February 8
Tafakari ya leo tangalie
kuwa dhana ya kusubiri majira ya mungu
imekuwa ni jambo gumu kwetu wanadamu;
zaburi ya 27:14 umngoje Bwana, uwe hodari, upige moyo konde naam umngoje
Bwana; Isaya 40:31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu
kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, walahawatachoka; watakwenda kwa miguu wala
hawatazimia.
Kusubiri wakati wa Bwana ni
kila kitu katika maisha yetu kwani tunaendelea
kuliweka tumaini letu mikononi mwa Mungu; sisi binadamu majira yetu tumeyafunga
zaidi katika kuupenda ulimwengu huu. Leo dunia yetu na majira yetu yametawaliwa
sana na dhana ya umimi na hakuna dhana ya subira; Tumesahau kuwa subira ni fadhila na kamwe hatutaki kusubiri.
Matatizo mengi tunayoyashuhudia leo msingi mkubwa ni kushindwa kusubiri. Binadamu
leo tumetawaliwa na msemo huu 'Nipatieni mimi haraka au sahau kuhusu hilo!
Majira au wakati ni dhana
ambayo inatembea na haisubiri hivyo yatupasa kutumia sana busara kuikabili ili
mwisho wake tuweze kuona faida; mfano tu binadamu tunapitia majira makubwa matatu,
kuzaliwa ; kipindi cha mpito cha kuishi na hatimaye kifo; hivyo kwa sentensi
moja ninaweza sema Majira ni ni kila
kitu katika maisha yetu. Lakini tunatakiwa tukumbuke kuwa Mungu ndiye kila kitu
katika majira yetu kama Isaya 55:8-9
anavyosema maana mawazo yangu si mawazo yenu wala njia zenu sio njia zangu, zi
juu sana kuliko njia na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua
ishukavyo, na theluji kutoka mbinguni wala hairudi huko bali huinywesha ardhi
na kuizalisha na kuchipuza ikampa mtu apandaye mbegu na mtu alaye chakula;
Tafakari yetu leo
inatuonyesha jinsi Majira yanavyoweza kukuletea
furaha, chuki, mafanikio,utajiri na kumpenda Mungu; tukimwangalia mkulima
anahitaji kujua wakati gani wa kupanda
mazao yake na wakati gani atatakiwa kuvuna. Hii inamsadia kufanya maandalizi
yanayofaa kwa ajili ya mbegu na matayarisho ya shamba na hata matayarisho ya
ghala la kuhifadhia mazo pindi akimaliza kuvuna.
Mwekezaji anahitaji kujua
wakati gani akitaka kununua kahawa itakuwa tayari kwa manunuzi; hii itamsaidia kujiandaa kuwa na fedha ambazo
atakuwa anahitaji kwa manunuzi ya kiasi kila ambacho anahitaji, kuandaa namna
ambayo atakuwa akisafirisha mazao aliyonunua; na wapi atauza mazao yake na
itamchukua muda gani kuweza kuuza mazao yake.
Tafakari ya leo inatukumbusha
kuwa tupende tusipende hatuwezi kushindana na wakati; hata kuongea kwetu kwa
afya njema yatupasa tuzingatie majira/wakati kuna wakati wa kuongea na wakati
wa kukaa kimya;
Je tunampa Mungu wakati
mzuri wa kutafakari zawadi ya maisha ambayo tunayo; Mungu ametupa uwezo wa
kuweza kutawala majira yetu kwa namna tupendavyo. Tukumbuke kuwa ile tuweze
kuutumia wakati wetu vizuri bado tunahitaji masaada wa Mungu.
Najua wakati mwingine
tunapata wakati mgumu wa kuelewa ugumu wa majira hasa pale ambapo mategemeo
yetu na matokeo yetu yanakuwa tofauti.
Kwani wakati unasonga mbele bila kuwa na mafanikio ambayo tulikuwa
tunayafikiria utayapata. Kalalamika, kukasirika, kugombana au hata kuuana kamwe
hakutasimamsiha wakati bali kutaendelea kuleta wakati mgumu zaidi. Kama
binadamu tunaishia tu kusema Ninge…… ninge… lakini huwezi simamisha wakati hata
kwa sekunde moja tu. Sisi binadamu mara nyingi tumekuwa ni watu wa kujisahau na
kujua kuwa tunaouweza wa kuuchezea na kubadilisha wakati/majira ili uweze
kwenda sambamba na matakwa yetu ya maisha.
Ni mungu peke yake
anayeweza kusimamisha majira au wakati; tukiangalia ukuu wa mungu wa milele
tunaona kuwa wakati au majira yote yako mikononi mwake nay eye anaweza kupanga
vile ambavyo anataka iwe; hata pale
ambapo sisi hatuelewi yeye tayari ameshakuwa na mipango yake endelevu juu
yake. Hata majira mazuri ambayo
tunayafurahia tayari yamepata kibali cha Mungu. Mungu anapanga majira yote kulingana na kalenda yake na sio
kalenda yetu. Majira ya mungu hayana mfano ni mazuri na yanaleta Baraka kwa
watu wake.
Tukisoma litabu cha warumi
8.28 tunakumbushwa kuwa katika mambo
yote Mungu hufanya kazi kwa manufaa ya wale wanaompenda, walioitwa kwa kusudi
lake. Mungu amefanya kila kitu kizuri kwa wakati
Mungu ameumba vitu vyote
kwa wakati wake kwa faida yetu japo tumeshindwa kutimiza maelekezo yake,
tukakimbilia zaidi anasa na dunia na mambo ambayo sisi tunafikiri ya maana
kumbe sio ya maana kabisa, tukaacha kufanya mambo yenye faida kubwa kwetu
tukifikiri kuwa wakati utaendelea kutusubiri. Tukasahau kuwa haya mambo ya
dunia yanakuja na kupotea na kamwe hatutaridhika wala hatutosheka kabisa. Majira na wakati ulio nao unatakiwa
kutupa sisi hamu ya kuonja maisha bora ya mbinguni.
Ni sawa kama unakwenda
kwenye sherehe mategemo ambayo wengi
tunayo ni kupata chakula kizuri na kingi ambacho kitatosheleza haja ya mwili
wako ukizingatia wakati wako ambao umetumia;
cha ajabu kama ukifika hapo na wakawa wanatoa tu chakula kidogo na
chepesi ni wazi kuwa utakasisirika kuwa umepoteza wakati wako; lakini kumbe
tatizo hawakusema kuwa hicho ni kisafisha kinywa, na wakatangaza baadae kuwa
tusubiri mlo kamili unakuja, utaridhika na kufurahi hata kama utasuburi kwa muda mrefu hutajali
kuhusu muda unaopoteza kwani haja ya
moyo wako itakuwa imekamilika.
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa kwa vyovyote vile tunavyofikiria kuhusu majira kamwe
hatuwezi kubadilisha mipango ya mungu; yeye ndiye aliyeweka mchana na usiku,
yeye ndiye aliyeweka siku, yeye ndiye aliyeweka masika na kiangazi: kama mzaburi
31.15 anavyosema nyakati zangu zimo mikononi mwako,Uniponye na adui zangu, nao
wanaonifuatia. Kitabu cha Maombolezo
3.25 Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, kwa hiyo nafsi imtafutayo. Kwa maneno
mengine majira ya Mungu ni ya uhakika kwa mafanikio yetu.
Tafakari ya leo
inatukumbusha jambo moja kubwa Sisi binadamu tunapaswa kushukuru mungu siku zote na kwa wakati wote; japo
hatuwezi kuelewa mipango ya Mungu juu yetu bado tuna wajibu wa kuendelea
kumshukuru mungu wakati wote; Mungu ana makusudi yake juu yetu kuhusu utendaji
wake kwetu kwa wakati wake na sio kwa wakti wetu. Mungu anajua nini tunahitaji
na kwa wakati gani. Kwa hiyo Majira au Wakati wa Mungu hauna mbadala.
Tafakari ya leo
inatukumbusha kuwa maisha yetu yamejaa SUBIRI; Japo ni kitu ambacho hatukitaki
lakini ukweli utabaki kuwa ukweli KUSUBIRI ni sehemu ya maisha yetu; kwani wengi
wetu ni afadhali kufanya kitu chochote kuliko kusubiri. Baadhi yetu ni afadhali
kufanya kitu kibaya kuliko kusubiri.
Ukweli lazima usemwe;
Msingi mkubwa wa maisha ni kusubiri.
Tunausubiri ili tuweze kumwona daktari. Tunasubiri ili tuweze kumaliza shule na
kuhitimu. Tunasubili ili tuweze kupata nafasi ya kukubalika na Kuingia katika chuo. Tunasubiri kwa ajili ya kuanza kazi kwa mara ya kwanza.
Tunasubiri kuona kama benki itaweza kutoa mkopo. Tunasubiri kwa Bwana kuleta
mume au Mke bora ndani ya maisha yetu. Tunasubiri Kwa mwenyezi Mungu kujibu
sala zetu.
Je, umewahi
kujiuliza kwa nini Mungu hasemi nasi kwa uwazi zaidi? Inawezekana ni kwa sababu
wewe unakwenda kwa mwendo kasi na hivyo
huwezi kusikia sauti yake? tunatakiwa tutafakari vipaumbele vyetu,
kupunguza mwendo kasi wetu na kuangalia
upya ratiba yetu, kwa kufanya hivyo tutaweza sisi kupata nafasi ya kusikiliza
sauti ya Mungu.
Hii ni tafakari yetu ya leo Amina
No comments:
Post a Comment