April 13
2 Petro 2:19
Tafakari ya leo tuangalie
kwa namna gani ukosekano wa uadilifu na uwajibikaji husababisha watu
kutokutekeleza majukumu yao ya kiroho katika namna ambayo inampendeza Mungu;Tatizo
kubwa tulilonalo kama Taifa ni ufinyu wa viongozi bora na utashi binafsi wa
wachache walio katika nyanja za uongozi kwa kukosa sifa muhimu kwa viongozi.
Kwani inatupasa kutambua kuwa uongozi si lelemama, ni kipaji na ni kazi ngumu.
Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana, kwamba
waongozi watatekeleza dhamana na wajibu wao kwa makubaliano na
maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na
maadili fulani yanayoitambulisha na kuiongoza jamii husika.
Tafakari yetu inalenga kumwonyesha kiongozi muadilifu jukumu
lake ni kufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi
vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na
Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye magomvi na
hasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na
uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na
mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi
Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima
pamoja na ukuaji wa kiroho, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na
tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya
muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila
hatua anayochukua. Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni kukubali
kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja.
Tafakari yetu inasisitiza kuwa kikwazo kukubwa sana cha uadilifu na
uwajibikaji ni matumizi mabaya ya ofisi kwa masilahi ambayo hayagusi maisha ya
wananchi, rushwa na matumizi mabaya ya pesa ni miongoni mwa malalamiko makubwa
katika hoja hii. Rushwa ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili dunia nzima kwa
ujumla.
Kipimo kimoja
kikubwa cha uongozi bora ni uwezo wa kusimamia rasilimali za wananchi,
uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na kumcha Mungu; kiongozi akiwa na vitu hivi
huzaa hekima ua uwajibikaji wa kweli na uzalendo wa kupenda nchi yako na
kusimamia rasilimali zake kwa faida ya Taifa.
Tafakari yetu
ya leo inatuonyesha kuwa baadhi ya viongozi
wetu kutumia nguvu zao sio kuondoa
umasikini bali kuongeza umasikini kwa mtanzania wa kawaida. Hivyo hata kumletea
maisha yake ya Kiroho kuyumba na kuingia katika vitendo ambavyo havimpendezi
Mungu. Ni wajibu wa viongozi wetu kuhakikisha kuwa wanatekeleza wajibu wao kwa
misingi ya haki na sheria wakikumbuka kuwa hata wao wamechaguliwa na Mungu ili
kutimiza adhima ya Mungu Dunia.
Hii ndio
tafakari yetu ya leo;
Emmanuel
Turuka
No comments:
Post a Comment