WELCOME - KARIBUNI SANA

GOD’S PROMISES ARE NEW EVERY MORNING” LAMENTATION 3;23

“All our dreams can come true – if we have the courage to pursue them.” - Walt Disney


Saturday, May 7, 2016

YATUPASA KUSHUKURU KWA KILA JAMBO

May 7


Tafakari ya leo dhana kubwa kama tulivyofundishwa katika injili mara kwa mara yatupasa kushukuru kwa kila jambo. Hii ndio tafakari yetu ya leo;

Friday, May 6, 2016

ASANTE SANA MAMA

May 6 

Tafakari ya leo tunapokaribia kusherekea siku ya kuwakumbuka mama zetu ambao wametufikisha hapa tulipo tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mungu.Upendo wa mama ni wa ajabu ambao haulinganishwi na kitu chochote kile; hata ukimkasirisha vipi atakasirika na baada ya Muda tu atasamehe na kusahau na kurudisha upendo wake wote kwako. Je kwa nini tusiseme asante sana Mama na sina chochote cha kukulipa zaidi ya kukuombea tu kwa mungu ili neema zake ambazo hazina mipaka zizidi kutawala maisha yako amina. 

Thursday, May 5, 2016

NAKUTEGEMEA MUNGU WANGU

MAY 5



Tafakari yetu leo inalenga na kusisitiza kuwa pamoja na uelewa wetu ambao ni kazi ya mikono ya Mungu wetu bado tegemeo letu liko juu yake; yeye pekee yake anaweza kusimamisha Jua na kila kitu kwa neno lake tu; Hivyo tusijifanye kuwa sisi hatumtegemei mungu.

Wednesday, May 4, 2016

WAACHENI WATOTO WADOGO WAJE KWANGU



May 4

Mathayo 18: 3-4

Tafkari yetu leo tunaangalia jinsi Yesu alivyotuagiza kuwa tukiwa kama motto mdogo ni rahisi sana kuingia katika ufalme wa Mungu; Je Kwa nini yesu anataka sisi tuwe na fikra na akili za motto mdogo katika kuridhi ufalme wa mbinguni? Watoto wadogo mara zote ni wategemezi wa wazazi wao kwa kila kitu; ni wasikivu, na pale wanapokosea wataumia watalia lakini mwishoni hujinyenyekeza na kuomba msamaha, hawana kiburi, hawafikirii madaraka , wala mali na kila kitu mbele yao wanachokipata wanashukuru na kufurahia; hupenda kujifunza na hata wakikosolewa hucheka na kujaribu tena;
Tafakari yetu leo wazo kubwa ni ugumu wa sisi kama watu wazima ambao tayari tumeshakuwa na akili zetu zimeshakuwa na tunakuwa na ugumu wa kujinyenyekeza mbele ya mungu tukitambua kuwa sisi tunaweza kujitegemea sisi wenyewe na hatuhitaji msada wa Mungu; Yesu hapa anatukumbusha kuwa ili ukuu war oho unahitaji unyenyekevu ambao watoto wanao na sisi watu wazima tunapingana nao; tukumbuke kuwa unyenyekevu ni hatua ya kiroho ya kukua na sio hatua ya kujidumaza;  Yesu anatufundisha kuwa lazima tubadilike kama tunataka kuingia katika ufalme wa mbinguni; Lazima tutubu makosa yetu kwa moyo na kuweka kusudio la kuacha kutenda dhambi au kuendelea kutenda dhambi. Lazima tabia zetu kuhusu dhambi ziwe za kupinga dhambi.

Tafakari yetu  tukisoma 1 Wakoritho 14: 20 inatukumbusha kuwa Ndugu zangu, msiwe watoto katika akili zenu; lakini katika uovu mgeuzwe watoto wachanga, bali katika akili zenu mkawe watu wazima. Akili ya watotohawafikirii mabaya; ma hawafikirii kutendewa mabaya humpenda kila mtu, humwamini kila mtu, humfurahia kila mtu wamwonaye; hivyo sisi kama wakristo tunatakiwa kubadilika kuwa wema, kuishi katika maadili mema, kutenda mema, na tukifanya hivyo thawabu yetu itakuwa kubwa mbele ya Mungu; ndio hata tukisoma kutoka Injili ya Yohana 3:3-5 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.  Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?  Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kwa kuzaliwa kwa mara nyingine ni kuwa tayari kubadilika na kuuvaa unyenyekevu ambao ni msaada mkubwa katika matendo yetu katika kukamilisha safari yetu ya Mbinguni;

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa Mtoto hana hadhi yeyote ndani ya familia au jamii; kwa vile huonekana kuwa ni tegemezi basin a hana nafasi ya kufanya maamuzi yeyote; Hili ni tatizo kubwa kwetu kwani tunapenda kuheshimiwa, kunyenyekewa, hata wakati mwingine kuabudiwa; tunatakiwa tuwe watu ambao sio kitu katika ulimwengu huu bali tukijua kuwa Mungu ndio tegemeo letu na ngao na kinga yetu; Kama vile watoto wanavyowategemea wazazi wao kwa kila kitu nasi ni wakati wetu wa kumtegemea Mungu kwa kila kitu. 

Hii ndio tafakari yetu ya leo Amina

Emmanuel Turuka









Tuesday, May 3, 2016

JE WEWE NI MKE WA LUTU?



May 3

Mwanzo 19:26

Tafakari ya leo tunatafakari maisha yetu hapa dunia kwa kuangalia zaidi lengo letu kubwa na hatima ya maisha yetu tunaielekeza wapi? Yesu kupitia injili ya  Luka 17: 28-29 Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;  lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Bwana wetu Yesu Kristo alituonya kuwa Mke wa Lutu alikuwa Baridi, hajali, hana utii sio tu kwa mumeo hata kwa Mungu ndio sababu hukumu ya mungu alishuka juu yake; Kama uilivyokuwa kwa Adam na Hawa ndivyo ilivyokuwa na Mke wa Lutu; Aliambiwa asigeuke nyuma na akageuka nguzo ya Chumvi kwa kupenda kuishi katika ulimwengu wa dunia na sio ulimwengu wa Kimungu.

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa tulio wengi leo hii ni kama Mke wa Lutu, hatusikii sauti ya Mungu na maelekezo yake, na kama tunaisikia basi hatuko tayari kufuata haya maelekezo yake na tunaishia kuwa Nguzo ya chumvi ambazo zinatemebea na hazina huhai wa kimungu. Mathayo 24:12 inatukumbusha kuwa  na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa; Kama ilivyokuwa kwa mke wa Lutu kuwa pamoja na kuishi na mume ambaye alikuwa akimwogopa na kufanya kazi na Mungu kwa imani kubwa na Mungu Kuwapa zawadi ya Kuishi zaidi pale alipoamua kuwasha moto wa kibiriti na kuiingamiza Sodoma, Mke wake alishindwa kutembea katika Mwendo huu wa imani na kumwogopa Mungu.

Tafakari yetu inatukumbusha kuwa wakati huu Sodoma ilikuwa imejaa uchafu wa kila aina; hivyo mke wa Lutu sio tu alihamia Sodoma bali Sodoma ilihamia ndani ya Nafsi yake; alikuwa mwanamke ambaye alipenda na kuabudu anasa ambazo zilikuwa zikifanyika Sodoma; Ndio maana hakuweza kusikia sauti ya Mungu ambayo ilikuwa ikimwokoa katika maangamizi alijawa na kiburi cha anasa na hivyo alishindwa kutekeleza agizo la Mungu. Hivyo tatizo kubwa ni nini hapa? Mke wa Lutu aliupenda zaidi ulimwengu kuliko kumpenda zaidi Mungu;

Kama ilivyo kwa mke wa Lutu hata sisi leo tumesongwa sana na anasa za dunia hata ile damu ya yesu ambayo imetukomboa hatuipi thamani kwani matendo yetu hayafanani na thamani ya Damu hiyo. Hata hatufanyi majukumu yetu vile inavyotakiwa; hatuna nafasi ya kuwalea watoto wetu katika maadili ya kimungu; muda wetu mwingi tunapotezea katika maisha ya anasa za dunia hii; sauti ya Mungu daima inatuambia kuwa “Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea”. Lakini hatusikii sauti hiyo na tunaendelea na maisha yetu ya anasa za duniii hii. 

Tafakari yetu leo inaendelea kutukumbusha kuwa tuache dhambi ya kiburi ambayo ndio msingi wa dhambi nyingine zote; Tuwe wanyenyekevu tusikie sauti ya bwana na kutekeleza maagizo yake; tukumbuke kuwa utii ni sadaka ya juu sana, Yesu alituagiza kama tunampenda tutazishika amri zake; kutotii ni dhambi mbaya sana; Mungu anafurahishwa na utii wetu kwake na amri, mafundisho yake kwetu sisi kupitia Mwokozi wetu yesu kristo. Tunakumbushwa kuwa tusiwe kama Mke wa Lutu aliyeangalia nyuma kwa kufikiri kuwa dunia hii ndio zaidi kwetu kuliko Mungu. Tunatakiwa kuacha dhambi ya kiburi na kutekeleza utii kwa Mungu katika kuishi maisha yetu kama yeye anavyotaka sisi tuishi;

Tafakari yetu inatutadharisha na matendo yetu ya kuangalia Nyuma; Tumeagizwa tuangalie mbele ili tuweze kufuzu kuingia katika nyumba ya Mungu; lakini kwa kuangalia nyuma kama mke wa Lutu tunakuwa tumejiondoa wenyewe katika kushiriki utukufu wa Mungu; tukisoma Luka 9: 61-62 Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu. Hatutakiwi kabisa kuangalia nyuma tunapoutafuta ufalme wa Mungu; Kuangalia nyuma hapa maana yake ni nini? Tunayaangalia maisha yale ya zamani, ya ulevi, uzinzi, uwongo, wizi, chuki, na kadhalika; tukumbuke kuwa hakuna maisha ya baadae bila mipango hiyo kupokea maelekezo ya Mungu ndani ya Nyoyo zetu. Agizo ambalo tunapata leo hatutakiw kugeuka nyuma na kuyarudia maisha yaliyojaa dhambi. Tumepata Baraka ya kukombolewa na damu ya Yesu jukumu letu sasa ni kusonga mbele na kamwe kuto geuka Nyuma.

Hii ndio tafakari yetu ya leo;

Emmanuel Turuka


 

TAZAMA ILIVYO NJEMA NDUGU WAKIKAA KATIKA UPENDO


May 2

1Peter 3:8

Tafakari ya leo inatukumbusha kuhusu umuhimu wa wa kuishi pamoja kwa upendo na maelewano; kama waraka wa 1 Petro 3:8 unavosema Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu;  kama Waraka wa Waefeso 4: 2-8 unavyoyukumbusha kuwa sote lazima tuishi kwa upendo na kuwa wamoja tukizingatia kuishi katika unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.  Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.  Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.  Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. 

Tafakari yetu vile vile inasisitiza kuwa  bibilia inatukumbusha kuwa tunatakiwa kuishi kwa kupendana pamoja kama waraka wa Warumi 12: 15- 18 Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.  Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.  Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Tukumbuke kuwa pale penye amani na upendo furaha ya bwana utawala na watu wanakua katika neema ya Mungu na maarafa ya mungu; umoja wa kweli huzaliwa miongoni mwetu. Lakini pale ambapo pana chuki amani hutoweka neema ya Mungu na maarifa yake hutoweka pia; woga hutawala, uwazi hupotea shetani natawala na kuleta maangamizo ambayo mwisho wake humwangamiza mwanadamu na kumfanya kujenga kiburi na majivuno.

Tafakari ya leo neno la msingi katika kuishi kwa upendo na wezetu linatawalia na neno heshima; tukiweza kuwaheshimu wezetu na kuwapa haki wanayostahili upendo utatawala maisha yetu, na hakuna kiburi wala chuki kitapata nafasi katika maisha yetu; mwenyezi Mungu anatamani sana sisi tuwe tofauti katika dhana nzima ya kuishi pamoja kwa kupendana; Mungu anataka sisi tuwe chanzo cha Baraka kwa wenzetu; tuwe watu ambao hatutamani wenzetu wapate shida au tabu; na pale wanapofanikiwa tusiwe watu wa kwanza kuwaonea wivu na kuwachukia. Bali tushangilie pamoja katika mafanikio yao na tulie pamoja na kuwapa nguvu katika shida zao.

Tafakari yetu leo inatukumbusha kuwa ili tuweze kufanikiwa lazima tukubali na kujikataa wenyewe; tusiwe watu ambao tunajijali wenyewe na kuona vitu bora vyote ni vyako na wengine hawastahili; bali tunahitaji kuwa wenyenyekevu na kuweka matakwa ya wengine mbele zaidi katika kuleta maisha ya upendo wa kweli miongoni mwenu na kufanikisha amri ya upendo wa kuishi pamoja. Ni jambo gumu ambalo linasumbua katika utekelezaji wake. Maisha yetu yamejaa choyo, umimi, wivu na unafiki; ni neema tu itakayo tusaidia kutekeleza dhana ya kuishi kwa pamoja kama ndugu kama tutaweza kusoma na kuelewa nyakati za Mungu na maarifa yake, katika kutekeleza upendo wa kweli .

Hii ndio tafakari yetu ya leo; Amina

Emmanuel Turuka



Sunday, May 1, 2016

TUMSHUKURU BWANA KWANI NI MWEMA


mAY 1

ZABURI YA 107


Tafakari ya leo tunakila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake na kwa Kutujalia kuweza kuanza Mwezi Mpya wa May tukiwa na tunaendelea kufunikwa na damu ya Mkombozi wetu, na kuendelea kuneemeka na baraka na neema zake katika maisha yetu ya kila siku. Mzaburi ametuonyesha njia zote ambazo Mungu anatusaidia kama alivyowasaidia wana wa Israeli  kutoka katika mikono ya Farao na kuwalisha na kuwannemesha wakati wote wa safari kwenda katika makazi mapaya. Je wewe na mimi tunaendelea kumshukuru Mungu kila siku?

1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. 

Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. 

Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. 

Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. 

Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. 

Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. 

Akawaongoza kwa njia ya kunyoka, Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa. 

Na wamshukuru Bwana, kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. 

Maana hushibisha nafsi yenye shauku, Na nafsi yenye njaa huijaza mema. 

10 Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma, 

11 Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu. 

12 Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi. 

13 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. 

14 Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao. 

15 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. 

16 Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma. 

17 Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa. 

18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti. 

19 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. 

20 Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. 

21 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. 

22 Na wamtolee dhabihu za kushukuru, Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba. 

23 Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, 

24 Hao huziona kazi za Bwana, Na maajabu yake vilindini. 

25 Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake. 

26 Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya. 

27 Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea. 

28 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. 

29 Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. 

30 Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani. 

31 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. 

32 Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee. 

33 Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu. 

34 Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa. 

35 Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji. 

36 Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa. 

37 Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake. 

38 Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao. 

39 Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni. 

40 Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia. 

41 Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo. 

42 Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa. 

43 Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.
Hii ndio tafakari yetu ya leo; Amina
Emmanuel Turuka