WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Thursday, April 7, 2016

ROHO YANGU INA WAJIBU GANI

April

Tafakari ya leo tuangalie umuhimu wa roho katika kumtukuza Mungu. Ni wajibu wa Roho, kumsifu, kumwimbia na kumtumaini Mungu kwa sababu ya Matendo yake makuu.

Wednesday, April 6, 2016

FAIDA YA UVUMILIVU KATIKA MAISHA YETU YA KIROHO NA KATIKA JUMUIA ZETU


APRIL 6

Wafilipi 2:4-8

Kwa haraka haraka tu Uvumilivu ni uwezo wa, au ni mazoezi ya, kutambua na kuheshimu imani au matendo ya wengine; uvumilivu uko katika kila nyanya ya maisha yetu, kuanzia maisha yetu ya kila siku; TATIZO katika maisha ya kawaida sana, swala la uvumilivu halizungumzwi sana, tunachokiona sana ni mazungumzo ya kulipa kisasi;Nafikiri itakuwa jambo njema kama tutaendelea kufundisha na kuhubiri uvumilivu katika nyanya zote. Pengine fujo hizi ambazo taifa linaendelea kujionea zikizidi kujitokeza zingeweza kukoma au kupungua

Hii inatokana na kukosekana mambo makubwa matatu ambayo ni ufahamu au maarifa, hekima na  hasa uvumilivu. Kiongozi asiye mvumilivu anaweza kujikuta anatumia mabavu kutawala ili watu wajue kuwa yupo, ana nguvu na ana mamlaka. Na hii falfasa ambayo huangukia kwa wananchi vile vile pale ambapo wanakuwa hawana uvumilivu; Bibilia inatuonyesha mfano mzuri wa bwana wetu yesu ambaye pamoja na ukuu wake alijishua na kuvumilia yote na kuwatumikia wote bila makuu: wafilipi 2:4-8 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;  bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;  tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 

Tafakari yetu leo inatufundisha kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa  kiongozi anatakiwa kuwa, mtulivu, mvumilivu na anayetumia zaidi hekima kuliko mabavu, kiongozi anatakiwa Kuwa na  msimamo wa uvumilivu ni moja ya kazi ngumu zaidi miongoni mwa viongozi dhidi ya wananchi katika jamii. Ni ukweli ambao haufichiki kuwa viongozi hawakuzaliwa wakiwa wavumilivu, lakini lazima tujifunze kuwa wavumilivu. Na hii ni kweli hata kwa jamii inatupasa kuvumiliana na kumaliza tofauti zetu kwa busara ya majadiliano.

Tafakari yeru tunaangalia hata katika siasa uvumilivu wa kisiasa unakuza  utamaduni wa utawala bora na ukomavu wa demokrasia; na Kwa demokrasia kufanya kazi vizuri, wananchi lazima kuwa tayari kuvumilia na kuvumiliana. Tukumbuke kuwa dhana ya uvumilivu ni ya msingi sana kwa maendeleo kwani inaruhusu mawazo mapya ndani ya jamii; kupitia dhana hii ya uvumilivu, kiongozi anakuwa  tayari kukubali  na kuheshimu  maoni na mawazo ya watu wengine na haki zao kwa uwazi na uhuru. Katika hali hii,uvumilivu huruhusu kuwepo kwa vyombo  huru vya habari kutumika kama chombo muhimu kuwahabarisha wananchi na kuwasilisha madai yao kwa viongozi wao.

Tukumbuke kuwa demokrasia inahitaji vyombo vya habari ambavyo hugeuka kuwa daraja la mawazo kati ya viongozi na waongozwa. Vyombo huru vya habari husaidia   wananchi kuelewa taratibu ambazo zinaimarisha demokrasia.uvumilivu wa viongozi huru utasaidia kueneza demokrasia  na uwajibikaji kwani wananchi wataweza kukosoa serikali na ujumbe kufikishwa serikalini bila kuogopa.

Tafakari yetu leo inatuonyesha ukweli kuwa Falsafa ya Uvumilivu hufunza na kuwakumbusha viongozi na wananchi wake kuwa wanatakiwa kuishi kulingana na fikira njema. Mwenye kuifuata falsafa ya uvumilivu hayuko tayari kuamsha fikra mbaya za uvunjajiwa amani bali daima atajitaidi kuziepusha kwa kuendeleza uamuzi  wa uwazi na kwa kutumia njia  ya utulivu wa hekima kupitia uzoefu makini wa kimantiki: Kiongozi mwenye uvumilivu daima hutafakari, na kuziweka fikira mahali pamoja kabla ya kufanya uamauzi.Msingi wa kimaadili wa falsafa ya uvumilivu  kama mtaalam mmoja alivyo wahi kusema kuwa kwa ufupi tunaweza kusema kuwa uvumilivu umesheheni nini?

Tafakari yetu inalenga kurunzi kwa sisi wananchi wa Tanzania bado tuna kila sababu ya kuendelea kuenzi na kuthamini uvumilivu miongoni mwetu; uvumilivu kati ya wananchi wa dini tofauti, kusikilizana na kushauriana kwa faida ya taifa letu; tukiweza kuutumia uvumilivu katika kiwango cha juu tutafanikiwa kuondoa chuki ambayo inaanza kueneakatika taifa letu; Ni kweli kama tutaweza kuwaweka wenzetu mbele katika maisha yetu ya kila siku na kuwa tayari kushirikiana nao tutakuwa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza injili hii ya uvumilivu.

Hii ndio tafakari yetu ya Leo; Amina

Emmanuel Turuka



Tuesday, April 5, 2016

KICHEKO BORA KIMEJAA IMANI - FURAHA YAKE NI YA MILELE




April 5

Mwanzo 18:9 -15

Tafakari ya leo tuangalie jinsi imani inavyotuwezesha kutuletea kicheko; na kicheko cha imani ni kicheko chenye ushindi mkubwa sana; kwani kinakuwa kimejaa matumaini ya Mungu yaliyojaa ukamilifu wa ahadi yake kwako; ni kicheko ambacho kitadumu katika maisha yako yote; Tukisoma Hadithi ya Abraham alivyotembelewa na wageni watatu kitabu cha Mwanzo 18:9 -14 Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani.  Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake.  Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.  Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?  Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee?  Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.  Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka. 

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa pamoja na kicheko cha matumaini lakini Sara aliguna na kuwa na mashaka juu ya uwezo wake wa kuzaa akiangalia ukuu wa umri wake akiwa amesahau kuwa ahadi yiho ilikuwa imetolewa na Mungu katika umbo la kibinadamu kama wageni ambao walitembelea nyumba yao. Sara bado anatuwakilisha sisi binadamu pamoja na  furaha kubwa ya imani ambayo mungu huwa tayari ametuandalia ili tuweze kuifurahia bado hatuwezi kucheka au kuifurahia bila kuwa na mashaka katika mioyo yetu. Abraham na Sara walipata bahati ya kuwa Mungu alikula nao chakula pamoja nao na kutoa hiyo ahadi nzuri kwa Sara. Tukumbuke kuwa habari njema wakati mwingine hatuzipokei katika ukamilifu wake.

Katika maisha yetu tunapopata habari nzuri ambazo tunatakiwa tuzipokea kwa furaha kwa imani yetu sisi tunakuwa mbali na Mungu na kuanza kuwaza kibinadamu zaidi nakuona kuwa hili haliwezekani; Ndio haliwezekani katika upeo na maono yetu bali kwa Mungu hakuna linaloshindikana; Tunatakiwa tubadilike na tubadili uelewa na jinsi ambavyo tunavyoamini vitu; Tuweke imani yetu mbele na daima tutacheka kicheko cha ushindi na Bwana. Tukisoma Warumi 4:17 mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Luka 1:37 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. 

Tafakari yetu pili inatuonyesha kuwa Sara pamoja na kuwa na mashaka na maelekezo ya Mungu vile vile alicheka na akijua kuwa hataweza onekana mbele ya macho ya watu; Lakini Mungu aliyaona matendo yake na alimuuliza kwani ulicheaka Sara? Naye kwa woga akajibu sikucheka; Mungu alisisitiza tena kuwa ulichena na kuonyesha wasiwasi moyoni mwako; fundisho kubwa hapa hatuwezi kuficha matendo yetu au mawazo yetu mbele ya uso wa Mungu. Tunatakiwa daima kukiri udhaifu wetu na kufanya toba ya kweli. Ndio maana Mtoto aliyezaliwa aliitwa Isaka maana yake “ Utacheka”

Ni kweli ukiwa na imani utacheka na bwana; katika mwaka mmoja tu Abraham na Sara walipata motto na wote pamoja walicheka na kumshukuru Mungu baada ya miaka mingi ya Sara kuwa Mgumba Bwana ameshusha Baraka zake kwake na kwa familia yake; Tukiwa na imani ya kweli tunaamini katika maono ya kimungu  na tunaondokana na wasiwasi wa kibinadamu; tunaondokana na mashaka ambayo mwisho wake yanatuangamiza. Hata katika shida zetu tunatakiwa tumtumaini Mungu na tucheke na Mungu katika imani ikiwa ni ishara ya ushindi ya shida zetu; tukumbuke kuwa vicheko na furaha daima vinatuonyesha ni Mungu gani ambaye sisi tunamwabudu kwani mungu wetu ni wa upendo; hapendi watu ambao wamejaa mashaka na ukiwa na mashaka wasiwasi huwezi kuwa na furaha. Ndio maana hata Injili ya Bwana wetu Yesu kristo inajulikana ni habari njema kwa watu wote; ni habbari inayoleta matumaini ya kweli; imeleta furaha ya kweli; imeleta wokovu wa kweli na faraja ya kweli kwetu sote.

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa tunaweza kuwa na shaka kama Sara kufuatia umri wake mkubwa kuweza kupata motto lakini alijua kosa lake na alikiri na Mungu akamsamehe na kasha alipata motto katika kipindi kile kile ambacho aliambiwa ili furaha yake ikamilike. Imani yake ndiyo iliyompa furaha ya kudumu. Najua sasa hivi mimi na wewe tunamashaka makubwa sana kuhusu shida zetu na tunalia na shida zetu, tunafadhaika na shida zetu, tumesahau kuwa tukiwa na imani dhabiti na tukiamini katika nguvu ya msalaba kamwe hatutakiwi kulia tunatakiwa kucheka kama Sara.

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa kwanza tunatakiwa kutafakari jinsi Mungu alivyotupenda na kutufikisha hapa tulipo leo; tukiweza kulitafakari hili vizuri hatuna haja ya kuwa na mashaka wakati sauti ya Mungu ikiongea nasi tunatakiwa kuamini na hivyo kufurahi kwa ushindi wa kushinda matatizo yetu; Daima vicheko vyetu vinatakiwa view vya ushindi kwa sababu ya Imani yetu katika uwezo wa Mungu juu yetu; Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake; Sara alicheka sana kwa furaha ya Imani baada ya Kumzaa Isaka motto wa ahadi ya Imani; najua Mungu anatufanikisha sana katika masha yetu lakini tulio wengi hatuko kama Sara hatutubu na kumshukuru Mungu na tunajawa na mashaka katika Imani yetu. Hivyo tunakumbushwa leo kuwa ni wakati mzuri wa kutafakari mapito yetu ili vicheko vyetu view vya Imani na vitakavyo dumu milele yote kama tutasikia sauti ya Mungu na kuitii bila mashaka yeyote. Amen

Hii ni tafakari yetu ya Leo


Emmanuel Turuka

Monday, April 4, 2016

MAFUNDISHO YA BIBILIA JUU YA SERIKALI ZENYE RUSHWA NA UFISADI – KIINI CHAKE NI NINI?



Wafilipi 2: 4

APRIL 4

Tafakari yetu ya leo  tujiulize kuwa je kuna serikali yeyote ya kidunia ambayo inaweza kuwa madarakani bila kuwa na kutumikia rushwa na ufisadi? Tukumbuke kuwa mwisho wa siku watumishi wa serikali bado ni raia wa nchi husika na zao la taifa husika; Je kwa mantiki hii viongozi ambao wanaunda serikali wanaweza kuepukana na vitendo vya rushwa na ufisadi? Je unakubaliana nami kuwa serikali za kidunia zimejaa rushwa na ufisadi ambao ni ubatili mtupu? Je tunaweza kuwa na serikali ambayo haina tabia hizi katika dunia hii? Bibilia inatukumbusha kuwa  serikali ambayo haitakuwa na harufu ya rushwa lazima itoke nje ya serilaki za kibinadamu;

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa serikali za kidunia ambazo hatimaye zinatawaliwa kwa rushwa na ufisadi, zinasaidiwa kuingia madarakani na raia ambao wanakuwa na malengo tofauti kwa masilahi yao binafsi; wengine wakijua wazi kuwa endapo serikali hiyo itaingia madarakani basi haja zao za kukwepa ushuru, au kuendesha biashara yao bila kufuata masilahi mapana ya nchi yatafanikiwa; hivyo na serikali itatengeneza mianya ya wao kuendelea kujinufaisha na kuwaacha wananchi wanyonge masikini katika umasikini wao kwani nguvu nyingi zitaelekezwa kwao. Tumeona sehemu kubwa za tawala hizi watu ambao ni waaminifu ndio wanaoumia zaidi.

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa ili tuweze kuangamiza rushwa na ufisadi lazima nguvu za kutokomeza zianzie kwa viongozi wa juu ambao wamepewa mamlaka juu ya nchi na Mwenyezi Mungu. Serikali yeyote ile ambayo itakuwa tayari kupambana na rushwa na ufisadi ujue kuwa itapoteza umaarufu wake; katika hili bibilia tukisoma Mhuburi 7:20 bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.

Tafakari yetu bado inatuongoza kuwa  tukiondoa wanadamu ambao sio wakamilifu; Yesu Kristo ambaye Mungu alimchagua kutawala ufalme wake, hakuweza kushawishika katika yale ambayo yalikuwa sio sahihi kutenda;  Yesu alionyesha hili pale alipokataa rushwa  kubwa ambazo alipewa na shetani juu ya kukabidhiwa utawala wote wa kinunia na fahari zake kwa kuambiwa kumsujudia shetani Mathayo 4: 8-10  kisha ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha miliki zote za ulimwengu na fahari yake; akamwambia haya yote nitakupa , ukianguka kunisujudia; Ndipo Yesu akamwambia Nenda zako shetani, kwa maana uimeandikwa msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Katika shida na mateso yote bado Yesu aliendelea kudumisha msimamo wake ulio sahihi wa kumtumikia Mungu bila kushawishiwa na mtu mwingine yeyote kwa ukombozi wetu sisi.

Ni ukweli mtupu kuwa nchi nyingi zinafanya uchaguzi ambao nadharia inaruhusu watu kuwachagua viongozi ambao wataingia ofisini/madarakani kwa ajili ya kuendesha nchi; lakini ukiangalia chaguzi nyingi na taratibu za chaguzi hizo hizo ambazo tunaona kampeni zake  nanatawaliwa kwa rushwa kwa kiasi kikubwa sana, hivyo wale wenye uwezo ndio wanaowaingiza watawala madarakani; hapa nafikiri utakubaliana na mimi vyama vya siasa ndivyo vinavyoongoza kwa matendo makubwa sana ya rushwa katika kuhakisha kuwa viongozi tukona vyama vyao ndio wanakuwa washindi ili waweze kuongoza serikali, hivyo watafanya kila hila ili waweze kushinda.

Tafakari yetu ya leo inawaasa viongozi wetu kuwa ili kuweza kuepukana na tabia zote za rushwa na kifisadi; lazima watekeleze amri kuu ya upendo ambayo ni amri ya dhahabu; kile ambacho wewe unataka ufanyiwe mfanyie mwenzako hivyo hivyo; Mathayo 7:12 Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu; nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hili kwa viongozi wetu wengi ambao ndio tegemeo la kuondoa umasikini wa watu wao wameshindwa kutekeleza hili; wao wanapenda kutendewa vizuri na kundi dogo la watu waliowaingiza madarakani na kunufaishana wao kwa wao; wameshindwa kabisa kutekeleza hii Golden Rule.

Kwa msingi huu rushwa na ufisadi unaimarishwa zaidi na choyo ya mali na ubinafsi wa kujilimbikizia mali; hapa tunaona kuwa viongozi wako tayari kupokea rushwa mfano kutoka kwa makandarasi, nao makandarasi wanapata nafasi ya mwanya wa rushwa katika kutumia vifaa ambavyo havina ubora unaotakiwa ili waweze kujilipa na kupata faida kubwa; kwa msingi huu rushwa na ufisadi utaweza tu kwisha kama tutaondoka na dhana ya ubinafsi na choyo ya kujitajirisha; kama Waefeso 4:23 inavyotufundisha na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu: tunatakiwa kuvua uongo na tunatakiwa kusema kweli daima ili tuweze kuvaa utu mpya ulioumbwa katika mungu ili kutekeleza wajibu wetu ipasavyo na kuwa na hofu ya Mungu. Na ujumbe huu kutoka katika waraka wa Paulo kwa Wafilipi 2:4  ni muhimu sana ambapo anatufundishwa kuwa Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe bali kila mtu aangalie mambo yaw engine.

Tatizo la tawala za kiduani hata kama wakati mwinginwe wanaweza patiwa elimu nzuri ya kupambana na rushwa na ufisadi bado viongozi wetu wanapenda kushiriki katika vitendo vya rushwa. Kwa msingi huu ni vigumu kwa serikali zetu kupambana na rushwa; tukumbuke mafundisho ya bibilia kuwa watu wenye uchu wa mali, na waongo hawataingia mbinguni; mara nyingi viongozi wala rushwa wana hizi tabia mbili ya Uchoyo wa mali na uongo wanapowadanganya watu wake ili kuhalalisha uovu wao na kikundi kidogo kilicho waingiza madarakani kwa masilahi yao;

Hii ndio tafakari yetu ya leo Amina

Emmanuel Turuka
Corrupt Government


Sunday, April 3, 2016

DAMU YA KRISTO MSALABANI INATUFUNDISHA TUSIWE WATU WA VISASI: - BALI WATU WA MSAMAHA


April 3

Waefeso 4:32

Tafakari ya leo inatukumbusha kuwa kwa hakika mwanandamu anahitaji upeo mkubwa wa nuru ya kiroho ambayo itaweza kumfanya azike tamaa zake na hisia zote za kulipiza kisasi; tunatakiwa kuwa na uwezo wa kujizuia na hasira, kuzikandamiza hasira, chuki kwa moyo mpana na kujenga daraja la msamaha.  Kusamehe mtu ambaye amekukosea, kuwapenda ndugu na jamaa ambao wameukata uhusiano pamoja nawe, na kuwa mkarimu kwa yule ambaye aliwahi kukunyima, kukutukana, kukusababishia hasira,kukudharau, kukudhalilisha na kadhalika sio jambo rahisi. Tumewaona hata watumishi wa Mungu ambao wanaielewa sana bibilia wakishindwa kabisa kuktekeleza kanuni hii. Kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyofanya pale msalabani, aliwasamehe wote waliompiga, mdhihaki, hata yule jambazi ambaye alisulubiwa pamoja naye alimsamehe dhambi zake na alimkaribisha katika utukufu wa mbinguni.

Kumsamehe yule aliyekutendea yasiyo sahihi hutusaidia kutupatanisha na Muumba wetu; vile vile msamaha hudumisha mshikamano wa udugu ambao umeharibiwa. Kwa kusamehe tunaandaa njia ya kumwendea Mungu; Lakini  pasipo  imani  haiwezekani  (Waebrania 11:6). Inatufundisha kuwa mtu  amwendeaye Mungu  lazima  aamini  kwamba  yeye  yuko,  na  kwamba  huwapa  thawabu wale wamtafutao,”. Msamaha hutujengea wa kumwendea na Kuishi na Mungu katika Imani.

Kama ilivyoandikwa hakuna mwenye haki, hata mmoja” (Warumi 3:10). Mungu yuko tayari na anasubiri kumsamehe mtu anaye omba msamaha imeelezwa katika Zaburi 86:5 "Kama wewe Bwana u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao". Daudi aliweka wapi tumaini lake la msamaha? Tukisoma Zaburi 51:1 "Ee Mungu unirehemu sawasawa na fadhili zako kiasi cha wingi wa rehema zako uyafute makosa yangu. Mathayo 6:14-15 Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao na Baba wenu wa mbinguni atawasamehe ninyi bali msipowasamehe watu makosa yao wala Baba yenu hatawasamehe makosa yenu." Wale wamesamehewa husamehe. imeandikwa Waefeso 4:32 "Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma ninyi mkasameheane kama na Mungu katika kristo alivyowasamehe ninyi."

Kusamehe kwa kweli hakuhesabu makosa. imeandikwa Mathayo 18:21-22 "Kisha petero akamwendea akamwambia Bwana ndugu yangu anikose mara ngapi nami ni msamehe? hata mara saba? Yesu akamwambia sikwambii mara saba bali hata saba mara sabini." Katika kusamehe Yesu ametukomboa kutoka kwa dhambi na mshahara wa dhambi. Wakolosai 2:13-14 inatueleza kuwa "Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu aliwafanya hai pamoja naye akisha kutusamehe makosa yote akisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake iliyo kuwa na uwadui kwetu akiondoa isiwepo tena akaigongomea msalabani."
Zaburi 51:7-12 "Unisamehe nami nitakuwa safi, unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko dheluji unifanye kusikia furaha na shangwe, mifupa ilio ponda ifurahi. usitiri uso wako usitazame dhambi zangu uzifute hatia zangu zote Ee Mungu uniumbie moyo safi uifanye upya roho iliyo tulia ndani yangu usinitenge na uso wako wala roho wako mtakatifu usiniondolee unirudishie furaha ya wakovu wako unitegemeze kwa roho ya wepesi."
Zaburi 32:1-6 "Heri aliyesamehewa dhambi na kusitiriwa makosa yake heri Bwana asiyemhesabia upotovu, ambaye rohoni mwake hamna hila niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa kwa kuugua kwangu mchana kutwa na kwa maana mchana na usiku mkono wako ulinilemea jasho langu likakauka hata nikawa kama nchi kavu wakati wa kaskazi nalikujulisha dhambi yangu wala sikuuficha upotovu wangu nalisema nitayari maasi yangu kwa Bwana naweukanisamehe uoptovu wa dhambi yangu kwa hiyo kila mtu mtauwa akuombe wakati unapopatikana hakika maji makuu yafurikapo hayatamfikia yeye."
Wale walio wanyonge moyo wako mbele ya Mungu na wala kutambua hatia yangu, haijafika hali ya kwanza ya kukubalika. Tunahitaji kuokolewa kutoka katika aina zote za tabia zetu mbaya pamoja na misukumo ya ndani inayotushurutisha kufanya mambo fulani mabaya: kama vile, kusema uongo, hasira inayomfanya mtu atukane watu, tamaa mbaya za mwili, uchungu, kutaja machache tu.
Tafakari yetu leo inatuonya kuwa hatuwezi kujiokoa wenyewe kutoka katika dhambi au kuigeuza tabia yetu kwa kujitegemea wenyewe kama vile Simba asivyoweza kuamua awe mwana-kondoo (Warumi 7:18). Dhambi ina nguvu nyingi kuliko nia yetu ya kufanya yale tuyatakayo. Lakini Kristo anaweza kukufanya wewe uwe "imara kwa uweza wake, kwa kazi ya Roho wake katika utu [wako] wa ndani" (Waefeso 3:16). Anafanya kazi yake ili kuondoa tabia zetu ziletazo uharibifu na mahali pake kuweka tabia hizi nzuri: upendo, amani, furaha, upole, uwezo wa kujitawala (Wagalatia 5:22,23). Kristo anaishi maisha yake kupitia ndani yetu, kisha tunapokea uponyaji wa kiroho, tunarejeshwa katika maisha mapya, na kuwezeshwa kuishi maisha hayo mapya.
Hakuna dhambi ambayo ni ya kutisha sana asiyoweza kuisameka Yesu anatamani sana kwamba kila mmoja wetu hatimayeawe na uhusiano mzuri na Yule aliyemkosea na kumsababishia majeraha ambayo yamejenga chuki ambayo inahitaji msamaha. Yesu anataka tupokea msamaha na utakaso wa Mungu ni; katika  imani jambo ni  rahisi na la maana sana kama tunavyofurahia kumpokea motto mdogo aliyezaliwa na kumkumbatia. Lakini kutokana na ubinadamu wetu, majivuno, kiburi, masengenyo inatuwia vigumu sana kutoa msamaha wa kweli pale tunapokosewa, tunakuwa na kiburi ambacho kinatufanya kuona kuwa Yule aliyetukosea hastaili msamaha wetu; lakini kama tunayafuata mafundisho ya yesu na mifano ambayo ametutolea katika Bibilia Takatitifu tunatakiwa tuondoe ugumu katika mioyo yetu na kuuvaa unyenyekevu kama yeye alivyovaa unyenyekevu na kuuvua Umungu kwa ajili ya makosa yetu, na alikuja kukaa nasi na ametutengenezea daraja la msamaha ambalo kila mwanadamu lazima alipite ili kuweza kukamilisha safari yake ya kwenda mbingu.
Hebu jitafakari kwa nini umekuwa na kiburi cha kushindwa kabisa kumsamehe, jirani yako, ndugu yako ambao wamekukosea kutokana na ubinadamu wao, usijali amekukosea mara ngapi angalia je wewe uko tayari kumsamehe wakati wowote ule? Lakini kama umefunikwa ndani ya damu ya Yesu yote yanawezekana kabisa. kwani Damu yake ndio ondoleo la dhambi zetu zote na faraja ya kweli wa maisha yetu bora. Lazima tutekeleze zana ya msamaha.
Hii ndio tafakari yetu ya leo Amina

Emmanuel Turuka




Saturday, April 2, 2016

NJONI KWANGU NIWATUE MIZIGO YENU

April 2

Tafakari ya leo bado tunaendelea kumshuruku Yesu kwa kufa msalabani kwa ajili yetu na uokovu wetu.
Tuna kila sababu za kusema asante kwa upendo huu wa khali ya juu kwetu.





Friday, April 1, 2016

NI WAJIBU WETU KUWAPENDA WAKE ZETU



April 1
Ephesians 5:23-27
Tafakari ya leo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutujalia kuwa na familia bora na imara kwa kutajalia mke mwema. Bibilia kupitia Mithali 19: 14 Mke mwema hutoka kwa BWANA; Kwa fundisho hili la bibilia inatukumbusha  kuwa Mungu pekee ndiye mwasisi wa ndoa ni; tukumbuke alivyomwambaia Adam na Hawa  zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Kwa maelekezo ya Mungu katika uumbaji wake tunakubaliana kuwa mwanaume na mwanamke ni nguzo mbili za msingi wa familia, lakini kwa kuwa wanaume wamepewa sifa maalum kwa amri ya uumbaji, na kwa sababu ya uwezo wao wa mantiki ni imara zaidi ya ule wa wanawake, wao huchukuliwa kama walezi wa familia zao na vichwa vya familia. tukisoma 1 Wakorintho 11:3 Lakini napenda muelewe kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, kama vile mume alivyo kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo. Waefeso 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mke kama vile Kristo alivyo kichwa cha kanisa, ambalo ni mwili wake, naye mwe nyewe ni Mwokozi wa kanisa. Ikumbukwe huyu ndiye ana uamuzi wa mwisho katika familia akiamua kuukana ukristo, kurudi nyuma inakuwa na athari kubwa sana katika familia. Hivyo hii ndio nguzo ya ndoa ya Kikristo.

Tafakari yetu ya leo msisitizo wetu uko katika wajibu wa wanaume kwa wake zetu; Ni mwanaume ambaye kwa kutumia busara yake, anaweza kuisadia familia yake na kutayarisha mazingira kwa ajili ya furaha yao, na ni yeye ambaye anayeweza kuigeuza nyumba kuwa Pepo na mke wake kuwa kama Malaika. Busara ya mwananume ni tuzo kubwa katika malezi ya familia;Mwanaume ambaye anaisaidia familia yake, lazima atambue kwamba mwanamke pia ni binadamu kama mwanaume. Siri ya ustawi wa familia inategemea na jinsi mtu anavyomtunza mke wake, na hii ni kama ilivyowajibu wa mke kwa mume wake ambao unaeleweka kuwa katika kiwango sawa na Jihadi, pia unatambua kama tendo jema na lenye thamani sana. Lakini mwanaume ajifunze namna ya kumshughulisha mke wake, katika namna ambayo atageuka kuwa na tabia kama Malaika.

Leo tunakumbushwa kuwa mwanaume lazima atafiti kuhusu tabia na matakwa ya mke wake. Lazima apange maisha yake kufuatana na matakwa ya mke wake na mahitaji sahihi. Mwanaume anaweza kwa tabia na msimamo wake kumshawishi mke wake katika njia ile ambayo inampendeza yeye (mke wake), kwake yeye mume na nyumba yake. Kama tunavyokumbushwa kutoka katika waraka wa Waefeso 5:33 Hata hivyo kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake. Upendo ni nguzo ya Pili na pia ni moja ya tunda la Roho katika ndoa.

Tafakari yetu inawauliza wanaume kama wanajua kuwa mwanamke amejaa wema na ni kiumbe chenye hisia kubwa sana ya upendo na utunzaji wa nyumba? Tunatakiwa tukumbuke kuwa furaha yake hutegemea huruma na upendo wa mume wake. Tukiwapenda wake zetu kwa upendo halisi ndivyo wanavyofurahi zaidi. Kwa hiyo siri ya mwanamume aliyefuzu katika maisha ya furaha ya ndoa ni jinsi anavyo onesha mapenzi kwa mke wake. 1 Wakorintho 13:4-8 Upendo huvumilia, upendo hufadhili; upendo hauna wivu au majivuno. Hili ndilo jukumu letu katika kuwapenda wake zetu na hatuwezi kulikwepa jukumu hili muhimu ili kukamilisha familia iliyo bora. Tukumbuke kuwa tusipokuwa mwema kwa wake zetu, basi anaweza kupoteza mvuto kwenye nyumba zetu, halikadhalika na watoto pia. Na zaidi ya yote kwako wewe mwenyewe. Wakati wote nyumba zetu zitakuwa katika hali machafuko. Mwanamke hubadilika haraka na hatakuwa tayari kufanya juhudi kwa ajili ya mtu asiyempenda.

Tafakari ya leo inatushauri akina baba kutumia mazuri yaliyo jaa sifa na hisia kwa wake zetu tukumbuke kuwa  maneno mazuri na matamu ya kuwasifia wake zetu kamwe hayaondoki kamwe hayaondoki moyoni mwao. Kama mambo yalivyo, mapenzi na huba lazima yawe halisi na kuvutia kwenye moyo wa mwingine, lakini hata kupenda sana kwa mtu haitoshi, kwa kuwa ni muhimu kuonesha huba. Kwa kuonesha hisia zako kwa maneno na vitendo vyako, mapenzi unayoonesha, yatapata jibu zuri kutoka kwa mkeo na nyoyo zenu zitaimarisha muungano wa mapenzi. Uwe wazi na udhihirishe mapenzi yako kwako bila kusita. Wakati yupo au hayupo, msifie. Mwandikie barua unapokuwa safarini na mtaarifu kwamba kutokuwa karibu naye unajihisi mpweke sana. Mara kwa mara mnunulie kitu kama zawadi. Mpigie simu unapokuwa ofisini au shughuli zako na umuulize hali yake. Wake zetu wanafurahi tunapowapa heshima iliyojaa upendo Heshima humfanya mtu ajione unamjali, wanaume wengine atasema anapenda lakini anamwita mwenzie hajasoma, ametoka familia duni, hafanani na hali yangu, kwakweli huku ni kumdhalilisha mwenzio 1 Petro 3: 7 – 9 7Kadhalika ninyi waume, ishini na wake zenu kwa kuwahurumia, mkitambua ya kuwa wao ni dhaifu na hivyo muwape heshima, kwa maana ninyi ni warithi pamoja nao wa neema ya uzima.
Tafakari yetu ni msingi mkubwa sana wa familia bora, jamii bora ni matokeo ya familia bora itokanayo na usimamizi mzuri wa Mume; Marko 10:7 Na kwa sababu hii mume atamwacha baba yake na mama yake na hao wawili, watakuwa mwili mmoja. Hivyo nyumba yenu itakuwa msingi wa maisha bora; ijae msamaha tukumbuke kuwa hapana mtu yeyote hapa duniani ambaye anazo sifa zote na hana makosa. Kwa ufupi, hakuna mtu ambaye hana mapungufu, na hakuna mtu yeyote hapa duniani anayeweza kuchukuliwa kama kiumbe kilichokamilika. Kwa kawaida, wanaume, kabla ya kuoa hudhani kwamba atakaye muoa awe hana dosari yoyote. Hawajali ukweli huu kwamba hakuna kiumbe kifananacho na malaika hapa ulimwenguni. Wanaume hawa, mara waoapo huwaona wake zao waliodhani wakamilifu, si wakamilifu na hivyo huanza kuonesha mapungufu yao. Hudiriki kuona kuwa ndoa zao hazikufuzu na wao wenyewe kuwa na ‘bahati mbaya.’

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa tuishi katika msamaha wa kweli tusamehe na kusahau, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatimiza  maandiko 1 Wakorintho 13:4-8 5 Upendo hauna kiburi na haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti kujipendeza nafsi; haukasiriki upesi, hauweki orodha ya mabaya. Bali tutajenga nyumba iliyo bora lakini msingi wote wa Nyumba bora Amepewa mwanaume kuusimamia na kuufanikisha. Wanaume tunajukumu kubwa na la msingi mkubwa san asana.

Hii ndio tafakari yetu ya leo – Amina

Emmanuel Turuka