Kwaresma
ni kipindi ambacho tunakumbuka maisha ya Mwokozi wetu Yesu kristo na kazi yake
ya ukombozi wa maisha yetu katika safari ya maisha yetu baada ya maisha ya hapa
duniani. Kwa maneno mengine Kwaresma ni kipindi maalum ambacho wakristo
Wanatakiwa
wayaelekeze maisha yao zaidi katika sala, kufunga na kuwasaidia wale ambao
wanahitaji masaada. Ni kipindi zaidi cha kutafakari
na kufanya toba na kumrudia Mungu.
Kipindi cha Kwaresma kinajumuisha siku arobaini za toba na
shukurani kwa Mungu. Tukisoma katika maandiko matakatifu tunaweza kuona
jinsi watumishi wa Mungu manabii ambao Mungu
aliwapa majukumu mazito baada ya kufunga na kusali kwa siku 40; Walitakiwa kutubu
kabla ya maombi au ahadi ambazo Mwenyezi Mungu aliwaandaa kuzipokea kwa faida
ya watu wao. Musa alifunga siku 40 kabla ya kupokea amri kumi za Mungu “Naye alikuwa
huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala
hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao hayo maneno ya maagano, hizo
amri kumi.” (Kutoka 34:28). Nabii Eliya alifunga siku 40 kabla ya kuonana na
Mungu kwenye mlima Orebu: “Akainuka, akala akanywa, akaenda katika nguvu za
chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu mlima wa
Mungu.(I Wafalme 19:8)
Kipindi cha kwaresma siku 40 kwa mfuasi mtiifu wa kristo lazima
atapambana na mitihani mingi; kwa vile shetani naye anakuwa kazini kupinga mema
ambayo unataka kufanya lazima utakutana chaweza taabu, wasiwasi, uzuzu, woga,
kukosa msimamo au mwelekeo.
Tukumbuke maisha ya Yesu kabla ajeanza utume wake Katika Agano jipya,
Yesu alifunga siku 40 (jangwani) akipambana na majaribu kabla ya kuanza kazi
yake. Alijaribiwa na shetani mara tatu; lakini aliyashinda majaribu ya shetani;
Tukumbuke kuwa Kufunga
ni jambo linalomsaidia mtu kutafakari kuhusu mambo ya kiroho na kumkumbusha
kwamba kuna mambo muhimu maishani kuliko mali na chakula. Funga inatusaidia
sana sisi kujenga uhusiano mzuri pamoja na Mungu. Na kubwa zaidi funga
inatusaidia sana sisi tuaminio katika
kutimiza ahadi ya kumshukuru Mungu na kuonyesha kwamba mtu amejitoa kwake.
Ninafunga kwa sababu ninampenda Mungu.
Yesu alitoa taadhari ambayo sisi tunapotekeleza Kwaresima hii ya mwaka
2017 tujiepushe kujiona kuwa sisi ni bora zaidi; mimi ni mwadilifu zaidi kuliko
mwenzangu; Tuondoe dhana ya kuhukumu; hii ni sawa na kujisifia mwenyewe wakati
hujui mwenzako pia amefanya nini ambacho kimempendeza Mungu. Tumkumbuke Yule farisayo
mwenye kiburi aliyejiona kuwa
bora kuliko wengine kwa sababu alifunga kwa ukawaida, unaonyesha wazi kwamba
Mungu anakataa mtazamo kama huo. Yesu anatukumbusha kuwa tendo la kufunga ni
tendo jema lakini ni tendo linalohusisha nafsi yako na Mungu na hupaswi
kuwaambia wengine kwamba umefunga.
Wote wakitambua hali yao ya dhambi mbele ya Mwenyezi
Mungu hutumia wakati huo katika kutubu, kuungama na kukiri makosa yao mbele ya
Mwenyezi Mungu. Toba hiyo hufanyika kwa njia mbalimbali. Licha ya kufanya hiyo
toba, pia wanashauriwa kusali zaidi wakati huo wa toba. Tunavyofahamu sala ni
mahusiano ya karibu sana ya binadamu na Muumba wake. Hapo hutoa sala za
kushukuru, sala za kuabudu, sala za kumsifu Mwenyezi Mungu, sala za kumtukuza,
sala za kuomba msamaha kwa dhambi mbalimbali tulizomkosea Mwenyezi Mungu na pia
zile ambazo tumewakosea binadamu wenzetu.
Maisha yetu sisi kama binadamu maisha yetu
yamejaa matendo maovu; hivyo kipindi cha kwaresima ni wakati mzuri wa kujipatanisha na Mungu kwani kwa kutenda
dhambi sisi tunajifarakanisha na Muumbawetu, na hivyo tuhitaji upatanisho. Siyo
hayo tu, pia huyo binadamu huwa amejitenga na binadamu wenzake anayeishi na
kushirikiana naye. Kwa hiyo jambo la tatu analopaswa kulifanya mtu yule mwenye
kufanya toba ni kufanya matendo mema, yaani kutoa sadaka kwa ajili ya maskini
na wale ambao ni wanyonge katika jamii yetu.
Ni matumaini yetu kuwa Mfungo huu wa Kwaresima
utakuwa ni wenye manufaa kabisa kwa Waumini wenyewe binafsi, lakini pia kwa
ndugu na marafiki wote. Tukumbuke kuwa hasira ya Mungu itatulizwa tu ikiwa
waumini tunafunga na kujinyima mambo mbalimbali. Tukiwa na imani tunasadiki
kuwa kwa mfungo huo wa waumini wakristo utasaidia kabisa kwa kutuletea neema.
Jambo jingine ambalo Waumini Wakristo
wanapaswa kulizingatia ni kwamba imewapasawa kutoa sadaka zao kwa moyo wa
ukarimu. Wakati huu wa Mfungo ni wakati hasa wa kutenda matendo mema na kuacha
uchoyo na ubinafsi. Waumini wanapaswa kuwa wema zaidi, na kuwa wakarimu zaidi.
Hivyo ndivyo inavyowapasa wale wote ambao wameamua kufunga na kumrudia Mwenyezi
Mungu.
Tukumbuke kuwa Kweresma inatupasa itubadilishe
kuwa waumini bora kabisa sisi tu kwa siku 40 bali kwa amsiah yetu yote mpaka
tunakufa mfungo, utusaidie kutubadilisha kabisa kutoka ndani ya mioyo yao.
Tunaweza kusema kuwa lengo la Mfungo ni kumbadilisha binadamu, ni kufanya
mageuzi ya ndani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Mfungo mtukufu ni
kipindi cha kubadilika kutoka ndani na kuwa binadamu aliye mwema na mkarimu
zaidi. tunanatakiwa kuonyesha upendo wao kwa maskini.Basi tunaomba kwa njia hii
ya Mfungo mtukufu waumini wazidi kujipatanisha na Muumba wao, na pia wajenge
mahusiano mema na ndugu zao wanaoishi nao. Kwaresima ni mabadiliko, Kwaresima
ni mageuzi, Kwaresima ni kuwa na upendo zaidi wenye ukarimu zaidi. Kwaresima ni
kuahidi kuacha mabaya na kuzingatia mema na hivyo Kwaresima ni kuwa watu wapya
waliojaa huruma na upendo kwa Mungu na jirani.
Nawatakieni kwaresma njema ya mwaka 2017
Emmanuel Turuka
Kalamazoo Michigan
No comments:
Post a Comment