April 26
Tafakari ya leo tujipime kama mwili wako ni bustani ya kweli ya Mungu? Tukumbuke kuwa Adam na Hawa baada ya kuumbwa walikabidhiwa bustani ya Aden ambayo ilikuwa na kila kitu.
Mungu aliwaambia kufurahi kila kitu katika bustani ile na walikuwa na mamlaka ya vitu vyote ambavyo vilikuwa katika bustani ile.
Tafakari yetu inatukumbusha jinsi Mungu alivyowaambia vyote tumieni lakini mti huu msiuguse. Hivyo hivyo Mungu anaongea nasi leo akitoa maelekezo kuwa : mwili wako ni bustani Takatifu niliyokukabidhi yafurahie maisha na vitu vyote ambavyo viko ndani ya mwili wako na hatutakiwi kuvunja amri za Mungu ambazo ni mwongozo wa maisha yetu bora.
Tafakari yetu inaonya kuwa pamoja na Yesu kutufia msalabani lakini bado tunatakiwa kutumia mwili wetu ambao ni bustani ya Mungu kwa hekima kubwa. Kama tutavunja amri za Mungu nasi tutakuwa kama Adam na Hawa tutalaaniwa na kuondolewa katika bustani ya uzima wa milele.
Tafakari yetu leo inatupa mwamko Mpya kuwa tunatakiwa kuitunza bustani hii ya ajabu ambayo Mwenyezi Mungu ametutunukia kwa kuimwagilia, kuitilia mbolea, na kuifyeka vizuri kila siku kwa kusali bila kuchoka.
Mungu wetu ni mwingi wa huruma, amejaa upendo na anataka kuona kuwa bustani ambayo ametukabidhi ikiwa inastawi; lakini haiwezi kustawi bila msaada wake na utayari wetu wa kufuata amri zake. Hivyo ni wajibu wetu kuendelea kuomba na kushukuru wakati wote wa uhai wetu.
Hii ndio tafakari yetu ya leo. Amina
Emmanuel Turuka
No comments:
Post a Comment