi wa kutimiza kazi
ambayo alikuwa amepewa na Mwenyezi Mungu, bado alikuwa na muda wa kuwawekea mikono na kuwabariki
watoto; Muda ulikuwa rafiki kwake.
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa Mungu anaishi
katika wakati wote yeye ndiye aliyeumba muda huu ambao sisi leo hii
unatuendesha mbio. Lakini tukisoma bibilia kwa makini tutajua namna ya kuutumia
muda ili uwe rafiki na sio adui. Mwenyezi Mungu anatukumbusha kuwa tunatakiwa
kuthamini muda na kuufanya kuwa kitu muhimu sana katika misha yetu. Kila siku
ipitayo ina maana kubwa sana kwetu.
Je tunajua thamani ya
mwaka mzima katika maisha yetu? Kipimo rahisi cha kupima wakati kwa mwaka mmoja,
tunaweza kupima kwa kumuuliza mwanafunzi ambaye amefeli katika masomo yake na
ameshindwa kuendelea na shule;
je tunajua thamani
ya saa moja tumuulize mfanya biashara ambaye
ndege yake ilicheleweshwa na akakosa mkutano wa kibiashara na akaishia kupata
hasara kubwa katika biashara zake.
Je dakika moja ina
thamani gani tunaweza kujifunza kwa mtu ambaye amepata shida ya Moyo na maisha
yake yakaokolewa na wafanyakazia wa dharura;
na je sekunde ina faida
gani muulize mtu ambaye amekoswa koswa kugongana uso kwa uso na gari nyingine. Hawa
wote watakusimulia nini maana ya kujali wakati: na wangeweza kupata nafasi mpya
wangeutumia wakati vizuri sana.
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa jana ni historia,
kesho haiko mikononi mwetu; muda ambao tunao ni sasa ambao ni zawadi; muda upo
jinsi ulivyo sisi tunatakiwa tujibadilishe ili kwenda sambamba na muda huo
lakini kamwe hautungoji sisi; muda ni kitu ambachohakibadiliki;
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa pamoja na mbio zetu zote za maisha bado tuna nafasi nzuri ya
kuweza kuratibu Muda wetu; kama nafasi ya kwanza tutampa Mungu na nafasi ya
pili kwa ajili ya familia zetu; tukikumbuka kuwa kila dakika ni zawadi kutoka
kwa Mungu hivyo tunapasa kuitumia vizuri. Hivyo wajibu wetu sio kuhangaika
Kuutawala muda bali tunatakiwa kujitawala wenyewe na kuutumia muda vizuri. Kama
waefeso 5:14 -15 Hivyo husema, Amka wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na
Krsito atakuangaza. Basi angalieni sana jinsi mnavyoenda; si kama watu wasio na
hekima bali kama watu wenye hekima. Tunatakiwa kutembea kama watu wenye hekima
sio wapumbafu.
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa kama hatutaweza kutumia vizuri muda wako hivyo mtu mwingine
atakusaidia kuutumia muda wako vizuri. Muda ambao tumepata uko sawa kwa wote
hivyo hakuna mtu ambaye amepata muda mwingi zaidi. Bibilia kupitia Luka 12:34
kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapo kuwapo na mioyo yenu.
Tujikumbushe hadithi
ya Mariamu na Martha: Mariamu aliyeketi miguuni pake yesu,
akasililiza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi;
akamwendea, akasema Bwana huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike
peke yangu? Mwambie anisaidie. Bwana akamjibu akamwambia Martha, Martha,
unasumbuka na Kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi. Lakini kinatakiwa kitu kimoja
tu: Mariamu amelichagua fungu lililo jema ambalo hataondolewa.
Yesu anatufundisha hapa
kuwa Imani na kazi ni vitu vinavyo tegemeana na vyote ni muhimu kwa ukuaji wetu
wa mwili na kiroho. Lakini tunatakiwa kutumia muda wetu mwingi katika katika
kutafuta ufalme wa Mbinguni; ndilo fungu ambalo Mariamu alichagua; hili ni
fungu sahihi kwetu sote. Bibilia inatufundisha kuwa matumizi yetu ya muda na
maisha yanakwenda sambamba. Tunatakiwa kuwa makini na matumizi ya Wakati ili
ulete faida ya kweli mwisho wa maisha haya tunayoishi.
Tafakari ya leo
inatukumbusha Wakati huu tulio nao ndio haswa wakati wa kumtumikia Mungu. Kama 2
Wakorinto 6:2 kwa maana anasema, wakati uliokubalika nalikusikia, siku ya
wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndio sasa tazama siku ya wokovu
ndiyo sasa. Tukumbuke kuwa Mungu ametupa sisi wakati mzuri wa kumjua Yesu kama
mwokozi wetu na kupitia yeye tufurahie maisha ya mbinguni lakini tunatakiwa kutumia
wakati wetu vizuri.
Nahitimisha tafakari
yetu ya leo kwa kutoa ushauri kuwa wakati ni huu wa kumtumikia Mungu;
tukiangalia hivi sasa jinsi migongano mingi inavyoikabili dunia; tukumbuke mafundisho
ya ya bibilia kuwa, mwisho wa dunia utakavyokaribia kutakua na vita, tetesi za
vita, kusalaitiana; mauaji; majeshi kuasi; tauni na balaa la njaa kila mahali; tunatakiwa
kutumia muda wetu vizuri tusije chelewa kama
Mithali 1:28 inavyosema ndipo watakaponiita, lakini sitaitika;
watanitafuta kwa bidii wasinione. Leo ndio siku yetu wa wakovu kwani Mwenyezi
Mungu yuko tayari kusikia sauti yetu na kilio chetu. Wakati ni huu wa
kumrudia na kumtumikia Mungu wetu.
Hii ndio Tafakari yetu ya leo Amina.
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment