March 11
MATHAYO 16:19
Tafakari Ya leo inalenga
kuonyesha jinsi ambavyo sisi wana wa Adamu tumekabidhiwa funguo za uzima wa
milele. Ni zawadi ya pekee sana kwetu kuaminiwa na kukabidhiwa funguo hizi
ambazo ni muhimu sana katika safari yetu ya kuelekea kwenye maisha yetu ya
baadae; funguo unakupa uwezo, nguvu ya kuingia sehemu ambayo imefungwa au
kufunga ili mtu mwingine mwenye nia mbaya asiweze ingia katika nyumba hiyo.
Isaya 22:22 anasema kuwa Na ufunguo wa Nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake;
yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana
atakayefungua.
Tafakari ya leo
inatuonyesha kuwa funguo ni Nguvu, ni mamlaka, ni upako kwa sisi wakristo
inawakilisha ni nguvu au uwezo ambao Mungu anatujalia sisi binadamu, na
inapatikana kwa kila mtu aliyeelewa umuhimu na kuwa tayari kuzitumia funguo hizo kwa maisha ya Mbinguni.
Mwenjili Mathayo anaweka wazi tukisoma Mathayo 16:19 Nami nitakupa wewe funguo
za ufalme wa Mbinguni; na lolote utakalo lifunga duniani; litakuwa limefungwa
mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.
Kwa ujumbe huu tumepewa kibali cha kufanya maamuzi.
Yesu alitoa kibali hiki
kwa Peter, kibali ambacho Peter aliwapa
mitume na wafuasi wote na hivyo hivyo kibali hicho kimeruhusiwa kwa wakristo
wote ambao wako tayari kutumia nguvu na mamlaka ya funguo na ambao wako tayari
kuzitumia. Hata tukisoma Injili ya John 20: 21-23 Amani iwe kwenu; kama Baba
alivyonituma mimi, mimi name nawapeleka ninyi. Naye akisha kusema hayo
akawavuvia, akawaambia pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi,
wameondolewa; na wowote mtakaofungia dhambi wamefungiwa. Wow kweli tumepewa
nguvu za ajabu lakini hatujui jinsi ya kuzitumia.
Tafakari ya leo
tunavyoendelea na mfungo wa siku arobaini kuelekea siku ya ufufuo ambayo ndio
siku maalumu ya mwokozi wetu alipounyesha ulimwengu kuwa yeye ni mbarikiwa wa
baba tuna kila sababu ya kusifu na kushangilia. Huku tukijitathimini wenyewe jinsi
ambavyo tunanashindwa kuzitumia vizuri funguo za uzima ambazo tumepewa. Yesu
aliliona tatizo hili tukisoma Luka 11:52 Ole wenu ninyi wanasheria kwa kuwa
mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia
mmewazuia.
Yesu anawaonya wanasheria
walikuwa wanatumia vibaya neema na maarifa ya funguo kwa kuto wafundisha watu
wengine jinsi ya kutumia funguo za mbinguni ili waweze kufurahi neema ya maisha
ya baadae hivyo wao wamekalia neema hiyo kwa faida yao pekee. Mathayo 13: 52
Akawambia, kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni
amefanana na mtu mwenye nyumba na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake
vitu vipya na vya kale.
Funguo ambazo tumepewa
zina nguvu sana ambazo zinaweza kufungua hazina na kutoa humo vitu vya thamani
kubwa katika maisha ya Kiroho; katika imani funguo ambazo tumepewa ni za
kufungua nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu juu ya maisha yetu.
Tafakari ya leo
inatuonyesha nini faidia ya kuweza kupata elimu ya kutumia funguo za mbinguni? Funguo
ambazo tumezipata tunaweza kuzieleza matumizi yake kama ifuatavyo: Unaweza
kuziweka pembeni uzizitumie; unaweza
kuzibeba katika mifuko yako hivyo wakati unapotaka kuzitumia unakuwa na kazi ya
kuzitafuta; na unaweza zivaa shingoni na ukapata urahisi wa kuzitumia.
Tatizo la kuzivaa funguo hizo shingoni
ni ushahidi kuwa kila mtu ataziona na shetani atakuwa anakushawishi uzivue au
uweke mahali ambapo hapaonekani mbele ya Macho ya dunia. Kama wakristo
tunatakiwa tuone fahari ya kuzivaa na kuzitumia bila woga wowote. Je unaona
aibu kusoma bibilia mbele ya yatu? Au kumtangaza Kristo mbele ya watu? Tukumbuke
kuwa pale tunapovaa funguo zetu shingoni kunatupa sisi ujasili wa khali ya juu
kuwa wewe ni mfuasi mwaminifu wa Kristo. Na uko tayari kumpigania wakati wote.
Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa tuna
kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumtoa mwanae yesu kristo ambaye
alitufundisha kuhusu funguo za uzima wa milele, na Baraka zitokanazo na funguo
hizo na ametusistiza kuwa lazima tuwe watu wa kuomba msamaha na kusamehe ili
tuweze kuzitumia vyema funguo hizi .
Hii nitafakari yetu ya leo Amen
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment